Pacome zPacome z

YANGA yalipa kisasi mbele ya matajiri wa Dar, Azam FC kwa kukamilisha dakika 180 msimu wa 2024/25 kwa wababe hao wawili kugawana pointi tatutatu kila mmoja kwenye mechi za ligi ndani ya uwanja katika msako wa ushindi.

Ni Aprili 10 2025, Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilishuhudia ubao wa Azam Complex ukisoma Azam FC 1-2 Yanga ikilipa kisasi cha kupoteza pointi tatu za mzunguko wa kwanza ubao uliposoma Yanga 0-1 Azam FC.

Kibwana v Nado
Kibwana Shomari wa Yanga kwenye msako Dar Dabi dhidi ya Nado wa Azam FC, Aprili 10 2025. Source: Yanga.

DAKIKA 90 ZA JASHO NA KISASI

Ilikuwa ni dakika 90 za kisasi na jasho la kazi kuvuja kwa wachezaji wote ndani ya uwanja kusaka pointi tatu muhimu ndani ya mchezo wa ligi uliokuwa unasubiriwa kwa shauku kubwa, mwisho kisasi kwa Yanga kikalipwa.

Yanga walianza kasi kusaka lango la Azam FC wakiwa ugenini walisubiri mpaka dakika ya 11 kupata bao la kuongoza kupitia kwa Pacome Zouzoua ambaye alikuwa kwenye ubora wake katika dakika alizocheza kabla ya kupata maumivu na kutolewa nje.

Pacome v JKT Tanzania
Pacome nyota wa Yanga akiwa na wachezaji wenzake kwenye mchezo wa ushindani.Source: Yanga.

Bao la pili kwa Yanga ni mali ya Prince Dube alipachika bao hilo dakika 33 likiwa ni bao lake la 12 ndani ya ligi akiwa na uzi wa Yanga mara baada yakusepa katika kikosi cha Azam FC ambao walikuwa ni waajiri wake wa zamani.

Dube Prince (-)
Dube Prince mshambuliaji wa Yanga kwenye mchezo wa Dar Dabi, Uwanja wa Azam Complex. Source: Yanga.

Dakika 45 za mwanzo ilikuwa ni mali ya Yanga ambao walitawala mchezo kwa asilimia kubwa na kumtungua kipa Zuber Foba ambaye alianza kwa matajiri wa Dar, Azam FC kikosi cha kwanza huku Djigui Diarra safu ya ushambuliaji ya Azam FC ikikwama kumtungua dakika 45 za mwanzo.

Kipindi cha pili, Azam FC walidhamiria kuweka usawa kwenye mchezo huo kwa kuongeza mashambulizi kuelekea kwa Diarra matarajio yao yaliamka dakika ya 81 kwa bao la Lusajo Mwaikenda ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo na ubao ukasoma Azam FC 1-2 Yanga.

SEMAJI ALI KAMWE KICHEKO

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa kwao ni furaha kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo mgumu ambao ulikuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja.

“Ulikuwa ni mchezo mgumu kwa kuwa kila timu ilikuwa inasaka pointi tatu muhimu, hili ni kubwa kwetu na tumefanya kazi kubwa kupata pointi tatu muhimu, hii kwetu ni kubwa.”

HASHIM IBWE WA AZAM

Hashim Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kuwa walifanya kazi kubwa wachezaji kutafuta ushindi mwisho wamepoteza ni sehemu ya mchezo.

“Tulicheza vizuri ambacho kilikosekana ni matokeo kwa upande wetu, pongezi kwa wachezaji walijituma na mwisho tukapata hiki kilichotokea, hesabu zetu ni kwenye mechi zijazo ndani ya ligi.”

MWAMUZI ARAJIGA NA REKODI YAKE

Mwamuzi wa kati Ahmed Arajiga ameandika rekodi yakuchezesha mechi kubwa mbili za Dabi ndani ya msimu wa 2024/25 kwenye Ligi namba nne kwa ubora Afrika ambazo ziliwakutanisha Yanga na Azam FC kwenye msako wa pointi tatu uwanjani.

Mchezo wa kwanza ilikuwa ni Dar Dabi, Novemba 2 2024, Yanga 0-1 Azam FC uliochezwa Uwanja wa Azam Complex. Kwenye mchezo huu ushindi ulikuwa ni mali ya Azam FC ambao walibaki na pointi zao tatu wakiwa ugenini.

Dabi ya pili ilikuwa Dar Dabi, Aprili 10 2025 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Azam FC 1-2 Yanga. Ni dakika 180 za mgawanyo wa pointi tatutatu, ugenini Yanga alipoteza na akasepa na pointi tatu ugenini. Arajiga alionyesha kadi nyekundu kwa mchezaji mmoja ambaye ni Ibrahim Bacca wa Yanga mzunguko wa kwanza.

COASTAL UNION YAITULIZA SINGIDA BLACK STARS

Wakiwa Uwanja wa Mkwakwani baada yakufanyiwa maboresho, Coastal Union waliituliza Singida Black Stars kwa kukomba pointi tatu mazima wakiwa nyumbani pale Tanga. Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Coastal Union 2-1 Singida Black Stars.

Lucas Kikoti dakika ya 47 alifunga bao lakuongoza likawekwa usawa na Jonathan Sowa kwa mkwaju wa penati dakika ya 76 huku bao la ushindi likifungwa na Bakari Msimu dakika ya 82 zikiwa zimebaki dakika 8 mpira kugota mwisho.

JKT TANZANIA 2-2 NAMUNGO

Uwanja wa Isahmuhyo baada ya dakika 90 ubao ulisoma JKT Tanzania 2-2 Namungo, mabao yakifungwa na Maka Edward dakika ya 63 na Shiza Kichuya dakika ya 69 kwa JKT Tanzania. Ndani ya dakika 6, JKT Tanzania walifunga mabao mawili wakipindua meza dhidi ya Namungo ambayo ilianza kupata mabao yakuongoza.

Kwa Namungo inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda mabao yalianza kufungwa na Saleh Karabaka dakika ya 18 na Fabrince Ngoy dakika ya 49. Nyota Kichuya alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo.

MASHUJAA V TABORA UNITED

Mashujaa
Wachezaji wa Klabu ya Mashujaa wakishangilia moja ya bao kwenye mechi ya ushindani. Source: Mashujaa.

Uwanja wa Lake Tanganyika nyuki walipoteza makali yao kwa kushuhudia ubao ukisoma Mashujaa 3-0 Tabora United. Mundhir Abdullah alifungua akaunti ya mabao dakika ya 8, Jafari Salum alipachika bao la pili dakika ya 45 na kamba ya tatu ilikuwa ni mali ya David Richard dakika ya 87.

Share this: