Davids FadluDavids Fadlu
  • Jean Ahoua dhidi ya Stellenbosch FC nusu fainali ya kwanza alipata maumivu ya misuli dakika ya 86 akatolewa kwa machela.
  • Che Malone kajumuishwa kwenye msafara kamili kwa mchezo ujao Aprili 27 2025.
  • Air Manula, Mzamiru Yassin hawapo kwenye mpango kazi anga la kimataifa ugenini, Afrika Kusini.

Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ni ndoto kubwa kwa Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids msimu wa 2024/25.

Fadlu Kocha Mkuu Simba
Fadlu Davids Kocha Mkuu Simba kwenye kibarua kingine kimataifa Aprili 27 2025 Afrika Kusini. Source: Simba.

Tiketi ya Simba SC kutoka Tanzania kwenye kutinga hatua ya fainali ipo Afrika Kusini katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza dhidi ya Stellenbosch FC mchezo unaotarajiwa kuchezwa Aprili 27 2025 mshindi wa jumla atacheza fainali ya CAF.

HUYU HAPA FADLU DAVIDS

Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi matokeo ambayo waliyapata kwenye mchezo uliopita hayawafanyi waamini wamemaliza kazi bali wataingia uwanjani kwa nguvu kutafuta ushindi.

“Tulikuwa na mchezo mzuri nyumbani tukitengeneza nafasi nyingi ambazo tulishindwa kuzitumia, kwa yaliyotokea ni sehemu ya mchezo na tunafanyia kazi kwani tunatambua kwamba ni ngumu kupata nafasi nyingi kwenye mechi za kimataifa.

“Kikubwa ni kuanza upya na kufikiria namna nzuri kupata matokeo ugenini, tupo tayari kwa ajili ya kupata matokeo mazuri tunajua wapinzani wetu nao wanahitaji matokeo katika mchezo wetu.”

WACHEZAJI WA SIMBA WALIOPO AFRIKA KUSINI

Kikosi cha Simba kikipokewa Afrika Kusini
Moussa Camara kipa wa Simba ni miongoni mwa wachezaji waliopo Afrika Kusini. Source: Simba.

Moussa Camara, Ally Salim na Hussen Abel kwa upande wa makipa, Karaboue Chamou, Abdurazack Hamza, Mohamed Hussen, Shomari Kapombe, Valentino Nouma, David Kameta, Che Malone kwa upande wa mabeki.

Viungo ni Fabrince Ngoma, Awesu Awesu, Yusuph Kagoma, Kibu Dennis, Deborah Mavambo, Ladack Chasambi,Ellie Mpanzu, Augustine Okejepha, Jean Ahoua, Joshua Mutale.

Washambuliaji Simba imesepa nao wawili amba oni Leonel Ateba na Steven Mukwala ambao hawa wote kwenye mchezo uliopita Uwanja wa Amaan baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 1-0 Stellenbosch.

Mukwala alikuwa ni miongoni mwa wachezaji walioanza kikosi cha kwanza na alimpisha Ateba ambaye aliingia kipindi cha pili ilikuwa ni dakika ya 84 Ateba aliingia akikomba dakika sita kwenye mchezo huo.

WATAKAOKOSEKANA KWA SIMBA SC

Kuna mastaa ambao watakosekana kwa Simba kwenye mchezo huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni kipa Aishi Manula ambaye huyu bado hajawa fiti.

Che Malone
Che Malone beki wa Simba kuna hatihati akakosekana mchezo wa Aprili 27 2025 Afrika Kusini. Source: Simba.

Mbali na Manula, Valentino Mashaka ambaye ni mshambuliaji, Mzamiru Yassin kiungo wa kazi hajawa uwanjani kwa muda mrefu kutokana na kutokuwa fiti.

Licha ya beki Che Malone kuwa kwenye msafara kuna hatihati akaukosa mchezo kwa sababu hajawa na fiti baada ya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu.

AHOUA HALI YAKE IMEFIKIA HAPA

Kiungo Jean Ahoua yupo kwenye kikosi kilichotia timu Afrika Kusini ambapo kwa sasa anaendelea vizuri licha yakupata shida kwenye mchezo uliopita wa nusu fainali ya kwanza.

Jean Ahoua (-)
Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba ambaye alipata maumivu kwenye mchezo uliopita dakika ya 86. Source: Simba.

Ikumbukwe kwamba Aprili 20 2025 nyota huyo alipachika bao pekee la ushindi dhidi ya Stellenbosch FC dakika ya 44 na alipata maumivu dakika ya 86 alitolewa kwa machela lakini alirudi uwanjani kuendelea na majukumu yake na dakika ya 90 alikosa nafasi ya dhahabu kufunga bao akiwa ndani ya 18.

Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally ambaye aliweka wazi kuwa alipata maumivu ya misuli kwenye mchezo uliopita wakiwa nyumbani alipata matibabu kutoka kwa jopo la madaktari.

“Ahoua anaendelea vizuri kwa kuwa kwenye mchezo uliopita alipata maumivu ya misuli ila kwa sasa yupo imara na tayari kwa ajili ya mchezo wetu ujao, kikubwa ambacho tunahitaji kwenye mchezo wetu ujao ni kupata matokeo chanya.

“Lengo kubwa ni kuona kwamba tunatinga hatua ya fainali hilo linawezekana kwa kuwa tulianza kupata ushindi nyumbani na wachezaji wanatambua umuhimu wakucheza fainali, bado kazi inaendelea na tunaamini itakuwa hivyo, mashabiki wazidi kutuombea.”

KITUO KINACHOFUATA

Kete inayofuata kwa Simba ni ugenini Aprili 27 2025 dhidi ya Stellenbosch FC utakaopigwa  Uwanja wa Moses Mabhida. Ni dakika 90 za maamuzi ambazo zitatoa timu itakayotinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika.

Mshindi wa mchezo huu wa jumla anatarajiwa kucheza na mshindi wa mchezo kati ya RS Berkane ama Constantine ambapo kwenye hatua ya nusu fainali ya kwanza, RS Berkane Aprili 20 alipata ushindi wa mabao 4-0 hivyo ametanguliza mguu mmoja kwenye fainali.

Mchezo wa pili unatarajiwa kuchezwa Aprili 27 hivyo mshindi wa jumla atakata tiketi kutinga hatua ya fainali Kombe la Shirikisho Afrika ambalo limekuwa na ushindani mkubwa kwa kila timu uwanjani.

Share this: