- Yanga SC vs Simba SC Juni 25 2025 matukio makubwa mawili kufanyika ndani ya siku moja Uwanja wa Mkapa.
- Waamuzi wa Kariakoo Dabi kutoka mataifa matatu, haijawahi kutokea ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
- Simba SC hawana chaguo kutwaa ubingwa lazima washinde, Yanga SC pointi moja ama tatu ubingwa wanaubeba.
Yanga SC vs Simba SC matukio mawili makubwa kufanyika mchezo wa funga kazi ndani ya msimu wa 2024/25 Juni 25 2025. Watani hawa wa jadi wanakutana Uwanja wa Mkapa wakiwa tofauti ya pointi moja baada ya mechi 29. Yanga SC ambao ni mabingwa watetezi wana pointi 79 na Simba SC nafasi ya pili wakiwa na pointi 78.

Soma hii: Yanga SC vs Simba SC vita ya ubingwa bado inaendelea
Matukio mawili makubwa Yanga SC vs Simba SC
Matukio mawili makubwa yanatarajiwa kufanyika kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi. Juni 25 2025 Uwanja wa Mkapa utakuwa kwenye kazi nzito kwa wababe wawili kukutana. Ni Yanga SC amba oni wenyeji dhidi ya Simba SC.
Huu unakuwa ni mchezo wa mzunguko wa pili msimu wa 2024/25. Ikumbukwe kwamba katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Yanga SC ilishinda. Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba SC 0-1 Yanga SC.

Matukio mawili makubwa yanayotarajiwa ni mchezo wenyewe wa Kariakoo Dabi. Pili ni tukio la sherehe za ubingwa baada ya dakika 90 kukamilika. Mshindi wa mchezo wa Juni 25 2025 ana uhakika kutwaa ubingwa na furaha mbili, kumfunga mtani na kutwaa ubingwa mbele ya mtani.
Huyu hapa Boimanda Ofisa Habari TPLB
Kwa mujibu wa Karim Boimanda, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi Tanzania, (TPLB) ameweka wazi kuwa mara baada ya mchezo huo kutamatika kutakuwa na sherehe za kukabidhi kikombe cha ubingwa.
“Tumekuwa na msimu mzuri na wenye ushindani mkubwa jambo ambalo limeongeza ushindani na mchezo wa Kariakoo Dabi ni mkubwa na unawavutia watu kutoka ndani na nje ya nchi.
“Unaona tumemaliza mpaka mzunguko wa 30 kwa timu zote kucheza tukisaliwa na mchezo mmoja ambao uliahirishwa. Lakini mbali na mchezo huo wa ligi ambao ni mchezo mmoja ambao umesalia baada ya kutamatika kwa mchezo huo kutakuwa na sherehe za kukabidhi kikombe cha ubingwa.
“Mabingwa wa NBC 2024/25, wapya watajulikana. Tulikuwa na msimu mzuri ambao hauhitaji kujielezea kutokana na mechi zote kuchezwa na bado hakuna bingwa. Wanakutana wakiwa na tofauti ya pointi moja.
“Sasa tuna matukio makubwa mawili ambayo yanakwenda kutengeneza kitu kikubwa ndani ya siku moja. Mchezo wa Kariakoo Dabi wenyewe ambao ni mkubwa. Pili ni kitendo cha kukabidhi kikombe cha ubingwa.” amesema Boimanda.
Waamuzi kutoka Misri, Somalia na Tanzania

Soma hii:Sakata la kuyeyuka Kariakoo Dabi Machi 8 2025, Sababu Zipo Hivi – SportPesa Tanzania
Waamuzi katika mchezo wa Kariakoo Dabi Juni 25 ni kutoka mataifa matatu, Tanzania, Misri na Somalia. Hivyo watashirikiana kwenye maamuzi ndani ya dakika 90. Hii ni kwa mara ya kwanza msimu wa 2024/25 tukio la waamuzi wageni linafanyika Tanzania.
Mwamuzi wa kati ni Amin Mohamed Amin Omar kutoka Misri. Match Commissioner ni Salim Omary Singano kutoka Tanga na Referees Assessor ni Alli Mohamed kutoka Somalia. Mzunguko wa kwanza mwamuzi alikuwa Ramadhan Kayoko ambaye ni Mtanzania. Kwenye mchezo uliotarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 ni Ahmed Arajiga alitangazwa kuwa mwamuzi wa mchezo huo.
Hii hapa bei ya viingilio

Soma hii: Mechi namba 184 Yanga SC vs Simba SC ni pasua kichwa
Bei ya viingilio Kariakoo Dabi mechi namba 184 Juni 25 2025 imewekwa wazi. Kwa mujibu wa Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC amesema VIP A tayari tiketi zimekwisha. Kamwe amewaomba mashabiki kumalizia hizo ambazo zimebaki.
“VIP A – 50,000 (sold out), VIP B – 30,000, VIP C – 20,000, Orange – 10,000 na mzunguko ni 5,000. Mashabiki tunawaomba mjitokeze kwa wingi kwenye mchezo wetu muhimu.”
N Card watoa ufafanuzi kadi ambazo zilitumika
Catherine Chammy Kutoka N-Card ameweka wazi kuwa kuhusu tiketi ambazo zilitumika Juni 15 2025 kabla ya mechi kuahirishwa na kupangiwa siku nyingine ambayo ni Juni 25 zitatumika zilezile. Ikumbukwe kwamba awali mchezo huu ulitarajiwa kuchezwa Machi 8 ukaahirishwa. Mara ya pili ulitarajiwa kuchezwa Juni 15 ukaahirishwa na tarehe ambayo imepangwa kwa sasa ni Juni 25 2025.
Catherine amesema: “Kuna jambo moja la mashabiki wetu ambao walikata tiketi zikatumika siku ya tarehe 15. Kwa tiketi zote ambazo zilitumika N Card tuna utaratibu wa ndani, kwa mashabiki ambao walikuja na kuingia getini N Card kadi zilezile zitatumika. Kwa wale ambao hawana kumbukumbu ya namba zao lazima wawe wanakumbuka namba za tiketi ili kufanyiwa swap vizuri hivyo atakachotoa ni 1000 kwa ajili ya kununua kadi ila tiketi yake ipo salama.
“Kwa wale ambao hawajanunua tiketi mpaka muda huu wanunue. Ila VIP A tayari imeshaisha hilo lipo wazi. Ni Orange na VIP C tiketi bado zipo.”
Simba SC ili itwae ubingwa lazima ishinde mchezo wa Juni 25. Yanga SC akipata pointi moja ama pointi tatu kwake ni faida. Yanga SC mchezo wa mzunguko wa kwanza ilivuna pointi tatu ikiwa ugenini mbele ya Simba SC.

