FUNGA kazi Desemba 2024 haikuwa rahisi kwa wababe kufanya kazi kubwa ndani ya uwanja kusaka pointi tatu ambapo wengine waliambulia ushindi na wengine ilikuwa ni maumivu baada ya kupoteza pointi tatu muhimu kwenye mchezo.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa sio kinyoge walifunga Desemba kwa kicheko baada ya kuvuna pointi tatu wakiwa nyumbani kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Fountain Gate.

Bao la kwanza la Yanga limefungwa na Pacome dakika ya 15 akafunga bao la pili dakika ya 45, Mudathir Yahya dakika ya 41, Jackson Shiga wa Fountain Gate alijifunga dakika ya 53. Clement Mzize ndani ya dakika 45 ametoa pasi mbili za mabao ya kwanza alimpa Mudathir na nyingine alipewa Pacome.
Yanga imetoka kupata ushindi ugenini dhidi ya Dodoma Jiji Uwanja wa Jamhuri, Dodoma baada ya dakika 90 ubao ulisoma Dodoma Jiji 0-4 Yanga na langoni alianza Mshery akishuhudia wakisepa na pointi tatu mazima.

KIKOSI CHA YANGA
Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomary, Ladack Boka, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki, Pacome
Wachezaji ambao walikuwa benchi ni :Aweso, Kibabage, Nondo, Nkane, Abuya, Sure Boy, Sheikhan, Mkude, Farid Mussa, Kennedy Musonda.
SIMBA WALIITULIZA SINGIDA BLACK STARS
Vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids waliwatuliza Singida Black Stars kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Liti.

Zilikuwa dakika 90 zenye ushindani mkubwa huku dakika 45 za mwanzo Singida Black Stars hawakuwa bora kwenye umiliki wa mpira kwa mujibu wa Kaimu Kocha Mkuu, Ramadhan Nswazurimo.
Baada ya mchezo Nswanzurimo alibainisha kuwa wachezaji walicheza kwa umakini mkubwa kipindi cha pili lakini kipindi cha kwanza walipoteza mipira mingi.
“Kipindi cha kwanza hatukuwa kwenye umiliki mzuri wa mpira na niliwaambia wachezaji kwamba ni muhimu kutulia kipindi cha pili ikawa hivyo ndio maana kulikuwa na utoafuti mkubwa kwenye kipindi cha pili katika mchezo wetu.”
Bao pekee la ushindi kwa Simba lilifungwa na Fabrince Ngoma dakika ya 42 akitumia pigo la kona iliyopigwa na Jean Ahoua lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo ambao Kibu alianza kikosi cha kwanza.

Ngoma alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo baada ya dakika 90 kugota mwisho ambapo Simba inafunga Desemba ikiwa namba moja kwenye msimamo wa ligi.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids aliweka wazi kuwa walipambana kutafuta matokeo kwenye mchezo huo jambo ambalo lilitokea hivyo wachezaji wanastahili pongezi kwa kazi kubwa waliyofanya.
“Wachezaji wanastahili pongezi kutokana na kazi kubwa ambayo wameifanya na unaona tumepata pointi tatu muhimu, ulikuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa na mwisho tumepata matokeo mazuri.”
HILI HAPA JESHI LA SIMBA DESEMBA 28
Kwa upande wa kipa ni Mousa Camara, mabeki ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussen, Che Malone, Hamza. Viungo ni Yusuph Kagoma, Fabrice Ngoma, Jean Ahoua, Ellie Mpanzu, Kibu Dennis, Steven Mukwala.
Kwenye benchi mastaa walikuwa ni: Ally, Kijili Kelvin, Chamou, Mzamiru Yassin, Ladack Chasambi, Mavambo, Ateba, Awesu Awesu, Mashaka, Alexander.
MATAJIRI WA DAR HAWAPOI

Desemba 27 matajiri wa Dar, Azam FC walipindua meza kibabe baada ya kutanguliwa kufungwa mapema na wapinzani wao JKT Tanzania kwa pigo la faulo iliyozama kimiani na mtupiaji alikuwa ni Said Ndemla ilikuwa dakika ya 13.
Baada ya bao hilo Azam FC walirejea kwenye mchezo na kufunga mabao matatu, walianza kupachika bao la kuweka usawa kupitia kwa Pascal Msindo dakika ya 36 na Idd Nado alitupia mawili dakika ya 63 na 71.
Nado alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo wakikomba pointi tatu mazima na pasi mbili zote za Nado zilitoka kwenye miguu ya kiungo Feisal Salum ambaye anafikisha jumla ya pasi tisa za mabao.
Feisal anakuwa ni namba moja kwa wakali wenye pasi nyingi za mwisho ndani ya ligi msimu wa 2024/25 na katupia mabao manne ndani ya kikosi cha Azam FC.
MASHUJAA FUNGA KAZI YAO KINYONGE
Mashujaa wakiwa Uwanja wa Jamhuri, katika funga Desemba walishuhudia Dodoma wakisepa na pointi tatu mazima ilikuwa Desemba 28 walipasuka kwa kupoteza pointi tatu katika mchezo huo kwa kushuhudia ubao ukisoma Dodoma Jiji 3-1 Mashujaa.
Mabao ya Dodoma Jiji yalifungwa na Mwana Kibuta dakika ya 12, Lulihosi Heritier dakika ya 16, Zidane Serari dakika ya 83 na lile la Mashujaa lilifungwa na Crispin Ngush dakika ya 90.

