- Tanzania Prisons 0-5 Yanga SC dakika 180 wapigwa nje ndani kwenye mechi za ligi, Kariakoo Dabi inakuja Juni 25 2025.
- Yanga SC yajikita kileleni na pointi zake 76 na safu ya ushambuliaji imetupia mabao 76 ikiwa ni timu namba moja kufunga mabao mengi.
- Clatous Chama afanya maajabu akitokea benchi kwa kupachika bao dakika tatu zikipita baada ya Mudathir Yahya kufunga bao la ufunguzi.
Tanzania Prisons 0-5 Yanga SC dakika 180 wapigwa nje ndani msimu wa 2024/25 katika msako wa pointi tatu muhimu. Jumla Yanga SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi imeifunga Tanzania Prisons mabao 9 huku safu ya ushambuliaji ya Prisons ikikwama kufunga mbele ya Yanga SC. Mechi mbili zimebaki kwa Yanga SC huku unaosubiriwa kwa shauku ni ule wa Kariakoo Dabi, Juni 25 2025.

Soma hii: Ibenge & Maxi watikisa taarifa mpya usajili Bongo
Juni 18 2025 ulikuwa ni mchezo wa mzunguko wa pili msimu wa 2024/25. Katika dakika 15 za mwanzo Tanzania Prisons ilikuwa imara kwenye kujilinda huku ikifanya mashambulizi ya kushtukiza jitihada hizo ziligotea kwenye kichwa cha Mudathir Yahya ambaye alitibua rekodi hiyo.
Yanga SC ushindi huo unaifanya ijikite kileleni ikiwa imekusanya jumla ya pointi 76 baada ya kucheza mechi 28 ambazo ni dakika 2,520 ndani ya msimu wa 2024/25. Yanga SC ina wastani wa kuwa na hatari yakufunga bao moja kila baada ya dakika 33 ndani ya ligi kwa kuwa imefunga mabao 76.
Idadi ya pointi ambazo imekusanya Yanga SC kibindoni ni sawa na idadi ya mabao ambayo imefunga kwenye ligi ikiwa ni timu namba moja kufunga mabao mengi. Simba SC inafuatia kwenye timu zenye mabao mengi ambayo ni 68.
Tanzania Prisons walitulizwa namna hii na Yanga SC
Kwenye mchezo dhidi ya Yanga SC, Tanzania Prisons wakiwa nyumbani Uwanja wa Sokoine walishuhudia ukurasa wa mabao ukifunguliwa na kiungo Mudathir Yahya ilikuwa dakika ya 31 ya mchezo kipindi cha kwanza. Mudathir alipachika bao hilo kwa pigo la kichwa akitumia pasi ya Israel Mwenda aliyepiga pasi hiyo kwa mguu wa kulia akiwa nje ya 18.

Soma hii: Yanga SC wanazitaka pointi tatu za Tanzania Prisons Juni 18 2025
Clatous Chama ambaye aliingia dakika ya 22 akichukua nafasi ya Prince Dube alipachika bao la pili dakika ya 35 zikiwa zimeyeyuka dakika tatu tangu bao la kwanza kwa Yanga SC kufungwa kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Pacome Zouzoua alifunga mabao mawili dakika ya 56 na 76 katika mchezo huo na alichaguliwa kuwa mchezaji bora baada ya dakika 90 kugota mwisho, Israel Mwenda alipachika bao moja ambalo lilikuwa la nne dakika ya 60 na alionyeshwa kadi ya njano kwa kuvua jezi wakati anashangilia baada ya kufunga bao hilo.
Mzunguko wa kwanza Yanga SC walikomba pointi tatu
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Desemba 22 2024 walipokutana Uwanja wa KMC Complex ulisoma Yanga 4-0 Tanzania Prisons. Mzunguko wa pili Tanzania Prisons 0-5 Yanga SC Juni 18 2025. Tanzania Prisons wameshindwa kufurukuta mbele ya Yanga ndani ya dakika 180.

Ni mabao 9 Yanga SC imeifunga Tanzania Prisons msimu wa 2024/25 wakikomba pointi sita jumla kwa kushinda nje ndani kwenye mechi ambazo walikutana huku safu ya ushambuliaji ya Prisons ikikwama kufunga bao mbele ya Yanga SC.
Msimamo Tanzania Prisons vs Yanga SC
Yanga SC kwenye msimamo ni namba moja ikiwa na pointi 76 baada ya kucheza mechi 28. Mechi mbili zimebaki kwa timu hiyo kukamilisha mzunguko wa pili. Mchezo ujao ni Juni 22 dhidi ya Dodoma Jiji na Juni 25 itakuwa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba SC.
Tanzania Prisons ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 30 inapambana kujinasua kwenye nafasi ya kucheza play off baada ya mechi 29 ina kete moja mkononi kukamilisha mzunguko wa pili. Safu ya ushambuliaji ya Yanga SC imefunga mabao 76 ni timu namba moja kufunga mabao mengi huku Prisons safu ya ushambuliaji imetupia mabao 23 ikiwa ni miongoni mwa timu ambazo hazijawa imara kwenye eneo la ushambuliaji ndani ya msimu wa 2024/25.

Soma hii: Yanga SC vs Simba SC kwenye msako wa pointi tatu ndani ya ligi Juni 18/ Mechi namba 184 kimbembe
Mchezo ujao kwa Tanzania Prisons kukamilisha mzunguko wa pili itakuwa dhidi ya Singida Black Stars. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Juni 22 Uwanja wa Liti. Singida Black Stars ipo nafasi ya 4 ikiwa na pointi 56 baada ya mechi 29.
Hiki hapa kikosi cha Yanga SC dhidi ya Prisons
Djigui Diarra, Israel Mwenda, Boka, Job Dickson, Ibrahim Bacca. Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Clement Mzize. Hawa ni wachezaji ambao walianza kikosi cha kwanza na wachezaji wa akiba ilikuwa ni Mshery Aboutwalib, Kibwana Shomari, Kibabage, Nondo, Juma, Andambilwe, Shekhan, Abuya, Chama, Ikanga Lombo.

