SIMBA-Saido NtibaSaido Ntiba

 

https://sportpesa.co.tz/SIMBA
Jean Baleke (kushoto)

TETESI za usajili wa dirisha kubwa zinazidi kupamba moto ambapo taarifa inayoendelea kushika kasi kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ni kuhusu staa wa zamani wa Simba Mkongomani, Jean Othos Baleke ambaye ameziingiza vitani klabu za Yanga na Azam mara baada ya kuweka wazi kuwa yupo tayari kurejea kucheza soka Tanzania.

Baleke amekiri kuwa yupo kwenye mazungumzo na mabingwa wa Ligi Kuu Bara wanaodhaminiwa na Kampuni ya michezo ya SportPesa Yanga na Azam kwa ajili ya kujiunga nao msimu ujao mara baada ya kuhudumu kwa mafanikio makubwa ndani ya kikosi cha Al Ittihad ya Libya. Baleke aliondoka Simba katikati ya msimu huu katika dirisha dogo akiwa tayari ameifungia timu hiyo mabao nane.

Staa huyo yupo nchini akiwa katika mazungumzo na timu hizo mbili za Dar es Salaam, Azam na Yanga, ambapo kabla ya kujiunga na Simba alikuwa akihudumu  kwa mkopo akitokea TP Mazembe kabla ya kutimkia Al Ittihad ya Libya Januari mwaka huu.

SIMBA NINI KINAENDELEA?

SIMBA
Shaffih Dauda

Ndani ya Simba kwa sasa moto unazidi kuwaka ambapo kuna sintofahamu kubwa kwa baadhi ya viongozi wa timu hiyo kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni mwenendo mbaya wa kikosi cha timu hiyo ambacho kimekosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo, huku msimu huu wakimaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kukosa nafasi ya kushiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Kufuatia sakata hilo kumekuwa na maoni tofauti ya wadau wa michezo ambapo miongoni mwa waliotoa maoni yao ni mchambuzi wa habari za michezo, Shaffih Dauda ambaye amesema: “Tatizo la Simba kwa miaka yote ni MOHAMMED DEWJI ‘MO’ mwenyewe.

“Wakati watu wengi wanajiuliza tatizo la Simba ni nini? Jibu ni jepesi sana, tatizo kubwa la Simba ni Mohammed Dewji ‘Mo’! Lengo kubwa la huyu bwana ni kutaka kuwa mmiliko wa Simba na mara kadhaa ameshajitangaza hivyo.

“Habari ya kuwa mwekezaji wa Simba kwa 49% hataki kabisa kuisikia, anatengeneza mazingira ya kuipiga ‘shot’ Simba hadi lengo lake la kuimiliki klabu litimie.

“Ifike wakati Mo akubali kuwa mwekezaji wa Simba au kama vipi akaanzishe timu au anunue timu ili atimize lengo lake la kuwa mmiliki wa klabu.

“Anaposema kuna watu wanamkwamisha anamaanisha wanamkwamisha kuimiliki Simba sio kuwekeza. Kama ni kuwekeza mchakato ungekuwa umeshakamilika miaka mingi nyuma lakini yeye anataka kuwa mmiliki zaidi ya 51%.

“Hata uendeshaji wa timu ni wa kienyeji tangu mwaka 2018 huku yeye akiwa kama mmiliki na hujitambulisha hivyo kote duniani.”

AZIM DEWJI ASHUSHA PRESHA

 https://blog.sportpesa.co.tz/
Mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji

Mfadhili wa zamani, Azim Dewji amewatuliza mashabiki wa timu hiyo kwa kuomba kuacha kuendelea kuwashurutisha viongozi wao kujiuzulu akisema hatua hiyo itaibomoa timu yao.

Dewji ameyasema hayo kufuatia malumbano ya uongozi yanayoendelea ndani ya klabu hiyo, ambapo amewashauri viongozi wa Simba kujitokeza hadharani haraka kuwatuliza mashabiki wao, huku akiwataka pia kuhakikisha wanasimamia vizuri usajili wa dirisha kubwa sambamba na kutafuta kocha ambaye atakaa kwa muda mrefu badala ya kuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakiiathiri timu hiyo.

“Binafsi nawaomba mashabiki watulie, ni kweli hatujawa na msimu mzuri lakini hii isitusahaulishe kuwa hata msimu huu tumezidiwa magoli tu, na Azam ambao wamemaliza nafasi ya pili hivyo hatuko vibaya sana.

“Ni kweli kunaweza kuwa na shida mahali kwenye uongozi lakini kufukuzana sio suluhisho, tunapaswa kukaa chini na kumaliza changamoto ambazo tunazo ili kurejesha ufalme ambao tumekuwa nao.”

AHMED ATANGAZA MAZURI YANAKUJA

SIMBA
Ahmed Ally

Kuhusiana na yale yanayoendelea ndani ya timu hiyo Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema: “Kumekua na ukimya wa taarifa kutoka kwenye timu yetu kiasi cha kuzua hofu kidogo, usahihi ni kwamba mipango na mikakati thabiti inaendelea na itakapokua tayari wote mtajulishwa

“Jambo la kufurahisha ni kwamba mipango yote inatekelezwa kwa ustadi na ufanisi wa hali ya juu mnoo. Malengo tuliyojiwekea ya kuboresha timu yetu yamefikiwa kwa asilimia kubwa kwa maana ya kwamba mipango yetu kwenye soko la usajili iko vizuri sana

“Niwaombe tutulie, la mgambo likilia tutafahamu kila kitu kuhusu timi yetu pendwa.”

Share this:

By Joel Thomas

Joel Thomas is a Tanzanian sports writer with a BSc (Education) from Mwenge Catholic University. He spent 4 years at Global Publishers and is in his second year with SportPesa, covering football and betting education for local fans. Anapenda soka na anaandika kwa uwajibikaji.