Kagoma vs RS BerkaneKagoma vs RS Berkane
  • Simba SC wamepambania mchezo kuchezwa Uwanja wa Mkapa jitihada zimegonga mwamba CAF.
  • RS Berkane kwao kicheko kwa kuwa wanatambua Uwanja wa Mkapa una rekodi nzuri kwa Simba SC.
  • CAF wamebainisha sababu za mchezo huo kuchezwa Zanzibar ikiwa ni fainali ya pili Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo wa pili hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika Simba SC vs RS Berkane ni rasmi utachezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar badala ya Uwanja wa Mkapa kama ambavyo awali ilitarajiwa kuwa hivyo kutokana na sababu ambazo zilitolewa na CAF.

------------------------------------------------n (-)
Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC itakayomenyana na RS Berkane Mei 25 2025. Source: CAF.

CAF walielekeza fainali ya pili kuchezwa Zanzibar baada ya wataalamu wao kufanya ukaguzi katika Uwanja wa Mkapa uliopo Dar na kubainisha kuwa kuna tatizo lipo eneo la kuchezea hasa mvua inaponyesha hivyo wakaelekeza mechi isichezwe hapo.

Simba SC tayari walikuwa wameanza kuuza tiketi kwa ajili ya mashabiki kujitokeza kushuhudia mchezo huo wakiwa na kampeni ya hii tunabeba ambapo kuna baadhi ya tiketi zilikuwa zimeisha. Licha ya maboresho ya Uwanja wa Mkapa bado ngoma itakwenda Zanzibar.

Taarifa ya Simba SC imeeleza namna hii:-

“Uongozi wa Klabu ya Simba SC unapenda kuwaafahamisha licha ya jitihada zote zilizofanywa na Serikali, TFF na Klabu ya Simba SC katika kuhakikisha mchezo wetu wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya RS Berkane Mei 25 2025 unafanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa zimeshindikana.

Taarifa
Taarifa kutoka Simba SC kuhusu uwanja. Source: Simba SC.

“Kutokana na hatua hiyo mchezo huo utafanyika katika Uwanja wa Amaan Zanzibar kama ilivyoamuriwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika, (CAF). Tunawaomba mashabiki na wapenzi wetu kuwa watulivu katika kipindi hiki.

“Aidha tutatoa taarifa rasmi za mchezo huu na hatma ya mashabiki wetu kuelekea katika mchezo huu muhimu kupitia mkutano maalumu na waandishi wa habari, Mei 20 2025.” Hii ni Taarifa ya Simba SC imetolewa Mei 19 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Zubeda Sakuru.

Inahusiana na hii :Simba SC vs RS Berkane Uwanja wa Mkapa waleta sekeseke CAF

Simba SC inahitaji mabao 3-0 kutwaa taji

Kuelekea kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya pili ambayo inakwenda kukamilisha dakika 180 kwa wababe hawa wawili, deni la Simba SC ya Tanzania ili kutwaa taji hilo ni lazima ipambane kupata ushindi wa mabao 3-0.

Mpanzu vs RS Berkane
Mpanzu nyota wa kikosi cha Simba SC kwenye mchezo dhidi ya RS Berkane. Source: Simba SC.

Sababu kubwa ya kupata mabao hayo ni kupoteza kwenye mchezo wa fainali ya kwanza iliyochezwa nchini Morocco. Mei 25 wachezaji wa Simba SC watakuwa na kibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa kuwa hata RS Berkane nao wanahitaji ushindi.

Matokeo mchezo uliopita ugenini, kicheko RS Berkane

Kwenye mchezo uliopita wakati Simba wakiwa ugenini, faida ilikuwa kwa RS Berkane waliopata ushindi baada ya dakika 90. Mei 17 2025 kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya kwanza uliochezwa nchini Morocco baada ya dakika 90 ubao ulisoma RS Berkane 2-0 Simba SC, mchezo wa pili utaamua nani atatwaa taji hilo

Ni RS Berkane wametanguliza mguu mmoja kwenye hesabu za kutwaa taji hilo kutokana na ushindi ambao waliupata wakiwa nyumbani kwa mabao mawili .waliyofunga kupitia kwa Mamadou Camara dakika ya 8 na Ousama Lamlioui dakika ya 15.

Kazi wakiwa nyumbani RS Berkane waliimaliza ndani ya dakika 15 za mwanzo huku Simba SC ikikwama kupata bao la ugenini ambalo lingewapunguzia mzigo wa idadi ya mabao wanayohitaji ili kupata ushindi. Mchezo kupelekwa Uwanja wa Amaan ni kicheko kwa RS Berkane kutokana na kuwa na rekodi mbaya Uwanja wa Mkapa walipokutana na Simba SC walipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Inahusiana na hii :RS Berkane 2-0 Simba SC: Magoli, takwimu, yaliyotokea ‘haijaisha mpaka iishe’

Rekodi zao dakika 90 ugenini

Katika dakika 90 za mwanzo wababe hawa walipokutana rekodi zinaonyeshwa kuwa RS Berkane walimiliki mpira kwa asilimia 51.7 huku Simba SC ikimiliki mpira kwa asilimia 48.8. Kwa mashuti kuelekea langoni ni 14 RS Berkane walipiga katika hayo 6 yalilenga lango na mawili yakiwa ni mabao huku Simba SC ikipiga mashuti 9 katika mashuti hayo hakuna shuti ambalo lililenga lango.

Ateba vs RS Berkane
Ateba vs RS Berkane. Source: Simba SC.

Pasi za usahihi kwa RS Berkane ilikuwa ni 286 na Simba SC ilikuwa ni pasi 278. Kona RS Berkane walipiga kona 7 na Simba SC ilikuwa ni kona mbili. Sehemu ambayo rekodi zao zilikwenda sawa ilikuwa eneo la faulo ambapo kila timu ilicheza faulo 14.

Neno la Kocha Mkuu wa Simba SC

Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba SC amesema kuwa walifanya makosa kwenye mchezo uliopita jambo lililofanya wakapoteza mchezo wao na wanafanya maandalizi kuelekea kwenye mchezo wa fainali ya pili.

“Tulikuwa tayari kwa mchezo na tulikuwa tunahitaji matokeo bahati haikuwa kwetu tumepoteza mchezo na hii ilitokana na presha ya wachezaji kutokana na kuwa wachanga kwenye fainali lakini walifanya kazi kubwa ninawapongeza.

“Kuelekea kwenye mchezo wetu wa fainali ya pili tunaamini tutakuwa tayari kukabiliana na wapinzani wetu kwa kuwa huu ni mchezo wa mpira na kila timu inahitaji ushindi.”

Ikiwa Simba SC itapindua meza na kupata matokeo ya mabao 3-0 mbele ya RS Berkane itakuwa ni timu ya kwanza kwa ukanda wa Afrika Mashariki kutwaa taji kubwa la Afrika.

Ikumbukwe kwamba Yanga SC ambao ni watani zao wa jadi waligotea kwenye hatua ya fainali na kuwa washindi wa pili hivyo rekodi ya mshindi wa pili tayari ilishaandikwa na Yanga SC.

Share this: