KasongoKasongo
  • Mechi namba 184 Yanga SC vs Simba SC ni pasua kichwa kutokana na kupigwa kalenda kwa mara nyingine kutoka Juni 15 mpaka Juni 25 2025.
  • Almasi Kasongo CEO Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, (TPLB) amesimamishwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Wallace Karia.
  • Steven Mguto, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara awasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa wake.

Mechi namba 184 Yanga SC vs Simba SC ni pasua kichwa kutokana na kupigwa kalenda kwa mara nyingine tena huku baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu kwenye masuala ya usimamizi wa mpira Tanzania kuwa kando muda mfupi baada ya tarehe mpya ya mchezo kutajwa.

Ateba v Aucho
Ateba v Aucho kwenye Kariakoo Dabi mzunguko wa kwanza.Source: Simba SC.

Ikumbukwe kwamba Juni 9 2025 Yanga SC kupitia kwa Ofisa Habari Ali Kamwe waliweka wazi kuwa hawatacheza mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Simba SC mpaka matakwa yao manne yatimizwe na wakabainisha kuwa ikiwa hayatatimizwa hawatashiriki ligi msimu ujao wa 2025/26.

Mchezo huo ambao uliyeyuka Machi 8 2025, ulipangiwa tarehe mpya ambayo ni Juni 15 2025, Simba SC walikuwa kwenye maandalizi huku Yanga SC ambao ni wenyeji wa mchezo huo wakibainisha kuwa hawapo tayari kwa mchezo huo.

image
image

Juni 13 2025 taarifa kutoka TPLB ilieleza kuwa mchezo huo uliotarajiwa kuchezwa Juni 15 2025 ambayo ni Jumapili saa 11:00 jioni umepelekwa mbele mpaka Julai 25 kwa watani hao wa jadi Yanga SC vs Simba SC kukutana uwanjani kusaka pointi tatu.

Karim
Karim Boimanda, Ofisa Habari TPLB.

Isome hii:Yanga SC vs Simba SC ni Juni 25 2025 sio Juni 15 2025

Muda mfupi baada ya tarehe mpya ya mchezo wa Kariakoo Dabi kutangazwa, ilitolewa taarifa kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambayo ilisema Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) Steven Mguto amewasilisha barua ya kujiuzulu wadhfa wake huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 13 2025 na TFF, Rais Wallace Karia, amemsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almasi Kasongo. Taarifa hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao. Ikumbukwe kwamba Kasongo alikuwa kwenye sakata la kutakiwa kujiuzulu na uongozi wa Yanga SC ambao ulitoa matakwa manne ili ucheze mchezo wao dhidi ya Simba SC ulioahirishwa Machi 8 2025.

Jikumbushe maneno ya Kasongo kabla ya kusimamishwa

“Wenzetu wamekuja na mambo manne ambayo sisi kama bodi tuna wajibu wa kupokea na kuyachakata, sio kupokea tu na kuyachakata. Azimio la kwanza kuvunjwa kwa kamati ya usimamizi na uendeshaji ya bodi ya ligi. Kuna kamati ya kusimamia na kuendesha ligi ipo kwenye kanuni.

“Jambo la pili kujiuzulu kwa ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, jambo la tatu kujiuzulu kwa katibu Mkuu wa TFF na jambo la nne bodi ya ligi iwe chombo huru. Itoshe kusema kuwa tumepokea lakini haya mambo yote manne yapo nje ya uwezo wa Mwenyekiti wa Bodi, mamlaka ya utendaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu ndio wana uwezo kuyafanyia kazi na tutapeleka kwenye mamlaka husika.

“Kama nilivyotangulia kusema kwa haya waliyoyaleta tumeyapokea ila yapo nje ya uwezo wetu tuna mamlaka ya kuwasilisha kwa mamlaka inayohusika ili kuyafanyia maamuzi. Kwa yale ambayo yapo ndani ya uwezo wetu ikiwa ni ratiba sisi ratiba yetu ipo kama ilivyopangwa kwa sababu chombo kinachoendesha na kusimamia ligi ni chombo kingine.

“Ratiba yetu tulisema kuwa mechi namba 184 itachezwa Juni 15 2025, sisi tuna wajibu kupeleka hoja katika mamlaka husika, ratiba ipo vilevile mpaka kamati itakapotoa taarifa nyingine. Yanga SC nafasi yao ni kwamba wangetamani haya yafanyike ili warudi kwenye mchezo, ukitazama haya yanawezekana lakini haitakuwa kwa siku moja ni mchakato ambao unahusisha kamati nyingi. Ukiyatazama maazimip yapo nje ya mamlaka ya bodi ya ligi.” Almas Kasongo aliyekuwa CEO bodi ya ligi.

Kinachofuata kwa sasa ni mshikemshike

Ateba na Diarra
Ateba na Diarra, mzunguko wa kwanza 2024/25. Source: Simba SC.

Isome hii: Yanga SC vs Simba SC iliyopangwa Juni 15 2025: Ngoma imekuwa ngumu, Yanga yatishia maamuzi magumu

Kinachofuata kwa sasa ni mshikemshike kuelekea mzunguko wa 29 na 30 katika kukamilisha msimu wa 2024/25 huku mchezo namba 184 ukiwa ni kiporo kitakachochezwa baada ya mechi zote kukamilika Yanga SC wamecheza mechi 27 ni nafasi ya kwanza kwenye msimamo wakiwa na pointi 73 wanafuatiwa na Simba SC wenye pointi 72 kwenye msimamo. Mchezo wa Juni 25 unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa pande zote mbili.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Yanga SC ikiwa ugenini iliifunga bao 1-0 Simba SC na kusepa na pointi tatu mazima, mbabe mwingine anatafutwa kwenye mchezo huo unasosubiriwa kwa shauku kubwa. Simba SC bado hawajatoa taarifa rasmi kuhusu mchezo huo ila inaelezwa kuwa wapo tayari kwa maandalizi ya mchezo wa mzunguko wa pili baada ya ule wa awali Machi 8 2025 kuyeyuka mazima.

Share this: