- Yanga SC waambiwa kwamba kama wanamuhitaji Mpanzu wanapaswa kumsubiri kwa muda wa miaka 13 kuipata saini yake.
- Ellie Mpanzu mwenyewe hajafikia hata asilimia 100 ya ubora wake akiwa uwanjani katika kutimiza majukumu kitaifa na kimataifa.
- RS Berkane kunyolewa kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya kwanza Mei 17 2025 mpango mzito wachorwa.
UONGOZI wa Simba SC umeweka wazi kuwa ogopa matapeli, Ellie Mpanzu hauzwi kwa kuwa ni mchezaji wao halali akiwa na mkataba wa miaka miwili na sio mchezaji wa mkopo kwa muda wa miezi sita kama ambavyo inaelezwa na kubainisha kuwa timu ambayo inamuhitaji inabidi isubiri kwa muda wa miaka 13.

Taarifa zilikuwa zinaeleza kuwa Mpanzu ambaye ni ingizo jipya ndani ya kikosi cha Simba SC kwenye dirisha dogo ambapo aliibuka hapo akitokea Klabu ya AJ Vainqueur ambayo inacheza ligi ya Epfkin ( Ligi ya tatu Congo). Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC amesema kuwa kwa wanaomtaka mchezaji huyo lazima wawasiliane na Simba SC ambao ni wamiliki halali wa mchezaji huyo.
Mchezaji huyo aliwahi kucheza AS Vita pia ya Dr Congo ambayo ilimpa utambulisho na wengi wakitambua kwamba anatokea kwenye timu hiyo jambo ambalo limezua gumzo kutokana na tetesi kueleza kuwa watani zao wa jadi Yanga SC wapo kwenye mpango wa kuinasa saini ya kiungo huyo.
Hizi hapa rekodi za Mpanzu Bongo kwenye ligi
Ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Mpanzu ambaye ni ingizo jipya kwenye dirisha dogo kacheza jumla ya mechi 14 akitoa pasi tatu za mabao huku akifunga mabao matatu. Kahusika kwenye mabao sita kati ya mabao 62 ambayo yamefungwa na Simba SC iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo msimu wa 2024/25.

Akiwa na Simba SC timu hiyo imetinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mei 15 itakuwa na kazi kwenye fainali ya kwanza itakuwa dhidi ya RS Berkane mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Fainali ya pili inatarajiwa kuchezwa Tanzania itakuwa ni Mei 25 2025, awali ilitarajiwa itachezwa Uwanja wa Mkapa ila taarifa kutoka CAF zimeeleza kuwa mchezo huo utachezwa Zanzibar katika Uwanja wa New Amaan Complex.
Kuhusu suala hilo Simba SC imeweka wazi kuwa taarifa rasmi ya uwanja utakaotumika kwa mchezo wa fainali ya pili ambayo itaamua nani atakuwa bingwa itatolewa baada ya mchezo dhidi ya RS Berkane unaotarajiwa kuchezwa Mei 17.
Inahusiana na hii:Stellenbosch FC vs Simba SC dakika 90 za maamuzi CAF
Ahmed Ally kuhusu mkataba wa Mpanzu

“Kimsingi tumeona na tumeskia propaganda za watu wakisema kwamba Mpanzu yupo Simba SC kwa mkopo wa miezi sita. Simba SC tumeshavuka hatua ya kuchukua mchezaji kwa mkopo wa miezi sita.
“Tunafahamu baada ya Mpanzu kuonyesha kiwango kizuri uwanjani kuna vijana kutoka hapa wamekwenda Dr Congo kuuliza namna gani wataweza kumpata Mpanzu.Ila ninawaambia kwamba waepuke hilo waogope matapeli mchezaji wetu hauzwi.
Simba SC yatoa masharti ili Mpanzu kuondoka
“Mpanzu alisaini mkataba wa miaka miwili na ametumia miezi minne kwa sasa hivyo bado mwaka mmoja na miezi mingine mingi kwelikweli. Kama wanamuhitaji Mpanzu ana miaka 22 watapaswa kusubiri kwa muda wa miaka 13 mpaka atakapofikisha miaka 35.
“Ni vilevile ambavyo walimvumilia Jonas Mkude alipotimiza miaka mingi ndani ya Simba SC alipotimiza miaka mingi wao wakamchukua ilikuwa hivyo kwa Clatous Chama alipocheza kwa miaka mingi Simba SC wao wakamchukua.
“Waache kujitekenya kwa sasa sijui Mpanzu sijui nini, hapana wao kama wanamtaka Mpanzu wasihangaike kwenda Dr Congo mmiliki wa Mpanzu ni sisi Simba SC tutawauzia kama hiyo hela watakuwa nayo. Lakini wavumilie miaka 13 sio mingi kwa sababu Mpanzu ana mkataba wa miaka miwili, sisi ndio wenye Mpanzu wanapaswa kuwa makini wasubiri. Mpanzu sio mchezaji wa AS Vita wakienda huko watatapelewa.
“Huyo mchezaji sio mchezaji wa hiyo timu ambayo wanaijua hivyo wakienda kwenye hiyo timu watatapeliwa kwa kuwa sisi tunajua chimbo ambalo tulimpata sisi. Hivyo ikiwa watakwenda huko watatapelewa kwa kweli.
“Hakuna ambaye ataweza hiyo hela ya Mpanzu kwa sasa kwa mchezaji wetu gharama yake ni kubwa n ahata wakijichanga ile timu wakachangisha kila mmoja kwa mashabiki watashindwa kumpata kwa kuwa hela yake ni kubwa.
RS Berkane kunyonyolewa Mei 17 2025

Ahmed Ally ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo wao wa hatua ya fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika inayotarajiwa kuchezwa Mei 17 2025 nchini Morocco kutokana na maandalizi ambayo wamefanya na wanaamini watamnyonyoa mpinzani wao RS Berkane.
“Tunakwenda kumnyonyoa RS Berkane kwa kuwa tunatambua kwamba huu ni mchezo wa mpira. Tunajua kwamba timu ambayo tunakutana nayo ni ngumu na dunia inajua kwamba mpinzani wetu ni mgumu hivyo inapaswa kuwa hivyo ili tutakapotwaa ubingwa wa CAF watu wajue kuwa tulichukua ubingwa kwenye timu ngumu.”
Inahusiana na hii: Stellenbosch FC vs Simba SC dakika 90 za maamuzi CAF
Mpanzu bado kiwango chake hakijafika asilimia 100
Nyota huyo licha yakuonyesha ubora kwenye mechi ambazo anacheza aliweka wazi kuwa bado hajafikia asilimia 100 ambazo anaamini akifikia hizo atakuwa bora zaidi katika mechi za ushindani kitaifa na kimataifa.
“Ninaona bado sijafikia ule ubora ambao ninahitaji kwa asilimia 100 kwa kuwa nilikuwa nje kwa muda mrefu. Nina amini kwamba taratibu ninazidi kuwa imara kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu.”

