Bacca v AtebaBacca v Ateba
  • Simba SC yawatoa mashaka mashabiki yabainisha Kariakoo Dabi itachezwa Juni 15 2025 Uwanja wa Mkapa.
  • Yanga SC msimamo wao ni matakwa manne kutimizwa hapo watacheza Kariakoo Dabi tarehe nyingine itakayopangwa.
  • TPLB wafungukia kuhusu tarehe na matakwa ya Yanga SC kufika mezani.

Simba SC yawatoa mashaka mashabiki yabainisha Kariakoo Dabi itachezwa Juni 15 2025, Uwanja wa Mkapa kwa watani wa jadi kukutana uwanjani kwenye mchezo wa msako wa pointi tatu muhimu ndani ya uwanja ikiwa ni mzunguko wa pili msimu wa 2024/25.

Bacca na Ateba
Bacca na Ateba mzunguko wa kwanza 2024/25. Source: Simba SC.

Isome hii: Kariakoo Dabi mchezo wa watani wa jadi Yanga SC vs Simba mechi ipo Juni 15 2025

Mchezo huo awali ulipangwa kucheza Machi 8 2025 uliahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu ambapo walibainisha kuwa watapanga tarehe mpya ya mchezo huo namba 184 kwa watani wa jadi kukutana uwanjani. Meneja Idara wa Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa wanaendelea na maandalizi ya mchezo huo hivyo mashabiki wasiwe na mashaka mchezo upo kwa mujibu wa bodi ya ligi.   

“Simba SC tunafanya maandalizi makubwa ni maandalizi kabambe kuelekea mechi yetu ya tarehe 15 kwa sababu ni mechi ambayo lazima sisi viongozi lazima tuichukue kwa ukubwa wake na itatukutanisha na watani zetu wa jadi. Ni mechi ambayo lazima tuifanyie maandalizi makubwa kwa kuwa tunakutana na mpinzani wetu mkubwa katika nchi hii ambaye tunawania naye ubingwa wa ligi.

“Lakini wapo Wanasimba wengine ambao wanayumbayumba lakini ninapenda kuwathibitishia hii kwa Wanasimba kuwa mechi yetu namba 184 ipo palepale siku ya Jumapili. Kwa mujibu wa bodi ya ligi Tanzania imethibisha hivyo kwa maneno na kimaandishi.

Ahmed
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC. Source: Simba SC.

“Wanasimba wasiwe na mashaka mashaka wasiwe na wasiwasi wowote mechi ipo palepale benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Fadlu Davids kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu Uwanja wa Mkapa kwa kuwa imethibitishwa kimaandishi saa 11 Juni 15 2025 Uwanja wa Mkapa. Sisi viongozi tunafanya maandalizi na wachezaji kiujumla wapo kambini kwa sasa kuendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo.”

Haya hapa matakwa ya Yanga SC

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC, Juni 9 2025 alibainisha wazi kuhusu matakwa yao manne ambayo wanahitaji yafanyike ili wacheze mchezo wa Kariakoo Dabi na ikitokea hayatafanyika msimamo wao ni kutocheza mchezo huo.

“Takwa letu la kwanza na la pili linahusu ukiukwaji wa kanuni uliofanyika Machi 8. Tunataka Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi pamoja na CEO wa Bodi ya Ligi Almasi Kasongo wawajibike kwa kujiuzulu kwa kushindwa kusimamia kanuni na kuutia doa mpira wetu. Ligi yetu ni kubwa sana Afrika na inataka watu makini wenye weledi kuiongoza.

“Kuahirishwa kwa mechi ya Machi 8 tunaamini kama klabu hapakufuatwa utaratibu na kulikuwa na uvunjaji mkubwa wa kikanuni hivyo tunaamini CEO wa Bodi ya Ligi na kamati ya uedeshaji wa kamati ya ligi ilifanya hayo kwa ajili ya kuwapa favour timu fulani. Klabu ya Yanga SC haitakuwa tayari kushiriki mechi namba 184 kama kamati nzima ya uendeshaji na usimamizi wa bodi haitajiuzulu au kuvunjwa.

Ali Kamwe - Ofisa habari Yanga
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC. Source: Yanga SC.

Isome hii:Yanga SC wametoa matakwa manne yakitimizwa Kariakoo Dabi kuchezwa

“Takwa letu la tatu ni kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya maamuzi mabovu ya mara kwa mara ya waamuzi. Kamati ya waamuzi ipo chini ya TFF kwa Katibu Mkuu, unashangaa ni vipi mwamuzi mmoja anafanya makosa yakujirudia na bado anaendelea kupangwa kwenye mechi bila kuchukuliwa adhabu yoyote ile.

“Napenda kuwajuza waandishi wa Habari, yasipofanyiwa kazi matakwa yetu matatu kwa uharaka, Yanga SC hatutakuwa tayari kucheza mchezo namba 184, mechi zote mbili za Ligi zilizobaki na hatutashiri Ligi Kuu Msimu ujao. Huu ndio msimamo wetu na hatutayumba kwa lolote.

“Taarifa hii iwafikie ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF na Wadhamini wa mashindano ya Kombe la Shirikisho, kuwa hatutacheza mchezo wa Fainali wa CRDB siku ya tarehe 28, mpaka tutakapolipwa hela yetu ya Ubingwa kwa msimu uliopita. Tumevumilia dharau hizi kutoka kwa Mamlaka za Soka kwa muda mrefu sana, sasa imefika mwisho. Hii ya Zanzibar pia hatuchezi.

Bosi Bodi ya Ligi huyu hapa

Kasongo
Kasongo CEO bodi ya ligi. Source: TFF.

Isome hii: Yanga SC vs Simba SC iliyopangwa Juni 15 2025: Ngoma imekuwa ngumu, Yanga yatishia maamuzi magumu

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, (TPLB) Almas Kasongo hivi karibuni aliweka wazi kuwa matakwa ambayo yamepelekwa na Yanga SC wameyapokea na yale ambayo yapo kwenye uwezo wao watayafanyia kazi na yale ambayo yapon je ya uwezo wao watapeleka mahali husika kwa ajili ya mchakato kufanyika kwa kuwa kila idara ina kazi yake.


“Ratiba yetu tulisema kuwa mechi namba 184 itachezwa Juni 15 2025, sisi tuna wajibu kupeleka hoja katika mamlaka husika, ratiba ipo vilevile mpaka kamati itakapotoa taarifa nyingine. Yanga SC nafasi yao ni kwamba wangetamani haya yafanyike ili warudi kwenye mchezo, ukitazama haya yanawezekana lakini haitakuwa kwa siku moja ni mchakato ambao unahusisha kamati nyingi. Ukiyatazama maazimip yapo nje ya mamlaka ya bodi ya ligi.”

Share this: