
MASHINE za kazi bado zinatarajiwa kutambulishwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa ajili ya kuwa kwenye changamoto mpya kwa msimu wa 2024/25 unaotarajiwa kuanza Agosti 16 2024.
Timu hiyo inanolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi baada ya mechi 30 ambazo ni dakika 2,700 ilikusanya jumla ya pointi 80. Itapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kazi kubwa ambayo inafanywa na Yanga kwa sasa ni kuimarisha kikosi hicho kwenye kila idara. Nguvu kubwa kwenye eneo la ushambuliaji wakianza kumuongeza mwamba Prince Dube aliyekuwa anacheza Azam FC msimu wa 2023/24.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanafanya maboresho kwenye kikosi hicho ili kuwa imara kwa ajili ya mechi za ushindani kitaifa na kimataifa.
“Kazi kubwa inafanyika kwenye upande wa maboresho ya kikosi ambapo katika kila idara tunafanya maboresho kuwa imara na bora. Kuna washambuliaji ambao wanakuja na watatambulishwa kwa kuwa wapo.
“Yupo Prince Dube, Clement Mzize kwenye eneo la ushambuliaji hivyo tunaamini kwamba washambuliaji wengine wanakuja kwa ajili ya kuongeza nguvu eneo la ushambuliaji hivyo tunaamini kwamba tutakuwa bora kila eneo.
Miongoni mwa washambuliaji wanaotajwa kuwa kwenye hesabu za Yanga ni Jean Baleke aliyewahi kucheza Simba msimu wa 2023/24 na alipokutana na Thank You alikuwa kafunga jumla ya mabao 8.
MASHINE YA KAZI CHAMA

Katika utambulisho wa mashine za kazi kuelekea 2024/25 yupo kiungo mshambuliaji Clatous Chama tayari amesharipoti kambini na kuendelea na mazoezi kuelekea msimu mpya ambapo awali alikabidhiwa jezi namba 20 iliyokuwa inavaliwa na Zawad Mauya.
Ipo wazi kwamba Chama ni mchezaji wa kwanza kutambulishwa Yanga ilikuwa Julai Mosi 2024 msimu wa 2023/24 alikuwa kwa watani zao wa jadi Simba. Ndani ya kikosi cha Simba alifunga mabao 7 na kutoa pasi 6 za mabao.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa kiungo huyo amekabidhiwa jezi namba 17 kwa mpango kazi maalumu kuendelea kutimiza majukumu yake kwa umakini.
“Chama amekabidhiwa jezi namba 17 kutoka kwa Farid Mussa hii ni kazi nyingine kwake kwa ajili ya kutimiza majukumu yake na tunataka wale wasimsahau haraka wakimuona uwanjani.
“Chama ni yuleyule, uwezo wake ni uleule na amesema kuwa ana jambo lake hivyo ni jambo la kusubiria namna gani itakuwa kikubwa ni kuwa na subira.”
MASHINE ZENYE UHAKIKA KUWA YANGA
Ukiweka kando mashine mpya ambazo zinatarajiwa kutambulishwa hivi karibuni kuna wachezaji wengine tayari wameshatambulishwa ndani ya Yanga. Wapo ambao ni wapya na wengine kandarasi zao zimeboreshwa.
DJIGUI
Anaitwa Djigui Diarra wengi hupenda kumuita mdaka mishale yeye Julai 5 mkataba wake uliongezwa. Ni kutoka 2024 mpaka 2027. Nyota huyo raia wa Mali ni chaguo la kwanza la Gamondi.
NONDO
Nahodha Bakari Mwamnyeto bado ana uhakika wa kuwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa msimu mpya ujao. Ni Julai 3 alitangazwa kuongeza mkataba mwingine utakaomfaya awepo hapo mpaka 2026.
KIBABAGE
Julai 4 ilikuwa ni kwa Nickson Kibabage ambaye aliongezewa kandarasi nyingine.Kutoka 2024 yupo mpaka 2027 ndani ya kikosi hicho. Yeye ni mbavu ya kushoto.
MSHERY
Aboutwalib Mshery ambaye alisajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar Julai 4 ilitangazwa kuwa bado ni njano na kijani baada ya kuongeza mkataba wake. kipa huyo ni mpaka 2027.
MASHINE YA 7/7

Usiku wa kuamkia Julai 7 2024 ilitolewa zawadi ya 7/7 kwa mashabiki wa Yanga kwa utambulisho wa mshambuliaji Prince Dube kuwa ni mali ya Yanga.
BOKA
Beki wa kushoto kutoka FC Lupopo anaitwa Boka Chadrak alitambulishwa usiku wa kuamkia Julai 8. Anakuja kuwa mbadala wa Joyce Lomalisa ambaye hatakuwa ndani ya kikosi cha Yanga kwa msimu wa 2024/25 baada ya mkataba wake kugota mwisho.
KHOMEINY
Mwanzo wa siku mpya mapema kabisa ilikuwa Julai 8 2024 Yanga walimtambulisha kipa Aboubhakar Khomeiny ambaye msimu wa 2023/24 alikuwa ndani ya Ihefu.
KIBWANA
Kibwana Shomary beki wa kushoto yupo ndani ya Yanga baada ya mkataba wake kufanyiwa maboresho kutoka 2024 mpaka 2026 hivyo bado atazidi kuwa ndani ya Jangwani. Ilikuwa ni Julai 9 2024 alitambulishwa.

