BAADA ya kutoshana nguvu kwa kufungana bao 1-1 dhidi ya Fountain Gate benchi la ufundi la Simba limeweka wazi kuwa hesabu kubwa ni kuelekea katika mchezo ujao dhidi ya Tanzania Prisons ukiwa ni mtihani mzito kwa Simba kusaka pointi tatu ambazo zinahitajika pia na Prisons.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Complex Februari 11 2025 kwa wababe hao kushuka uwanjani kusaka pointi tatu muhimu ndani ya dakika 90. Prisons baada ya kucheza mechi 17 haijawa na mwendo mzuri kwenye ushindi ikipata ushindi katika mechi nne, sare 5 na kupoteza jumla ya mechi 8.
Ipo wazi kwamba kwenye mchezo uliopita ikiwa ugenini Simba ilishuhudia ubao ukisoma Fountain Gate 1-1 Simba, bao la Simba lilifugwa na Leonel Ateba dakika ya 57 akiwa ndani ya 18 kwa pasi ya Ladack Chasambi.

Haikuwa siku nzuri kwa Simba Februari 6 2025 dakika ya 75 Chasambi alijifunga kwenye harakati za kurudisha mpira nyuma kwa kipa Mousa Camara ambaye alikwama kuokoa mpira huo uliozamama mazima nyavuni.
Licha ya kipa wa Fountain Gate, Noble John kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90 kutokana na kadi mbili za njano bado Simba iligotea kuvuna pointi moja kwenye mchezo huo.
HUYU HAPA FADLU
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa wanatambua mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons utakuwa mgumu ukizingatia kwamba ni mzunguko wa pili kila timu inapambana kupata matokeo mazuri.
“Ni mchezo muhimu kwetu kutafuta alama tatu lakini tunakutana na upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wetu ukizingatia kwamba wamebadili kocha na mechi za mzunguko wa pili huwa zinakuwa ngumu tumefanya maandalizi kwa ajili ya kupata pointi tatu muhimu.”
Kwa upande wa beki Shomari Kapombe amesema kuwa wanatambua upinzani ambao wataupata kutoka kwa Tanzania Prisons lakini wanachohitaji ni pointi tatu muhimu ndani ya uwanja.
“Mara nyingi ambapo tunakutana na wapinzani wetu mchezo huwa unakuwa mgumu tunatambua kwamba haitakuwa kazi rahisi tunakwenda kupambana kupata pointi tatu kwa ajili ya mchezo wetu ambao utakuwa na ushindani mkubwa.”
HAWA HAPA VINARA
Vinara wa ligi namba nne kwa ubora ndani ya Afrika kwa sasa ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ikiwa na pointi 45 imecheza mechi 17 kama ambavyo Simba imecheza ndani ya ligi.

Februari 10 Yanga itakuwa ugenini kwenye mchezo wa kuwania pointi tatu dhidi ya JKT Tanzania mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Isamuhyo saa 10:15 ambapo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ipo wazi kwamba Yanga ikiwa na pointi 45 kwenye mechi 17 ni mechi 15 ilipata ushindi huku ikipoteza mechi mbili pekee ilikuwa dhidi ya Azam FC na Tabora United, hakuna mchezo iliotoshana nguvu na mpinzani wake ndani ya dakika 90.
Kwa upande wa JKT Tanzania ni ushindi kwenye mechi nne pekee huku ikipoteza mechi 6 na kuambulia sare katika mechi 7 ni miongoni mwa timu ambazo hazijafungwa mabao mengi ikiwa imeruhusu mabao 14 inakutana na timu ya Yanga ambayo imeruhusu mabao 7 yakufungwa.
Yanga kwenye upande wa kufunga imekuwa imara ambapo ni namba moja ndani ya ligi ikiwa imefunga jumla ya mabao 42 kinara wa utupiaji ni Clement Mzize mwenye mabao 9 ndani ya ligi na katoa pasi nne za mabao huku JKT Tanzania ikiwa imefunga jumla ya mabao 11 hivyo katika safu ya ushambuliaji haijawa imara.
MECHI NYINGINE HIZI HAPA
KenGold ipo nafasi ya 16 kwenye msimamo na pointi 6 itamenyana na Fountain Gate iliyo nafasi ya 7 pointi 21, Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
KMC ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo ikiwa na pointi 19 itawakaribisha Singida Black Stars nafasi ya nne pointi 34, Uwanja wa KMC, Complex, Dar.
JKT Tanzania ipo nafasi ya 10 itakuwa kwenye msako wa pointi tatu dhidi ya Yanga vinara wa ligi wenye pointi 45, Uwanja wa Isamuhyo, saa 10:45.
AZAM FC WAPOTEZA MBELE YA PAMBA
Matajiri wa Dar, Azam FC wakiwa ugenini mbele ya Pamba Jiji kwenye mchezo wa ligi waliyeyusha pointi tatu mazima ugenini katika msako wa pointi tatu muhimu ndani ya dakika 90.

Katika mchezo huo uliochezwa Februari 9 2025 ngoma ilikuwa nzito kwa timu zote mpaka dakika ya 86 kwa bao la kiungo mshambuliaji Deus Kaseke ambaye alipachika bao hilo la ushindi lililodumu mpaka mwisho wa mchezo.
Azam FC inabaki na pointi 39 kwenye msimamo ni namba tatu huku Pamba Jiji ikifikisha pointi 18 nafasi ya 12 kwenye msimamo, ina wastani wa kukomba pointi moja kwenye kila mchezo kwa kuwa ni mechi 18 imecheza ndani ya msimu wa 2024/25.

