YANGA hawacheki na wowote huko ni spidi ndefu kila kona kutokana na rekodi ambazo zinaandikwa na wachezaji wao uwanjani katika eneo la kufunga na kutoa pasi za mabao, iwe wameanza kikosi cha kwanza ama wameanzia benchi ni mwendo wa kazi na kituo kinachofuata ni dhidi ya Pamba mchezo unaotarajiwa kuchezwa .
Mchezo dhidi ya Mashujaa uliochezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Februari 23 2025 baada ya dakika 90 ubao ukasoma Mashujaa 0-5 Yanga, Clatous Chama akianzia benchi alifunga mabao mawili baada ya kuingia akichukua nafasi ya Aziz Ki na kufikisha jumla ya mabao matatu kwenye ligi akiwa na pasi mbili za mabao.

Mchezo uliofuata kwa Mashujaa ilikuwa dhidi ya Singida Black Stars ambao ulichezwa Februari 26 2025 Uwanja wa Liti baada ya dakika 90 ubao ukasoma Singida Black Stars 3-0 Mashujaa. Kutokana na mwendo wa kupoteza mechi za ushindani taarifa ilitolewa na Mashujaa kuwa wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha Mohamed Abdallah, Bares.
Mashujaa kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 22 ipo nafasi ya 11 imekusanya pointi 23 huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 17 na ukuta ukiruhusu mabao 26 ndani ya dakika 1,980 haijawa kwenye mwendo bora ndani ya ligi kwenye mechi za ushindani msimu wa 2024/25 ambao una ushindani mkubwa.
PRINCE DUBE MUUAJI ANAYETABASAMU
Kiungo Chama yeye amehusika kwenye mabao matano kati ya 55 mshambuliaji Prince Dube, muuaji anayetabasamu ndani ya kikosi cha Yanga kinachodhaminiwa na SportPesa huyu ana balaa zito ndani ya uwanja akiwa kahusika katika mabao 17 akiwa ni namba moja kwa mastaa waliohusika katika mabao mengi zaidi kwenye ligi.

Nyota alifungua akaunti yake ya mabao kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ilikuwa ni Desemba 19 2024 alipofunga hat trick akiwa ni mchezaji wa kwanza kufanya hivyo ndani ya ligi msimu wa 2024/25 na mchezaji wa pili kufunga hat trick ni Aziz Ki wa Yanga ilikuwa dhidi ya KMC, Uwanja wa KMC Complex.
Aziz Ki alifunga mabao hayo ilikuwa ni Februri 14 wakati Yanga wakikomba pointi tatu mazima wakiwa ugenini katika mchezo wa mzunguko wa pili na wamekomba pointi sita mazima mbele ya KMC kwa kuwa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Azam Complex ilikuwa Yanga 1-0 KMC.
Dube ni mabao 10 kafunga akitoa pasi 7 za mabao kwenye mechi za ushindani. Yanga ni namba moja kwa timu zenye mabao mengi ambayo ni 55 ikifuatiwa na watani zao wa jadi Simba ambao ni mabao 41 safu ya ushambuliaji imefunga.
PACOME YUPO
Mbali na Dube kuhusika kwenye mabao 17 kiungo Pacome yeye kahusika kwenye mabao 13 akifunga mabao 7 na kutoa jumla ya pasi sita za mabao kwenye mechi za ligi. Mchezo dhidi ya Mashujaa alitoa pasi mbili za mabao na alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo baada ya dakika 90.
Pacome amekuwa imara kwenye eneo la upigaji penati ambapo kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar alipiga pigo moja ambalo lilijaa nyavuni na kumshinda mlinda mlango Ramadhan Chalamanda ambaye aliokoa penati ya Aziz Ki kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex.
CLEMENT MZIZE
Mzawa namba moja mwenye mabao mengi ndani ya ligi msimu wa 2024/25 ni Clement Mzize ambaye bao lake la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Kaitaba walipokomba pointi tatu mazima kwa ushindi wa mabao 2-0.
Kahusika kwenye mabao 13 akifunga mabao 10 na kutoa pasi tatu za mabao kwenye mechi za ligi na kwenye mabao hayo Mzize hajapewa jukumu la penati hivyo hana bao la penati mzawa huyo mwenye kasi akiwa ndani ya uwanja.
AZIZ KI
Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Aziz Ki amehusika kwenye mabao 12 kati ya 55 akifunga mabao sit ana kutoa pasi sita. Huyu ni mtaalamu wa mapigo huru akiwa amepiga penati sit ana katika hizo ni nne alifunga huku akikosa mbili.
MBABE KWA SIMBA NA AZAM

Kwa upande wa Simba ni Jean Ahoua kahusika katika mabao 16 akifunga mabao 10 na pasi 6 za mabao. Kwenye mabao hayo matano kafunga kwa mapigo ya penati huku upande wa Azam FC akiwa ni Feisal Salum mwenye pasi 11 na katupia mabao manne akihusika kwenye mabao 15 kati ya 31 yaliyofungwa na timu hiyo huku Simba ikiwa imetupia mabao 43 baada ya kucheza mechi 20.

