KIBU Dennis, mkandaji chaguo namba moja la Kocha Mkuu, Fadlu Davids huenda akakosekana kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa kwenye dakika 90 za jasho la kusaka pointi tatu kwa wanaume 22.

Kibu alipata maumivu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United uliochezwa Februari 2 2025 ilikuwa dakika ya 50 alikwama kusepa na dakika zote 90 katika mchezo huo na mwisho ubao ulisoma Tabora United 0-3 Simba.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2024/25 Kibu hajafunga bao ndani ya ligi wala kutoa pasi, mara ya mwisho kufunga ilikuwa ni Novemba 5 2024 ambapo alifunga bao mbele ya Yanga inayodhaminiwa na SportPesa dakika ya 9 kwenye mchezo huo ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 1-5 Yanga.
Ni mechi 12 Kibu amecheza msimu wa 2024/25 ndani ya ligi akiyeyusha dakika 845. Rasta huyo amekuwa na matumizi makubwa ya nguvu ndani ya uwanja kwenye kutimiza majukumu yake uwanjani.
Kwa mujibu wa daktari wa Simba, Edwin Kagabo amesema kuwa maendeleo ya mchezaji huyo kwa sasa ni mazuri kwa kuwa alipata matibabu.
“Wachezaji wote wapo vizuri na kuhusu Kibu Dennis ambaye alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Tabora United hali yake inazidi kutengamaa, kuhusu kuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Fountain Gate ni 50/50,”.
PACHA HII SIMBA INABALAA

Ndani ya kikosi cha Simba kuna pacha mpya ambayo imekuwa na balaa ndani ya uwanja kutokana na maelewano yao kwenye mechi wanazocheza kitaifa na kimataifa kwenye msako wa ushindi.
Simba ni namba moja kwenye msimamo ikiwa na pointi 43 mchezo wao ujao wa ligi ni dhidi ya Fountain Gate unaotarajiwa kuchezwa Februari 6 2025 tayari maandalizi ya mwisho yanaendelea kuwakabili wapinzani hao.
Ikumbukwe kwamba Simba katika anga la kimataifa baada ya kucheza mechi sita hatua ya makundi ni mabao 8 safu ya ushambuliaji ilifunga kinara wa utupiaji ni kiungo mshambuliaji Kibu Dennis ambaye katupia mabao matatu.

Kapombe na Ateba wamekuwa na maelewano kazini kutokana na kila mmoja kufanyia kazi pasi ya mchezaji kwenye mechi ngumu ambazo zinahitaji pointi jambo ambalo limeongeza nafasi ya Simba kugotea nafasi ya kwanza ikiwa na pointi 13katika Kombe la Shirikisho Afrika.
Ilianza ugenini dhidi ya Bravos Januari 12 2025 dakika ya 69 wakati Simba ikiwa nyuma kwa bao moja pasi ya dhahabu kutoka kwa Kapombe ilikutana na Ateba ambaye alifunga bao la kuweka usawa wakagawana pointi mojamoja.
Bao la pili ilikuwa Uwanja wa Mkapa dhidi ya Constantie Januari 19 2025 alianza Kibu kufunga bao la kuongoza kisha Ateba akafunga bao la pili akitumia pasi ya Kapombe ilikuwa dakika ya 79.
Nyota hawa wamekuwa na maelewano na dakika zao zenye hatari ni zile zenye 9 mwisho kwa kuwa dhidi ya Bravos ilikuwa dakika ya 69 na dhidi ya Constanine ilikuwa dakika ya 79.
Mwendelezo wa pacha hiyo ulijibu Tabora dhidi ya Tabora United ambapo Ateba kwenye mchezo huo alifunga mabao mawili na alitoa pasi moja ya bao kwa Kapombe ambaye aliandika bao la tatu la Simba.
Katika mchezo huo Februari 2 2025 Ateba alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kutokana na kuhusika kwenye mabao yote matatu alifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao na Simba ikakomba pointi tatu ugenini.
Pacha hiyo inatarajiwa kuwa na kazi kwa mara nyingine ugenini kwenye mchezo wa ligi namba nne kwa ubora. Ateba amefikisha mabao 7 ndani ya ligi na ametoa jumla ya pasi mbili za mabao.
HII HAPA RATIBA YA FEBRUARI 6 2025

Tanzania Prisons ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 14 itamenyana na Mashujaa iliyo nafasi ya 7 na pointi 19 inatarajiwa kuchezwa saa 8:00 mchana, Uwanja wa Sokoine.
Dodoma Jiji iliyo nafasi ya 9 na pointi 19 v Pamba Jiji iliyo nafasi ya 14 pointi 12 inatarajiwa kuchezwa saa 8:00 mchana, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Fountain Gate yenye pointi 20 nafasi ya sita dhidi ya Simba yenye pointi 43 nafasi ya kwanza, Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa, saa 10:15 jioni.
Azam FC yenye pointi 36 nafasi ya tatu itakuwa dhidi ya KMC yenye pointi 19 nafasi ya 10 saa 1:00 usiku, Uwanja wa Azam Complex.

