HAZINA ile inayotunzwa ina faida kubwa wakati ujao kutokana na thamani yake kuongezeka maradufu hasa ukizingatia kwamba uhitaji haujawahi kugota mwisho, hivyo tu basi. Huku Yanga wakiwa na mwamba ambaye alibadili upepo na rekodi zake sio mchezo.
Wanasema dhahabu ili thamani yake iongezeke hupitishwa kwenye moto na hapo ndipo madini hayo yenye thamani kubwa yanaongezeka ule m’ngao wake licha ya moto kuwa mkali kinomanoma.

Katika ardhi ya Bongo katika eneo la wadaka mipira langoni, jina lake linatajwa kubadili upepo ghafla kwenye eneo hilo ambapo makipa wengi wamekuwa wakifuata nyayo zake na hata timu nazo zimeingia sokoni kutafuta makipa wenye aina hiyo.
Hii inatokana na namna ambavyo anatimiza majukumu yake akiwa ndani ya uwanja kwa kufanya wachezaji wote 11 kuwa kwenye mchezo, anatoka langoni anatuliza mipira na kutoa pasi kuelekea kwa wapinzani akiwa hana presha.
Ipo hivyo kwa nyota huyo aliye ndani ya kikosi cha Yanga inayodhaminiwa na SportPesa na mwendelezo wake haujawa na bahati mbaya kwa kuwa kwenye mikono yake uzoefu umetulia na katika ubongo wake anafikiria ushindi kwa ajili ya timu anayochezea akiwa anatimiza majukumu.
REKODI ZA 2021/22
Rekodi zinaonyesha kuwa msimu wa 2021/22 alitwaa tuzo ya kipa bora Bongo akimpoteza Aishi Manula kipa namba moja wa Simba kwa msimu huo uliokuwa na ushindani mkubwa. Diarra ni mechi 22 alikaa langoni akikusanya jumla ya hati safi 15 na alikomba dakika 1,944 huku akifungwa jumla ya mabao 7 akiwa langoni kwenye mechi za ushindani.

Kipa huyo alikuwa na wastani wa kufungwa bao moja kila baada ya dakika 277 akiwa langoni kwenye mechi ambazo alicheza kwa msimu huo na aliendelea kuwa kipa namba moja msimu wa 2022/23.
MSIMU HUU ALITUNGULIWA MABAO MENGI
Msimu wa 2022/23 Djigui Diarra ni mechi 25 alikaa langoni akisepa na dakika 2,217 ni hati safi 17 alikusanya na alifungwa jumla ya mabao 12 akiwa langoni, tofauti ya mabao matano ambayo yaliongezeka kwenye idadi ya mabao aliyofungwa na hati safi ziliongezeka mbili kibindoni.
Msimu huu alitunguliwa mabao mengi tofauti na msimu uliopita ambao alifungwa mabao 7 pekee. Ni wastani wa kila baada ya dakika 184 alikuwa akifungwa bao moja langoni.
Kwa mara nyingine tena alisepa na tuzo ya kipa bora ndani ya Yanga ambayo ilitwaa ubingwa wa ligi akiwapoteza makipa wengine aliokuwa akiwania nao tuzo ikiwa ni Aishi Manula wa Simba na Benedict Haule wa Singida Big Stars kwa wakati ule kwa sasa inaitwa Singida Black Stars.
2023/24 kazi ilikuwa nzito kwenye eneo la mlinda mlango baada ya kupata mshindani kutoka Coastal Union Ley Matampi ambaye huyu aliibuka kuwa kipa bora wa msimu huku Diarra akiwa kipa namba mbili kwa ubora alipokaa langoni kwenye mechi 23 alifungwa mabao 10.
Hati safi ilikuwa kwenye mechi 14 na alikomba dakika 1,935 uwanjani. Alikuwa na wastani wakuruhusu bao moja kila baada ya dakika 193 akiwa na uzi wa Yanga kipa huyo raia wa Mali.
Msimu wa 2024/25 yupo ndani ya kikosi cha Yanga akiwa ni kipa namba moja baada ya kucheza mechi 16 akikomba dakika 1,440 kakusanya hati safi 11 akikwa ametunguliwa mabao 7 kibindoni.
Kwa mujibu wa CAF Diarra ameletwa duniani Februari 27 1995 ni miaka 30 anayo kwa sasa ambapo baada ya miaka 10 kwa Neema ya Mungu raia huyu wa Mali atatimiza miaka 40.
NAFASI YA YANGA
Yanga kwenye msimamo msimu wa 2024/25 ipo nafasi ya kwanza ikiwa imekusanya jumla ya pointi 58 kibindoni ni timu namba moja kwa kufunga mabao mengi ambayo ni 58 ndani ya ligi namba nne kwa ubora Afrika.

Timu hiyo inayodhaminiwa na SportPesa inapambana kutetea taji la ligi ambalo ilitwaa msimu wa 2023/24. Kwa mastaa wenye mabao mengi namba eneo la ushambuliaji ni Prince Dube na Clement Mzize hawa wametupia mabao 10 kila mmoja.
Dube mbali ya kuwa nyota wa kwanza ambaye aliandika rekodi ya kufunga hat trick ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mashujaa kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex nim kali kwenye kutengeneza pasi za mwisho za mabao akiwa nazo 7.

