KUTOKA Ligi namba nne kwa ubora Afrika 2024/25 sio kitoto kwa kuwa kumekuwa na ushindani mkubwa kutoka timu zote kuanzia vinara Simba, wanaofuatia Yanga, Azam FC, Singida Black Stars mpaka Ken Gold nao wamo kwenye mapambano huku zikiandikwa rekodi zakutosha mzunguko wa kwanza.
Ipo wazi kwamba mabingwa watetezi wa ligi ni Yanga inayodhaminiwa na SportPesa imekuwa kwenye mwendo wake katika kusaka matokeo ndani ya uwanja.

Januari 23 2025 taarifa kutoka Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) ilieleza kuwa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS) limeitangaza ligi ya Tanzania (NBC Premier League) kuwa Ligi ya nne (4) kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024.
Ligi hiyo imepanda kwa nafasi mbili (2) kutoka nafasi ya sita (6) mwaka 2023 ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia. Hii ni habari njema na kubwa kwene soka la Bongo ambapo hapa tunakuletea baadhi ya rekodi zilizoandikwa kwenye mzunguko wa kwanza namna hii:-
WAKALI KWENYE HATI SAFI

Makipa naos io kinyonge wamekuwa wakifanya kazi kubwa kutimiza majukumu yao na ushindi mkubwa kwao ni kutoka na hati safi yaani kukamilisha dakika ambazo watakuwa langoni bila kufungwa.
Rekodi zinaonyesha kuwa ni Moussa Camara kipa wa Simba anaongoza chati akiwa kakaa langoni kwenye mechi 15 hajafungwa kwenye mechi 12 za Ligi Kuu Bara.
PATRICK MUNTHALI
Patrick Munthali kutoka Mashujaa ya mwisho wa reli Kigoma amekusanya hati safi 8 akiwa namba mbili kwa makipa ambao hawajafungwa kwenye mechi nyingi langoni.
DIARRA NA MNATA

Licha ya kutokuwa fiti kwenye baadhi ya mechi kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra anaingia kwenye orodha ya makipa ambao hawajafungwa kwenye mechi nyingi ambazo ni 7.
Kipa namba moja wa Singida Black Stars, Metacha Mnata naye pia ni mechi 7 amekamilisha akiwa langoni bila kutunguliwa.
MOHAMED MUSTAPHA
Kipa wa Azam FC Mohamed yeye hajafungwa kwenye mechi 6 ndani ya ligi alipokuwa ndani ya uwanja akitimiza majukumu yake.
WAKALI WA PASI ZA MWISHO
FEISAL SALUM

Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum yeye ni namba moja kwa wachezaji ndani ya ligi namba nne kwa ubora kutoa pasi nyingi za mabao ambazo ni tisa. Pasi yake ya kwanza msimu wa 2024/25 alitoa kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex alimpa Idd Nado ilikuwa dakika ya 19.
Katika mchezo huo kiungo Feisal alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo kwa kuwa alitoa pasi mbili za mabao na alicheza katika kiwango bora ndani ya dakika 90 wakiwa ugenini.
JEAN AHOUA

Kiungo mshambuliaji wa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni namba mbili kwa wakali wa kutengeneza pasi za mwisho akiwa nazo 5 ndani ya kikosi hicho ambacho kinaongoza ligi.
SALUM KIHIMBWA
Mkali ambaye amecheza Mtibwa Sugar, rasta ambaye ana uwezo mkubwa kwenye miguu yake ni mkali kwenye kutengeneza pasi za mwisho akiwa ndani ya Fountain Gate akiwa ametoa pasi tano za mabao.
AZIZ KI
Kiungo mwenye uwezo mkubwa kutumia mguu wa kushoto yupo zake ndani ya Yanga Aziz Ki katoa pasi nne za mabao akiwa amefunga mabao mawili pia ndani ya ligi.
JOSEPHAT ARTHUR
Nyota huyu yupo ndani ya Singida Black Stars ametoa jumla ya pasi nne za mabao saw ana Pacome Zouzoua wa Yanga na Clement Mzize.
TIMU ZILIZOPATA PENALTI
SIMBA 6

Ndani ya mzunguko wa kwanza timu ambayo imeongoza kwa kupata penalti katika mechi za Ligi Kuu Bara ni Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids baada ya kucheza mechi 15 ikiwa nafasi ya kwanza na pointi 40 kibindoni.
Kwenye mabao 31 Simba ni mabao sita imefunga kwa penalty ambapo mastaa wawili ni vinara kwa utupiaji kwa mapigo ya penati wakiwa na rekodi ya kufunga zote ni Leonal Ateba ambaye ni mshambuliaji huyu kafunga penalti 3 sawa na Jean Ahoua.
Ikumbukwe kwamba Ateba katupia jumla ya mabao matano na Ahoua ni mabao 7 kafunga huku yote akitumia mguu wa kulia kufunga ndani ya ligi msimu wa 2024/25.
MWENDO WA TANOTANO
Coastal Union ya Tanga imepata jumla ya penalti 5 ndani ya ligi ambapo timu hiyo msimu wa 2024/25 imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya 11 imekusanya pointi 18 baada ya mechi 16 safu yake ya ushambuliaji imefunga mabao 16.
Namungo FC ilipata penalti 5 pia huku nyota mwenye mabao mengi ya penalti akiwa ni kiraka Erasto Nyoni huyu katupia kambani penalti mbili kwa timu hiyo ambayo ipo nafasi ya 12 ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza mechi 16.
Tabora United ile nafasi ya tano kwenye msimamo ni penati 5 pia ilipata ambapo imekusanya jumla ya pointi 25 kwenye ligi ikiwa ipo ndani ya tano bora timu hiyo iliyokomba pointi tatu za Yanga ikiwa ugenini kwa ushindi wa mabao 3-2.
AZAM FC NA YANGA CHUNGU KIMOJA
Matajiri wa Dar, Azam FC ni penalti tatu walipata n azote walifunga kupitia kwa kiungo Feisal wa Azam FC ambaye jumla kafunga mabao manne na matatu ilikuwa kwa penati. Azam FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 36 baada ya mechi 16.
Yanga ni penati 3 imepata na azote mpigaji ni Aziz Ki alipata bahati ya kufunga mabao mawili kwa mapigo ya penati ndani ya Yanga na alikosa penalty moja ilikuwa dhidi ya Tabora United. Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 39 baada ya mechi 15.

