MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa hakuna wa kumlaumu baada ya kushuhudia ubao wa Uwanja wa Azam Complex, Novemba 6 2024 ukisoma Yanga 1-3 Tabora United ambao walikomba pointi tatu mazima kwenye mchezo hio wa ligi. Ushindi kwa Tabora United umebutua mkakati wa Yanga kuishusha Simba nafasi ya kwanza.
Ikumbukwe kwamba unakuwa mchezo wa pili kwa Yanga kupoteza msimu wa 2024/25 baada ya mchezo wa kwanza kupoteza mbele ya Azam FC, matajiri wa Dar. Ndani ya dakika 180 Yanga imekwama kupata ushindi kwenye mechi za ligi ikipoteza pointi sita za ushindani.
Ipo wazi kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ni mabingwa watetezi wa taji la ligi wakipambana kurejesha kwa mara nyingine tena Jangwani. Ni pointi 80 waligotea ndani ya 2023/24 kwenye mechi 30 ambazo walicheza uwanjani.
MASTA GAMONDI MSIKIE

Gamondi amebainisha kuwa walikuwa na nafasi za kufunga zaidi ya mbili katika mchezo wao lakini hawakazutumia ipasavyo jambo lililofanya wapinzani wao kutumia nafasi walizopata kufunga mabao.
“Kwa kilichotokea hakuna wa kumlaumu kwani kila mmoja ametimiza majukumu yake ikiwa nitasema nianze kulalamika, haiwezi kuwa sawa kwani huu ni mpira na unaonekana wazi kwa kila mmoja ambaye anafuatilia ilikuwa hivyo ndani ya uwanja.
“Tulitengeneza nafasi zaidi ya mbili ila hazikutumika mfano Kennedy Musonda alipata nafasi ya kufunga kwenye mchezo ila hakufunga unaona namna ilivyokuwa kwenye mchezo wetu ambao tulikuwa tunahitaji kupata matokeo mazuri. Usisahau kwamba tulipata penalti nayo tulikosa.
“Kwa kilichotokea siwezi kulaumu wachezaji ila tazama pia ratiba yetu tuna mechi sita ndani ya siku 20 na bado kalenda ya kimataifa wachezaji wanasafiri nchi mbili hadi tatu, wakirudi ni kama tunaanza upya.
“Hata ukiangalia idadi ya wachezaji ambao wanatoka Yanga kwenda kwenye majukumu ya timu zao za taifa ni zaidi ya 10 hivyo ni kikosi cha kwanza kinaondoka, idadi ya wale wanaobaki hauwezi kusema unafanya mazoezi haitakuwa hivyo.”
HAWA HAPA WATUPIAJI AZAM COMPLEX

Kipa namba moja wa Yanga, Djigui Diarra atawakumbuka nyota wawili ambao walimfunga kwenye mchezo dhidi ya Tabora United wakati wakipoteza pointi tatu na kuambulia bao moja ugenini baada ya dakika 90.
Ni Offen Chikola huyu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo alifunga mabao mawili dakika ya 19, 45 na bao moja likifungwa na Nelson Muganda dakika ya 77. Bao la pili la Chikola alifunga dakika moja baada ya Aziz Ki kukosa penalty iliyosababishwa na Pacome.
Kwa upande wa Yanga ni Clement Mzize alipachika bao pekee la kufutia machozi dakika ya 90 katika mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa. Hivyo dakika 90 zilikamilika mabao manne yakifungwa.
SILLAH NAYE NDANI

Nyota Gibril Sillah wa Azam FC huyu anaingia kwenye orodha ya nyota wa kwanza kuifunga Yanga ndani ya ligi msimu wa 2024/25 kwa kuwa ilicheza mechi 8 mfululizo bila kupoteza mpaka walipokutana na Azam FC huku Sillah akifunga bao hilo dakika ya 33.
HUYU HAPA KAMWE

ALI Kamwe, Meneje wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga amesema hawakuwa na mchezo mzuri tangu dakika ya kwanza mbele ya Tabora United hivyo wameyapokea matokeo kinyonge wanaamini watarejea kwenye ubora.
Mchezo wa kwanza kupoteza msimu wa 2024/25 ilikuwa ni Novemba 2 2024 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Yanga 0-1 Azam FC hivyo katika mechi mbili mfululizo ambazo ni dakika 180, Yanga imepoteza pointi sita ilizokuwa inasaka ndani ya uwanja.
Kamwe amesema kuwa wanatambua mashabiki, wachezaji na viongozi hawafurahii matokeo hayo kwa kuwa hayakuwa kwenye mpango hivyo wanaamini yatapita na Maisha yataendelea.
“Hiki ni kipindi cha mpito kwa kweli hakuna ambaye alitegemea matokeo ya aina haya, hatukuwa na mchezo mzuri tangu mwanzo wa mchezo wetu dhidi ya Tabora United kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya 90.
“Kilichotokea ni mpira na tunaamini kwamba benchi la ufundi limeona na makosa yatakwenda kufanyiwa kazi tunaamini kwamba tutarejea tukiwa imara zaidi kwenye mechi zijazo hilo linawezekana.”
Kwenye msimamo, Yanga ni namba mbili ikiwa na pointi 24 baada ya kucheza mechi 10 vinara ni Simba wana pointi 25 nao pia wamecheza mechi 10.

