TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya Kocha Mkuu, Hemed Morocco imeandika rekodi ya kufuzu AFCON 2025 Morocco kwa ushindi kwenye mchezo dhidi ya Guinea na kufikisha pointi 10 ikigota nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi H.

Ikumbukwe kwamba Stars ilikuwa ni lazima ishinde mchezo wake dhidi ya Guinea ambao walikuwa washindani wake wakubwa kutoka kundi H ambalo vinara ni Dr Congo na mwisho ilikuwa hivyo katika mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Tanzania 1-0 Guinea bao likifungwa na Simon Msuva nyota wa zamani wa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.
MSIKIE MSUVA SIMON

Nyota Simon Msuva ambaye alikuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Stars Uwanja wa Mkapa kwenye mchezo dhidi ya Guinea alifunga bao lake la ushindi ambalo lilidumu mpaka dakika ya 90 aliweka wazi kuwa ni furaha kubwa kuona haya yanatokeo na malengo ilikuwa kupata ushindi.
“Ninamshukuru Mungu kwa yote na kwa ushindi huu hakika ni furaha, tunawashukuru mashabiki ambao wamekuwa Pamoja nasi nyakati zote hakika wamekuwa wakifanya tujitume na tumepata matokeo jambo ambalo tulikuwa tunalihitaji hivyo wazidi kuwa nasi nyakati zote.”
Ikumbukwe kwamba Msuva alipata nafasi ya kufunga pia kwenye mchezo dhidi ya Ethiopia ugenini wakati Stars ikishinda mabao 2-0 kwenye mchezo huo walipokomba pointi tatu na kufikisha jumla ya pointi 7 kibindoni. Bao jingine lilifungwa na kiungo wa kazi Feisal Salum.
GUINEA ALITULIZWA NAMNA HII

Kwenye mchezo wa kundi H, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilikata tiketi kufuzu AFCON 2025 kwa ushindi dhidi ya Guinea ambao hawa walikuwa wakipambana kupata angala sare ili kufuzu hatua hiyo kubwa.
Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Tanzania 1-0 Guinea. Bao la ushindi katika lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 62 na alionyeshwa kadi ya njano baada ya kushangilia kwa kuvua jezi.
Ni Mudathir Yahya alitoa pasi iliyomkuta Msuva akiwa ndani ya 18 na kumtungua Mousa Camara.
Hongera Taifa Stars chini ya nahodha Mbwana Samatta, hongera mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa.

REKODI ZA WAZAWA
Wakati timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ikifuzu AFCON 2025 kutoka kundi H ikiwa na pointi 10 rekodi zinaonyesha kuwa benchi la ufundi lipo chini ya wazawa ambao wamekuwa katika mwendo mzuri.
Ni Hemed Morocco yeye ni Kocha Mkuu akiwa na Juma Mgunda ambaye ni msaidizi wamefanya kazi kubwa kuwaongoza wachezaji kumaliza nafasi ya pili na pointi 10.
2019 chini ya Emmanuel Ammunike raia wa Nigeria Stars baada ya kucheza mechi 6 iligotea nafasi ya pili na pointi 8 vinara walikuwa Uganda pointi 13.
2023 ilikuwa chini ya Adel Amrouche raia wa Algeria nafasi ya pili na pointi 8 vinara Algeria pointi 16. 1979 ilikuwa chini ya Slawomir Wolk raia wa Poland wakati ule kufuzu ilikuwa kwa mtoano.
NENO LA MAMA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliandika ujumbe kupitia mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na instgram namna hii: “Tukiwa katika majonzi na kazi ikiendelea katika kuwatafuta ndugu zetu ambao tunaamini bado wako hai kufuatia kuporomoka kwa jengo eneo la Kariakoo, ninawapongeza vijana wetu Taifa Stars kwa ushindi na kufuzu kushiriki Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
“Mmeandika historia kwa Taifa letu, ikiwa ni mara yetu ya nne kufikia mafanikio haya makubwa katika kipindi cha zaidi ya miaka arobaini. Hongera kwa kazi nzuri nyote tuliowapa dhamana kusimama na vijana wetu kukamilisha jukumu hili katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Benchi la Ufundi na Watanzania wote kwa kuendelea kuipenda, kuithamini na kuipa hamasa Timu ya Taifa. Baada ya ushindi huu, sasa tujikite katika maandalizi mazuri zaidi kwa mashindano yajayo.”
ZAWADI YA MILIONI 700
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Ndumbaro amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi ya Milioni 700 kwa kufuzu AFCON 2025 Morocco.
“Tunawapongeza wachezaji na benchi la ufundi kwa kupata ushindi na kufuzu AFCON 2025, mama ametoa zawadi ya milioni 700 na tayari fedha hizi zipo kwenye akaunti ya wizara ya michezo kilichobaki ni kuwafikia ninyi.”

