KUMEKUCHA ndani ya Simba iliyomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi 59 baada ya kucheza mechi 30 ambazo ni dakika 2,700 huku ukuta wao ukiruhusu mabao 25 na safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 59 ndani ya ligi. Kuna mastaa ambao wanatajwa kwamba watasepa mazima huku wengine wakianza kuaga.
Hivi karibuni Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally aliweka wazi kuwa kuna wachezaji ambao wataondoka msimu utakapoisha na wapo ambao wataongezewa mikataba yao hivyo ni jambo la kusubiri na kuona itakavyokuwa.
“Kuna wachezaji ambao wataondoka mwishoni mwa msimu na wapo ambao wataongezewa mikataba ipo hivyo lakini kinachofanyika kwa sasa ni uongozi kuzungumza na wale wachezaji ambao mikataba yao inaisha kuboresha na mchezaji ambaye anahitajika na Simba hataondoka, mashabiki wasiwe na mashaka hatushindwi.”.
Hapa tunakuletea baadhi ya wachezaji ambao wanatajwa kuwa kwenye hesabu za kusepa na wengine tayari wameshaaga mazima ndani ya timu hiyo inayonolewa na Juma Mgunda namna hii:-
BOCCO

John Bocco nahodha wa Simba amewaaga mashabiki na viongozi hivyo hatakuwa sehemu ya wachezaji ndani ya msimu mpya wa 2024/25 katika mechi za ushindani.
Mei 28 2024 kupitia ukurasa wake rasmi wa Instagram, Bocco alitupia video akiwa na uzi wa mnyama kisha akaachia ujumbe uliosomeka, First & Last, Thank You Lion. Ujumbe huo ukiwa ni moja ya dalili zinaonyesha kuwa tayari amewaaga mashabiki wa Simba.
Bocco ni miongoni mwa wachezaji bora kupata nafasi ya kucheza soka la ushindani Bongo akiwa ni mfungaji bora wa muda wote akifunga zaidi ya mabao 100 ndani ya ligi.
Kimataifa wakati Simba ikitinga hatua ya makundi msimu wa 2023/24 anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa akishirikiana na wachezaji wenzake dhidi ya Power Dynamos ulivyowachanganya mabeki wakajifunga.
Ni wazi kuwa hakuwa chaguo la kwanza ndani ya Simba kwenye mechi za ligi kutokana na kile ambacho kilielezwa kwamba alipata maumivu kwenye maandalizi ya Mapinduzi 2024. Alikuwa akikinoa kikosi cha Simba timu ya vijana kwenye alipokuwa nje ya uwanja.
SAIDO

Mkali wa kazi ngumu ambaye anavuja jasho kwenye mechi za kitaifa na kimataifa kutokana na uzoefu wake anatajwa kwamba atasepa. Ni Saido Ntibanzokiza mkali wa mapigo huru ndani ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2023/24.
Mabao 11 kafunga akiwa ni namba moja kwa wakali wa kucheka na nyavu Simba iliyofunga mabao 59 baada ya kucheza mechi 30. Nyota huyo kafunga mabao 7 kwa penalti akiwa ni mchezaji namba moja kufunga mabao mengi kwa penalti.
Ipo wazi kwamba Simba imegota nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 69. Msimu wa 2024/25 itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuporomoka kutoka nafasi ya pili iliyogotea msimu wa 2022/23 nafasi ya kwanza ni mabingwa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa.
Nyota huyo inaelezwa kwamba tayari amewaaga wachezaji wenzake hivyo hatakuwa kwenye kikosi cha Simba msimu mpya. Ikumbukwe kwamba kwenye moja ya mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold alipofunga mabao mawili aliweka wazi kuwa kuna mengi yanasemwa lakini watazidi kupambana.
“Kuna mengi ambayo yanasemwa lakini hakuna namna ni muhimu kupambana ili kufikia malengo ambayo tunahitaji. Wakati ukifika kila kitu kitakuwa wazi hivyo tunajua kile ambacho tunakitafuta.”
NGOMA
Nyota wa kazi ambaye ni chaguo la kwanza ndani ya kikosi cha Simba Fabrice Ngoma anatajwa kuwa miongoni mwa wale ambao wataondoka. Ikumbukwe kwamba kiungo huyo ni miongoni mwa wale waliofunga kwenye Mzizima Dabi.
Wakati ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Azam FC 0-3 Simba mwamba anaingia kwenye orodha ya nyota waliolifunga kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa. Taarifa zimeeleza kuwa sababu ya nyota huyo kuhitaji kusepa ni ofa ambazo zipo mkononi hivyo kama kila kitu kitakwenda sawa anaweza kuondoka.
LAKRED
Hakuwa anaaminiwa sana alipokuja Bongo kutokana na kufanya makosa kwenye mechi za awali alipopata nafasi. Chini ya Kocha Mkuu Robert Oliveira zama zile alianza kwa kuruhusu mabao kwenye mechi za kimataifa ilikuwa dhidi ya Power Dynamos.
Wakati hayo yakitokea ikumbukwe kwamba Aishi Manula hakuwa fiti huku kipa Ally Salim bado alikuwa hajawa imara kwenye mechi kubwa jambo lililoanza kuleta kelele kwa mashabiki.
Ghafla alianza kurejea kwenye ubora wake na kujihakikishia namba kipa Ayoub Lakred na kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika alifanya kazi kubwa licha ya timu hiyo kugotea hatua ya robo fainali.
Inaelezwa kuwa kuna timu ambazo zinahitaji kupata saini yake kutoka Morocco hivyo uwezekano wa nyota huyo kubaki Simba ni mdogo. Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa Simba unafanya jitihada kubwa kuzungumza naye na ofa wameongeza.
KRAMO
Aubin Kramo msimu wa 2023/24 hajapata zali la kucheza mechi za ushindani kwa kuwa hakuwa fiti.Taratibu ameanza kurejea kwenye ubora wake kiungo huyo wa kazi.
Inaelezwa kuwa jina lake limeondolewa kwenye orodha ya wachezaji wa Simba ambao watacheza mechi za ushindani yupo hapo ili kukamilisha mkataba wake.
Baada ya mchezo wa funga kazi dhidi ya JKT Tanzania, Kramo alibainisha kwamba anaamini bado yupo ndani ya Simba na atafanya kazi kubwa msimu ujao kwa kuwa tayari ameshapona.
INONGA

Moja ya mabeki waliokuwa wakifanya kazi kubwa ndani ya Simba lakini uwezo wake uliporomoka ghafla. Mechi 10 za ligi amecheza na alipata maumivu kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga.
Inatajwa kwamba licha ya mkataba wake kutarajiwa kugota mwisho 2025 yupo kwenye mazungumzo na viongozi wa Simba ili akapate changamoto mpya.
