- Dikcson Job chaguo la kwanza ndani ya kikosi cha Yanga SC upande wa ulinzi jina lake linatajwa kuwa mitaa ya Msimbazi kwa watani zao wa jadi Simba SC.
- Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC inaelezwa kuwa kuna timu ambayo inahitaji huduma yake hivyo ataondoka Bongo.
- Azam FC beki wao mwenye uwezo wa kupanda na kushuka Pascal Msindo kuna mabosi watavunja beki kuipata saini yake.
Dickson Job beki wa Yanga SC jina lake linatajwa kuwa katika rada za Simba SC ambayo inanolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini. Wakati akitajwa kuwa katika hesabu za watani wao wa jadi Simba SC kuna taarifa kuwa tayari ameanza mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya mitaa ya Jangwani kwa mabosi zake Yanga SC.

Job alitambulishwa ndani ya Yanga SC akitokea Mtibwa Sugar, wakati wa usajili wake kulikuwa na mvutano mkubwa kwa mapacha hawa wa Kariakoo na ilikuwa inatajwa kuwa Simba SC nao walikuwa kwenye hesabu za kuinasa saini yake.
Kuelekea kugota mwisho wa msimu wa 2024/25, taarifa zinaeleza kuwa mkataba wa Job unatarajiwa kufika ukingoni jambo ambalo linawapa nguvu watani zao wa jadi Simba SC kuanza kufanya mazungumzo na mchezaji huyo hivyo ikiwa mazungumzo yatakwenda vizuri anaweza kusaini kandarasi kwa watani hao wa jadi.
Ikumbukwe kwamba watani hao wa jadi Yanga SC tayari wamemuuza mchezaji mmoja ambaye ni Aziz Ki huyu yupo zake Wydad Casablanca kwa sasa kwa ajili ya changamoto mpya na kuna orodha ya wachezaji wengine ambao wanatajwa kuhitajika na timu nyingine kutokana na uwezo walionao.
Soma na hii:Fadlu Davids Kocha Mkuu wa Simba SC anatajwa Raja Casablanca
Mbali na Job kuna tetesi nyingine ambazo zinawahusu wachezaji mbalimbali kuhitajika katika timu nyingine hapa tunakuangazia baadhi yao namna hii ikiwa ni tetesi kwa sasa:-
Jean Ahoua wa Simba SC atajwa Kaizer Chiefs

Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Jean Ahoua anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Ahoua ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids. Ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika, Ahoua ni namba moja kwenye chati ya wakali wakufunga mabao mengi kwenye mechi za ushindani msimu wa 2024/25.
Ahoua ni mabao 15 kafunga akiwa anashikilia chati namba moja kwa wakali wakucheka na nyavu. Mbali na kufunga mabao 15 kiungo huyo katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao. Pasi yake ya 8 alitoa kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars.
Mchezo huo ulikuwa wa ligi ulichezwa Uwanja wa KMC Complex, alitoa pasi hiyo kwa Steven Mukwala ambaye alipachika bao la ushindi lililoipa pointi tatu Simba SC. Kutokana na ubora alionao anatajwa kuwa kwenye rada za Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Jonathan Sowah wa Singida Black Stars
Yupo ndani ya kikosi cha Singida Black Stars Jonathan Sowah akiwa katuma jumla ya mabao 11 msimu wa 2024/25. Kwenye mabao ambayo amefunga Sowah hayo 11 alimfunga pia kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra katika mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa KMC Complex. Mshambuliaji huyu anatajwa kuwa kwenye rada za Simba SC na Yanga SC.
Ally Salim anatajwa Mbeya City

Kipa namba mbili wa Simba SC, Ally Salim anatajwa kuwa anahitajika kwa mkopo ndani ya Mbeya City. Salim hana nafasi kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa Moussa Camara ambaye ni kipa namba moja wa Simba SC.
Alipoumia Camara kwenye mchezo dhidi ya Singida Black Stars, nusu fainali CRDB Federation Cup, Salim aliingia na alifungwa mabao mawili kwenye mchezo huo wakati Simba SC ikifungashiwa virago kwenye mashindano hayo makubwa.
Gibrli Sillah anatajwa Yanga SC
Kiungo mshambuliaji wa Azam FC ambaye yupo kwenye viunga vya matajiri wa Dar, anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Jangwani, Yanga SC. Sillah ana uwezo kwenye kufunga na kutengeneza nafasi za mabao ambapo kwa msimu wa 2024/25 kafunga mabao 9 na kutengeneza pasi mbili za mabao amekuwa akitajwa kuwa katika hesabu za Yanga SC inayomtafuta mbadala wa kiungo Aziz Ki.
Soma hii:Baada ya Aziz Ki: Mzize na Aucho wanaondoka Yanga? Tetesi usajili bongo
Ibrahim Keita wa TP Mazembe anatajwa Yanga
Ibrahim Keita ni mlinzi wa kulia ambaye mkataba wake na timu ya TP Mazembe unakaribia kufika mwisho na inaelezwa kuwa hayupo tayari kuongeza kandarasi nyingine. Singida Black Stars walianza kuulizia saini ya nyota huyo kisha Yanga SC wakafuata kuulizia ili kuinasa saini yake.
Pascal Msindo anatajwa Simba SC
Beki wakupanda na kushuka ndani ya kikosi cha Azam FC, Pascal Msindo anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Simba SC ambao wanahitaji kuongeza nguvu kwenye upande wa ulinzi ndani ya kikosi hicho. Ni miongoni mwa mabeki wenye uwezo wakufunga pia jambo ambalo litakuwa faida kwenye timu itakayompata.
Ikiwa Simba SC watakuwa wanahitaji huduma ya beki huyo wanapaswa kuvunja benki kwa kuwa nyota huyo aliongeza mkataba kuendelea kuwatumikia matajiri wa Dar, Azam FC ambao wanatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi za nyumbani.

