MERRY Christmas 2024 kwa kila mmoja huku katika ulimwengu wa mpira kazi ikiwa inaendelea kwa timu kusaka ushindi ndani ya dakika 90 na wababe wanavuja jasho mwanzo mwisho katika msako wa ushindi.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa Desemba 25 ilikuwa kazini kusaka pointi tatu dhidi ya Dodoma Jiji na ilishuhudia watani zao wa jadi Simba wakiwa kazini siku ya Desemba 24 2024 dhidi ya JKT Tanzania.
Kwenye mchezo wa Desemba 25 2024 mbele ya Dodoma Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Jamhuri Dodoma baada ya dakika 90 kugota mwisho ni Dodoma Jiji 0-4 Yanga.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Clement Mzize ambaye katupia mawili dakika ya 18 na dakika ya 37 kwenye mchezo huo, moja limefungwa na Aziz Ki kwa mkwaju wa penalti dakika ya 28 likiwa ni bao lake la pili ndani ya ligi na Kamba ya nne mali ya Prince Dube dakika ya 62 akifikisha jumla ya mabao matano sawa na Leonel Ateba wa Simba.

JESHI LA YANGA DHIDI YA DODOMA JIJI

Aboutwalib Mshery, Kibwana Shomari, Nickson Kibabage, Dickson Job, Ibrahim Bacca, Khalid Aucho, Clement Mzize, Mudathir Yahya, Prince Dube, Aziz Ki, Pacome.
Wachezaji wa akiba ni Khomein, Kassim, Nondo, Boka, Jonas Mkude, Dennis Nkane, Sureboy, Duke Abuya, Farid Mussa, Shekhan.
RUPIA ANAYETAJWA YANGA BALAA NA NYAVU
Mshambuliaji mwili jumba mali ya Singida Black Stars ambaye anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga amekuwa kwenye ubora wake katika kucheka na nyavu ndani ya uwanja msimu wa 2024/25.
Mbele ya Ken Gold kwenye mchezo wa ligi alifunga bao moja akifikisha jumla ya mabao 8 ndani ya ligi ni namba moja kwa watupiaji ndani ya kikosi cha Singida Black Stars akiwa kwenye ubora wake.
Kwenye mchezo huo uliochezwa Desemba 24 2024 baada ya dakika 90 ubao ulisoma Singida Black Stars 2-1 Ken Gold. Mchezo huo ulichezwa saa 8:00 mchana, Uwanja wa Liti. Licha ya Ken Gold kuanza kucheka na nyavu bado waliziacha pointi tatu ugenini.
Bao la Ken Gold lilifungwa mapema na Herbent Lukiondo ilikuwa dakika ya 25 yale ya Singida Black Stars yalifungwa na Arthur Bada dakika ya 46 na Elvis Rupia ilikuwa dakika ya 55 likaipa pointi tatu muhimu Singida Black Stars.
MERRY CHRISTMAS
Ikiwa ni sikukuu ya Christmas duniani, kuna burudani ambazo zinaendelea ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo Fountain Gate na Namungo walikuwa kazini mapema kusaka pointi tatu saa 8:00 mchana na jioni ilikuwa zamu ya Dodoma Jiji dhidi ya Yanga.

Ikumbukwe kwamba Yanga mchezo wake uliopita walikuwa Uwanja wa KMC walipopata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tanzania Prisons ikiwa ni mwanzo kuelekea kwenye Christmas.
Zawadi ya Christmas mapema ilikuwa kwa Namungo ambao wao waliambulia furaha kwa kukomba pointi tatu muhimu huku Fountain Gate wakipoteza pointi tatu kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.
Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Fountain Gate 1-2 Namungo, Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa bao pekee la Fountain Gate lilifungwa na Salum Kihimbwa, dakika ya 30 yale ya Namungo yalifungwa na Pius Buswita, dakika ya 10, Geofrey Julius, dakika ya 78.
ZAWADI KWA WANASIMBA

Wakiwa Uwanja wa KMC Complex, Simba walitoa zawadi kwa mashabiki wao baada ya kupata ushindi wa jioni mbele ya JKT Tanzania lililofungwa na Jean Ahoua dakika ya 90+3 kwa pigo la penalty iliyosababishwa na Shomary Kapombe ambaye alionekana kuchezwa faulo ndani ya 18.
Nyota wa mchezo ni Yakoub Suleiman ambaye ni kipa wa JKT Tanzania alikuwa bora kwa kuokoa hatari za Simba kupitia kwa Leonel Ateba, Ellie Mpanzu, Awesu Awesu.
Simba inafikisha pointi 37 baada ya kucheza mechi 14 msimu wa 2024/25 nafasi ya kwanza na ushindi wao ni kwenye mechi 12, sare moja na ilipoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga.
HAWA HAPA WATAFUNGUA MABOX
Kazi bado inaendelea ambapo Desemba 26 2024 ikiwa ni Boxing Day kuna timu zitakuwa kazini kusaka ushindi ndani ya dakika 90 na itafahamika nani ambaye atafungua box la shangwe na nani atafungua boxi lenye ganzi ya maumivu.
Ni mchezo mmoja unatarajiwa kuchezwa ambapo itakuwa kati ya Tanzania Prisons iliyotoka kupoteza dhidi ya Yanga Uwanja wa KMC na itapambana na Pamba Jiji mchezo nis aa 10:00 jioni kwa wababe hawa kusaka pointi tatu muhimu.
Pamba Jiji baada ya kucheza mechi 15 imekusanya jumla ya pointi 12, ushindi ni kwenye mechi 2, sare 6 na imepoteza mechi 7 na safu ya ushambuliaji imefunga mabao 7. Inakutana na Tanzania Prisons ambayo imekusanya pointi 11 baada ya kucheza mechi 15.
Prisons ushindi wake ni kwenye mechi 2, sare 5, imepoteza mechi 8 na safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao sita kwa msimu wa 2024/25 haijawa kwenye mwendo bora katika mechi za hivi karibuni.

