UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa mpango mkubwa ni kupata matokeo mazuri kwenye Kariakoo Dabi hivyo kitaumana baada ya kumalizana na Coastal Union dakika 90 kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Machi Mosi 2025 wakipata ushindi wa mabao 3-0 na watani zao wa jadi Yanga Februari 28 2025 ubao wa Uwanja wa CCM Kirumba ulisoma Pamba Jiji 0-3 Yanga.
Ikumbukwe kwamba mchezo wa mzunguko wa kwanza wababe hawa walipokutana katika Kariakoo Dabi, baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga, bao likifungwa na Kelvin Kijili wa Simba ambaye alijifunga.

Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ilisepa na pointi tatu mazima kwenye mchezo huo, inaongoza ligi ikiwa na pointi 58 baada ya kucheza mechi 22 ndani ya msimu wa 2024/25 ambao umekuwa na ushindani mkubwa.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa kwenye mechi ambazo zinafuata kwenye ligi kikubwa ambacho kinahitajika ni pointi tatu muhimu kwa kuwa kila mchezo ni muhimu kupata ushindi.
“Tulipata maumivu kwenye mchezo wetu wa ligi dhidi ya Azam FC katika dakika za mwisho tuliruhusu bao, hii inamaanisha kwamba ligi ina ushindani mkubwa na ulikuwa ni mchezo wa timu zenye ubora zilikutana uwanjani na mwisho tukagawana pointi mojamoja.

“Sasa kwa mechi ambazo zinafuata kikubwa ni kuona tunashinda, mchezo wetu dhidi ya Coastal Union ni muhimu halafu unakuja mchezo dhidi ya timu ambayo tunashindania ubingwa huu ni mchezo muhimu kwetu na ambacho tunahitaji ni pointi tatu muhimu.”
WABABE YANGA NA SIMBA
Yanga na Simba kwenye msimu wa 2024/25 vita yao imekuwa kubwa katika eneo la kusaka ushindi huku Yanga ikiwa na rekodi bora katika eneo la ushambuliaji ni timu namba moja kwa kufunga mabao mengi ambayo ni 58.
Mbali na kufunga mabao 58 baada ya mechi 22 Yanga imekusanya pointi 58 ikiwa nafasi ya kwanza kwenye ligi inaongoza kwa timu ambazo ziliambulia sare chache mpaka sasa ikiwa nayo moja pekee iliipata kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania.

Katika eneo la ulinzi Yanga imeruhusu mabao 9 yakufungwa uwanjani, dakika 180 ambazo ni mechi mbili iliambulia kichapo ilikuwa dhidi ya Azam FC na Tabora United.
Simba ni namba moja kwa timu iliyoruhusu mabao machache ambayo ni 8 baada ya mechi 21 na kwa upande wa safu ya ushambuliaji ni namba mbili ikiwa imetupia mabao 46 kinara wakucheka na nyavu ndani ya kikosi cha Simba ni Jean Ahoua mwenye mabao 10 na pasi sita za mabao.
Mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Uwanja wa Mkapa Simba iliyeyusha pointi tatu ikiwa nyumbani hivyo ilipoteza mchezo kwenye Kariakoo Dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa walipokutana mzunguko wa kwanza katika Kariakoo Dabi.
STEVEN MUKWALA AMEWAKA
Steven Mukwala mshambuliaji wa Simba amesema kuwa kazi kubwa ni kupambana kwenye mechi zote kupata matokeo mazuri kutokana na ushirikiano ambao upo kwenye timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.
Kwenye msimamo wa ligi Simba ni namba mbili baada ya mechi 21 imekusanya jumla ya pointi 54 vinara wakiwa ni Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi.
Simba mchezo wao uliopita wa ligi baada ya dakika 90 ubao ulisoma Coastal Union 0-3 Simba mtupiaji wa mabao yote akiwa ni Mukwala akisepa na tuzo ya mchezaji bora na mpira wake baada ya kufunga hhat trick.

Ni mabao 8 anafikisha Mukwala ndani ya ligi akiwa namba mbili wa wakali wakucheka na nyavu ndani ya kikosi cha Simba ni Jean Ahoua mwenye mabao 10 huyu ni namba moja, Mukwala na Leonal Ateba wote wametupia mabao 8.
Mukwala amesema kuwa kikubwa ambacho wanapambana ni kupata matokeo mazuri na wanaamini kazi itakuwa kubwa kwenye mechi zinazofuata.
“Shukrani kwa mashabiki ambao wapo nasi bega kwa bega kutokana uwepo wao kwenye mechi zetu zote, ambacho tunapambana ni kupata matokeo mazuri tunaamini itakuwa hivyo kwenye mechi zetu zote.”
Kituo kinachofuata kwa Simba ni Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Machi 8 2025.

