Bacca kwa hewaBacca kwa hewa

MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa mpango mkubwa ni kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tabora United unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex Novemba 7 2024 ikiwa ni mzunguko wa kwanza ndani ya msimu wa 2024/25 na mkakati mkubwa kurejea namba moja kwenye msimamo wa ligi.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa baada ya kucheza mechi 9 imepoteza mchezo mmoja ilikuwa Novemba 2 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Yanga 0-1 Azam FC bao la ushindi kwa Azam FC lilifungwa na Gibril Sillah dakika ya 33.

MIGUEL Gamondi
Gamondi Miguel, Kocha Mkuu wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

amebainisha kuwa wana kazi kubwa ya kufanya kwenye mchezo wao wa ligi dhidi ya Tabora jambo ambalo wamelifanyia kazi kwa umakini mkubwa hivyo wataingia uwanjani kwa tahadhari kusaka ushindi mbele ya wapinzani wao hao.

“Tuna mchezo mgumu dhidi ya Tabora United, tumewafuatilia wapinzani wetu sio timu mbaya ni nzuri hasa kwenye mechi zake zilizopita ilipata matokeo hii ina maana kwamba wamekuwa kwenye ubora kwa hivi karibuni tunalitambua hilo.

“Ushindi kwenye mchezo wetu utatupa nafasi ya kuwa namba moja kwenye ligi hii inamaanisha kwamba ili tuongoze ni lazima tushinde. Tumefanya maandalizi mazuri na wachezaji wapo tayari kwa ajili ya mchezo wetu.”

NYOTA wa Yanga
NYOTA wa Yanga, Prince Dube, Aziz Ki na Mudathir kwenye moja ya mchezo wa ushindani. Source: Yanga.

Yanga imekusanya pointi 24 baada ya mechi 9 kwenye msimamo ni nafasi ya pili huku kinara akiwa ni Simba mwenye pointi 25 baada ya kucheza jumla ya mechi 10 kwenye ligi.

Tabora United ipo nafasi ya 6 kwenye msimamo ikiwa imekusanya pointi 14 baada ya kucheza jumla ya mechi 10. Mchezo wao uliopita ilikuwa Novemba 4 ubao wa Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi ulisoma Tabora United 1-0 Mashujaa bao la ushindi likifungwa na Morice Chukwu.

SIMBA KUSHUSHWA KIMKAKATI

Ikiwa Yanga itapata ushindi kwenye mchezo wa leo itaishusha Simbainayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids  kimkakati wa pointi kutokana na tofauti yao iliyopo kwa sasa kwa kuwa Simba ipo nafasi ya kwanza na pointi 25 huku Yanga ikiwa nafasi ya pili na pointi 24.

FADLU
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids 2024/25. Source: Simba.

Mkakati maalumu wa kuishusha ni ushindi utakaoifanya Yanga kufikisha pointi 27 na kuwa tofauti kwa pointi mbili pekee lakini zote zitakuwa zimecheza mechi 10 na kama ikitokea mkakati wa kuvuna alama moja bado Simba ina nafasi ya kuwa namba moja kutokana na faida ya mabao mengi ya kufunga.

Hivyo dakika 90 zitaamua kwa kuwa mpira una matokeo yote matatu, ushindi, sare na kupoteza kwani Tabora United nao mkakati wao ni kuvuna pointi tatu.

MKWARA WA TABORA UNITED

Khalfan Mbonde, Kocha wa magolikipa wa Tabora United amesema kuwa wamefanya maandalizi kwa umakini ili kupata matokeo mazuri mbele ya Yanga licha ya kutoka kucheza mchezo mgumu hivi karibuni ndani ya Ligi Kuu Bara.

“Tumetoka kucheza mchezo mgumu hivi karibuni lakini tumefanya maandalizi mazuri kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Yanga, tunawaheshimu wapinzani wetu na tupo tayari kwa mchezo muhimu.”

 

HUYU HAPA KIBABAGE

Beki wa Yanga, Nickson Kibabage amebainisha kuwa wanatambua mchezo wao dhidi ya Tabora United hautakuwa mwepesi kutokana na mwendo wa timu hiyo yenye safu ya ushambuliaji makini kwenye kusakama lango.

“Tabora United ni timu nzuri na imara kwenye eneo la ushambuliaji. Tumefuatilia mechi zake zilizopita namna ambavyo imekuwa ikipata matokeo na aina ya washambuliaji wake sio wa kubeza hasa kwenye eneo hilo. Kuna mchezaji Heritier Makambo huyu ni mshambuliaji mzuri na anafanya kazi yake hiyo.

“Kwa maana hiyo kwenye eneo la ulinzi mabeki tutakuwa na kazi ya kuwazuia sio mabeki tu bali timu nzima kiujuma tutafanya kazi kwa ushirikiano kwa kuwa ambacho tunahitaji ni pointi tatu muhimu kwenye mchezo wetu.

“Matokeo ya mchezo wetu uliopita hayo tumesahau na sasa akili zetu ni kwenye mchezo wetu ujao dhidi ya Tabora United. Kilichotokea hatuwezi kukibadili hivyo ni muhimu kuwa makini zaidi kwenye mchezo wetu mwingine na maandalizi tumefanya kwa umakini mkubwa.”

KITASA CHA KAZI KUKOSEKANA

 

Bacca
Bacca beki wa kazi wa Yanga mwenye mabao mawili ndani ya ligi 2024/25. Source: Yanga.

Ibrahim Bacca, kitasa cha kazi ndani ya Yanga hakikatakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Tabora United kutokana na adhabu ya kadi nyekundu ambayo aliipata Novemba 2 2024 kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.

Rekodi zinaonyesha kuwa Bacca kwa msimu wa 2024/25 anakuwa nyota wa kwanza ndani ya kikosi cha Yanga kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi Ahmed Arajiga katika mchezo uliopita ambapo ilikuwa ni dakika ya 21.

Mchezo huo wa 9 ulikuwa ni wa kwanza kwa Yanga kupoteza kwa kuwa ni mechi 8 mfululizo ambazo ni dakika 720 ilicheza bila kuruhusu bao ndani ya uwanja kwenye mechi za ligi.

Share this: