Semaji la SimbaSemaji la Simba
Fadlu
Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba 2024/25. Source: Simba.

KAZI inaanza kuelekea Kariakoo Dabi kwenye mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Agosti 8 kwa wababe hao kukutana kusaka mshindi atakayecheza fainali inayotarajiwa kuwa Agosti 11 2024. Hiyo ni baada ya watani hao wa jadi  kukamilisha kazi ya utambulisho wa wachezaji wao, benchi la ufundi, uzi mpya na kurejesha kwa jamii ambapo Simba kauli mbio yao ilikuwa Ubaya Ubwela.

Fadlu Davids, Kocha Mkuu wa Simba ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili. Mchezo wa kwanza kwa kocha huyo akiwa ardhi ya Tanzania ilikuwa Agosti 3 2024 katika Simba Day aliposhuhudia ubao ukisoma Simba 2-0 APR ya Rwanda.

Kocha huyo amesema: “Kila mchezaji anapenda kuona tunapata matokeo kwenye mechi ambazo tunacheza, baada ya kukamilisha mchezo wetu dhidi ya APR tunakwenda kujiandaa kwa ajili ya Kariakoo Dabi. Kikubwa ni kuwa tayari kwa ajili ya mchezo makosa ambayo tumeyafanya tunakwenda kufanyia kazi.”

MUASISI WA SIMBA DAY AKABIDHIWA TUZO

Dalali na Mo
MO Dewji na Dalali muasisi wa Simba Day. Source: Simba.

Kwenye tukio la Simba Day, Ubaya Ubwela kilele chake Agosti 2024 Hassan Dalali ambaye alikuwa mwenyekiti wa zamani wa timu hiyo na muasisi wa Simba Day alikabidhiwa tuzo ya heshima kutoka kwa Rais wa Simba, Mohammed Dewji mbele ya mashabiki wengi waliojitokeza Uwanja wa Mkapa kushuhudia burudani katika siku ya Simba Day.

Muasis huyo wa tamasha la Simba Day ametaja sababu kubwa iliyopelekea kuanzishwa kwa tamasha hilo ambalo linazidi kuwa bora kila wakati kutokana na mapokeo mazuri kwa mashabiki na wafuatilia wa mpira duniani kote.

“Mimi ni muasisi wa Simba Day nakumbuka ilikuwa mwaka 2007  hatukuwa na hela kwa ajili ya kiwanja na ilikuwa kama milioni 107 hivyo nikawaza kwa nini tusiwe na tamasha la Simba Day ambalo mashabiki watakuja waone jezi mpya, wawaone wachezaji wao lakini fedha ambazo zitapatikana zianze kupunguza gharama za kiwanja?

“Hapo tukaanza wazo hilo na ninamshukuru Mungu imekuwa vizuri na linaingia kwenye orodha ya mtaamasha makubwa duniani ukiacha Kombe la Dunia, Simba Day linaingia namba nne hivi kutokana na kupokelewa vizuri na mashabiki na wengine wamefuata hili ni jambo kubwa.’ amesema.

Ipo wazi kuwa Agosti 3 ilikuwa ni Simba Day ya 16 ambapo Uwanja wa Mkapa mashabiki walijitokeza wengi na tiketi ilikuwa ni Sold Out mapema siku mbili kabla ya tukio hilo kubwa kwenye ulimwengu wa michezo.

WATUPIAJI SIMBA

Balua
EDWIN Balua nyota wa Simba akishangalia bao alilofunga dhidi ya APR 2024 Simba Day. Source: Simba.

Katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya APR wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 APR yote yalifungwa kipindi cha pili cha mchezo huo baada ya dakika 45 za awali kuwa 0-0. Ni Fernandes Debora alianza kufunga dakika ya 46, Edwin Balua alipachika bao la pili dakika ya 66 kwenye mchezo huo.

BURUDANI ILIKUWA NOMANOMA

Zilitolewa burudani kwa mpangilio mkubwa kutoka kwa wasanii wakubwa Afrika Mashariki na kati ikiwa ni pamoja na Ali Kiba ambaye wengi wanapenda kumuita King Kiba. Huyu alitoa burudani kwa mashabiki na wimbo wa Unyama ni Mwingi ulipokelewa vizuri na mashabiki wengi.

Ukiweka kando Kiba mwamba wa Kasakazin Joh Makini alitoa burudani kwa mashabiki wa Simba na Chino Man Wan naye aliwaambisha jukwaani mwanzo mwisho ikiwa ni burudani za maana kabisa Simba Day.

JESHI LA MTU MMOJA

Ahmed Ally
Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari Simba kwenye Simba Day 2024. Source: Simba.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari ni jeshi la mtu mmoja ambaye alipanda jukwaani kwa mtindo wake akiwa amevaa mavazi ya Kimaasai kutangaza utamaduni wa Kitanzania duniani jambo ambalo liliongeza mvuto pamoja na msafara wake wote walivaa mavazi hayo yaliyokuwa kwenye mpangilio mzuri.

Ni yeye alisimamia zoezi zima la utambulisho wa wachezaji wa Ubaya Ubwela wa timu hiyo na benchi la ufundi kwa mpangilio mkubwa akitamba kwamba watafanya vizuri kwenye mashindano ambayo watashiriki kitaifa na kimataifa ndani ya uwanja.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 Simba iligotea nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya mechi 30 ikiwa na pointi 69 itapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Coastal Union ya Tanga iliyogotea nafasi ya nne.

“Wachezaji wote wa Simba wapo tayari kwa ajili ya msimu mpya wa 2024/25 na tunatambua kwamba msimu uliopita haukuwa mzuri kwetu kutokana na kushindwa kufikia malengo yetu lakini tunaanza upya kuyakimbiza malengo yetu hilo inawezekana.’

“Mashabiki tunawashukuru kwa kujitokeza kwenu kwenye tamasha hili la Simba Day mmeonyesha namna ambavyo mpo pamoja na timu kila nyakati. Mmeacha shughuli zenu muhimu na kuja hapa Uwanja wa Mkapa kwa hili tunasema asanteni sana mashabiki nyinyi ni watu muhimu kwelikweli.”

FOUNTAIN GATE HAWAPOI

Wakati Simba ikikamilisha Simba Day bado kuna matamasha yanaendelea kuja ikiwa ni pamoja na lile la Fountain Gate, Agosti 9 2024  ambapo hiyo itakuwa ni siku ya Tanzanites Day ambayo ni maalum kwa ajili ya kutambulisha wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo. Tamasha hilo litafanyika katika uwanja wa nyumbani wa timu hiyo Tanzanite Kwaraa Stadium ambapo itachezwa mechi dhidi ya Gor Mahia na Kauli mbiu ya tamasha hilo ni Kama Mbwai iwe Mbwai

PAMBA DAY HAWA HAPA

Mbali na Yanga kukamilisha Wiki ya Mwananchi Agosti 4,  Agosti 10 itakuwa ni Pamba Day na Kauli mbio ya Pamba ni Mbelembele ambapo wao Pamba tamasha lao itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

 

Share this: