- Injinia Hersi anaondoka au bado yupo Yanga? Ndilo swali kubwa ambalo wanajiuliza mashabiki wa timu hiyo.
- Hii ni mara baada ya kiongozi huyo kujitosa kwenye ulingo wa siasa akiweka nia ya kugombea ubunge wa Kigamboni.
- Hersi kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa Rais wa Yanga mwaka 2022.
Injinia Hersi anaondoka au bado yupo Yanga? Ndilo swali kubwa ambalo wanajiuliza mashabiki wa timu hiyo mara baada ya kiongozi huyo kuingia kwenye ulingo wa siasa. Hersi tayari ametangazwa kuchukua fomu ya mtia nia kwa ajili ya kugombea ubunge jimbo la Kigamboni, jijini Dar es Salaam.

Kuhusu Hersi na uongozi wake ndani ya Yanga

Injinia Hersi kwa mara ya kwanza alichaguliwa kuwa Rais wa Yanga mwaka 2022, akiwa ndiye mgombea pekee wa nafasi hiyo ambapo yeye pamoja na makamu rais wake, Arafat Haji wamekuwa na uongozi wenye mafanikio makubwa wakishinda mataji manne mfululizo ya ligi Kuu ya NBC.
Pamoja na mafanikio hayo, Injinia Hersi pia amefanikiwa kuiongoza timu hiyo kufanikiwa kuwa washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika na kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.
SOMA NA HII PIA: Tetesi usajili ligi Kuu ya NBC 2025/26 wanaoondoka Yanga hawa hapa
Achaguliwa kuwa Mwenyekiti wa vilabu Afrika

Mwaka 2023 Shirikisho la Soka Afrika (CAF), usiku wa kuamkia Decemba 1, ulizindua Chama cha vilabu vya soka Barani Afrika (ACA), huku likimchagua Mtanzania na Rais wa klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chama hicho chenye makao yake makuu Morocco.
Katika majukumu hayo, Injinia Hersi anasaidiwa na Jessica Motaung wa Kaizer Chiefs kama makamu Mwenyekiti huku Paul Basset wa Akwa United ya Nigeria akichaguliwa kuwa makamu Mwenyekiti wa pili.
Uzinduzi huo uliofanyika Nchini Misri umesimamiwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe nchini, huku Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Simba SC wa wakati huo, Salim Try Again akiwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.
SOMA HII PIA: Yanga SC kupeleka kombe la ubingwa wa ligi ya NBC Ikulu
Ajitosa ulingo wa siasa kwenye Uchaguzi mkuu 2025
Mara baada ya kuwa na mafanikio makubwa kwenye uongozi wa soka, Hersi mwaka huu ukiwa ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa wabunge, madiwani na Rais ameamua kujitosa kwenye ulingo wa siasa kwa kuweka nia ya kugombea ubunge wa jimbo la Kigamboni
Je, Hersi ataondoka Yanga?
Kufuatia hatua zinazoendelea za uchaguzi, Wanayanga wamekuwa na wasiwasi wakijiuliza ikiwa ikiwa Rais wao atashinda ubunge wa Kigamboni, Je ataachia nafasi ya Urais wa Yanga? Hali iliyomlazimu kiongozi huyo kutoa tamko.
Kupitia kilele cha shamrashamra za ‘Parade’ a ubingwa Hersi alizungumza na mashabiki wa Yanga na kusema: “Najua wote mmeona kuwa makamu wetu Arafat nami tumechukua fomu kuweka nia ya kugombea ubunge, mnajiuliza kama tutaondoka au vipi.
“Niwahakikishie kuwa Yanga siku zote itakuwa imara hata sisi tusipokuwepo, tuna taasisi ambayo anayeondoka atarithiwa na mtu bora zaidi hii ndiyo falsafa yetu. Niliwaahidi makombe nimeleta, niliwaahidi nguvu ya kiuchumi na hatujatetereka.
“Niwahakikishie mazuri mengi yanakuja. Lipo moja niliwaahidi ambalo bado sijatekeleza n ani kuhusu ujenzi wa Uwanja wetu hapa Jangwani. Nataka kuwaambia Serikali imeruhusu kutuongezea eneo na hivi karibuni tutaanza rasmi ujenzi wa Uwanja huo. Viongozi wenu tupo imara na hatutaacha mtetereke.”
Kuhusu Parade la ubingwa

Mara baada ya kuwa na msimu wa mafanikio, wakifanikiwa kushinda mataji matano kwa msimu wa 2024/25, uongozi wa Yanga jana Jumatatu uliandaa msafara wa kusherehekea mafanikio hayo, msafara ambao ulikuwa gumzo jijini Dar es Salaam.
Mashabiki wa Yanga SC walijitokeza kutoka kila kona kuungana na msafara huo na funga kazi ilikuwa makao makuu ya Yanga SC, Jangwani Dar, ambapo Viongozi na wachezaji walionekana kuwa kwenye furaha ya juu wakikamilisha msimu wakiwa na mataji matano kabatini.
SOMA HII PIA: Pacome wa Yanga SC na Jean Ahoua wa Simba SC vita yao waliimaliza kibabe/ MVP kazi ipo
Safari ilianzia Zanzibar kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB

Juni 29 2025, Yanga SC ilitwaa taji la CRDB Federation Cup kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex. Taji hilo likikamilisha idadi ya mataji matano kwa msimu wa 2024/25.
Yanga waliiendea fainali hiyo mara baada ya kufanikiwa kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC kufuatia ushindi wa aina yake kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba SC ambapo Wananchi walipata ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Mkapa, Juni 25 2025.
Msafara waanzia Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa JK Nyerere
Mara baada ya kutoka Zanzibar, Yanga walirejea Dar, Juni 30 2025 na kufanya Parade la Kihistoria ambalo lilianzia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kuanzia saa 4:00 asubuhi na kufikia tamati majira ya saa tatu usiku kwenye viunga vya Jangwani.
Vituo ambavyo Parade la Kihistoria la Yanga SC iliyotwaa makombe matano msimu wa 2024/25 ilikuwa ni AirPort Terminal 1, Tazara, Keko, Karume, Msimbazi kwa watani zao wa jadi Simba SC na Jangwani.
Jangwani kulikuwa na shughuli ya burudani miongoni mwa wasanii waliowapa burudani Wananchi ni Mbosso Khan anayetamba na wimbo wake wa Aviola na alitambulishwa kuwa Mwananchi rasmi. Mbosso aliwashukuru Yanga SC na mashabiki kwa kumpokea. Aliwapa burudani Wananchi waliojitokeza kwa wingi.
Shinda mamilioni na Kindege cha SporPesa
Ukienda kuburudika na kuhabarika kwa makala kali za SportPesa, kumbuka unaweza kujishindia mamilioni kwa kucheza mchezo wa kindege ‘Aviator’ ya Kampuni ya SportPesa kwa kubonyeza picha hii chini.


