- Yanga SC mzunguko wa kwanza iliwacha Namungo FC sebuleni kwao mabao 2-0 ikiondoka na pointi tatu kwenye mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Majaliwa.
- Khalid Aucho kiungo wa kazi ndani ya kikosi cha Yanga arejesha kicheko baada ya kuanza mazoezi kamili kuwakabili Namungo FC.
- Namungo FC sio kinyonge, watamba kubadili mbinu kuwakabili wapinzani wao Yanga SC kupata pointi tatu muhimu.
Yanga SC vs Namungo FC mechi ya mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara inatarajiwa kuchezwa leo Mei 13 2025, Uwanja wa KMC Complex saa 10:15. Kuna wachezaji wa Yanga ambao walikosekana kwenye mechi zilizopita wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi.

Miongoni mwa wachezaji hao ni Khalid Aucho huyu alipata maumivu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union, Pacome alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC, Kennedy Musonda alipata maumivu kwenye Muungano Cup 2025.
Kurejea kwao kwenye uwanja wa mazoezi kunaongeza nguvu katika kikosi cha kwanza kinachotarajiwa kuwa kazini kuvuja jasho kusaka pointi tatu muhimu ambazo kila timu inazihitaji.

Huyu hapa kocha Miloud wa Yanga SC
Miloud Hamdi, Kocha Mkuu wa Yanga SC amesema kurejea kwa baadhi ya wachezaji ambao walikuwa hawapo katika kikosi hicho kunaongeza nguvu kwa timu kuelekea kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa mgumu kwa pande zote mbili.

Kocha Miloud amebainisha kuwa maandalizi yao yapo vizuri kwa ajili ya kukabiliana na wapinzani wao Namungo FC kwenye mchezo wao wa ligi wakiwa tayari kupata matokeo kutokana na utayari wa wachezaji.
“Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu dhidi ya Namungo FC, wachezaji wote wana morali ya kutosha kwa ajili ya mchezo wetu. Tunajua wazi kuwa Namungo wanautaka mchezo huu kuhakikisha wanapata alama muhimu kwao.
“Tuna muda mrefu bila mechi ya ushindani hivyo tutacheza kwa umakini mkubwa kila dakika ndani ya uwanja kuhakikisha tunapata kile ambacho tunahitaji kwenye mchezo wetu muhimu.
“Lengo letu kuu ni moja tu, kushinda kila mechi ambayo ipo mbele yetu. Tunahitaji kuwa mabingwa msimu huu na hilo lipo wazi. Nawaheshimu Namungo FC, nafahamu wana timu nzuri.
“Kwetu sisi ni mchezo muhimu wa kushinda, hatupaswi kabisa kudondosha alama tena ukizingatia tupo nyumbani. Alama tatu kwetu ni muhimu. Nina furaha baadhi ya wachezaji wangu muhimu wote wamerejea kwenye kikosi, hivyo nina kikosi madhubuti. Tupo tayari kwa ajili ya mchezo wetu.”
Benchi la ufundi Namungo FC
Benchi la ufundi la Klabu ya Namungo FC limebainisha kuwa maandalizi waliyofanya kwa muda mrefu yanawapa matumaini kupata matokeo mbele ya wapinzani wao Yanga SC.
Mei 12 2025, Namungo FC chini ya Kocha Mkuu, Juma Mgunda walifanya mazoezi ya mwisho kwa ajili ya mchezo wa leo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya dakika 90.
Kocha msaidizi wa Namungo FC, Ngawina Ngawina amesema kuwa wanawaheshimu wapinzani wao Yanga SC kutokana na kuwa na timu imara yenye wachezaji wazuri wamepanga namna bora kuwakabili.
“Mchezo wetu dhidi ya Yanga tunaamini utakuwa mchezo mzuri tunawaheshimu Yanga wana timu nzuri na wachezaji wazuri pia sisi Namungo tumekuwa na muda mzuri wa kujiandaa kwasababu kila mchezo una mbinu yake ya kucheza kulingana na mpinzani tunayeenda kukutana nae.
“Tumekuwa na muda mrefu wa maandalizi yuna imani tutafanya vizuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga SC, tutaingia kwa tahadhari ili kupata matokeo mazuri kwani mpinzani wetu sio wakumbeza.
“Kila mchezo una mbinu zake hivyo tutaingia kwa mbinu tofauti kwa ajili ya kuwakabili wapinzani wetu Yanga SC. Tunatambua ubora wao ulivyo kutokana na namna walivyo na wachezaji imara.”
Mzunguko wa kwanza matokeo yao

Mchezo wa leo Mei 13 2025 ni mchezo wa mzunguko wa pili katika kukamilisha dakika 180 kwenye kutafuta pointi sita ambazo tatu za mwanzo zilirejea kwa Yanga SC ilipokuwa ugenini.
Kete ya kwanza iliyochezwa Novemba 30 2025 Uwanja wa Majaliwa ulisoma Namungo 0-2 Yanga SC hivyo mchezo wa leo itakuwa ni kisasi kwa Namungo FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda kusaka pointi tatu huku Yanga SC wakilinda rekodi yao.
Inahusiana na hii:Yanga Novemba kufunga ugenini, dakika 270 ganzi
Msimamo wa ligi upo hivi
Kwenye msimamo wa ligi, Yanga SC ni vinara wakiwa na pointi 70 baada ya kucheza mechi 26, ushindi ni kwenye mechi 23, sare moja na kupoteza mechi mbili. Namungo FC nafasi ya 10 wakiwa na pointi 31 kibindoni. Yanga SC ni timu namba moja kuruhusu mabao machache kwenye ligi ambayo ni 10 baada ya mechi 26 inakutana na Namungo FC ambayo imeruhusu mabao 33.

