KAZIGamondi Yanga
MASHUJAA v Yanga
NYOTA wa Yanga na Mashujaa wakiwa uwanjani kwenye moja ya mchezo wa ligi. Source. Yanga

KAZI inaendelea kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga ndani ya msimu wa 2023/24 ambao unakaribia kugota mwisho kutokana na mechi za kukamilishia mzunguko wa pili kuzidi kuyeyuka taratibu.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa imekuwa kwenye mwendo mzuri wakupata matokeo kwenye mechi zake inazocheza ndani ya uwanja.

Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kocha bora Aprili baada ya kucheza mechi 25 imekomba jumla ya pointi 65 kibindoni ikiwa ni namba moja kwenye msimamo inafuatiwa na Azam FC inayofundishwa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo ikiwa nafasi ya pili na ile ya tatu mikononi mwa Simba.

Gamondi amesema kuwa wanatambua mechi ambazo wanacheza ni ngumu kutokana na wapinzani wao kuhitaji pointi tatu lakini watapambana kufanya vizuri kwenye mechi zao zote.

“Ni ngumu na ushindani ni mkubwa kwenye kila mchezo ambao tunacheza hilo lipo wazi kwa sababu tunahitaji pointi tatu ambazo wapinzani wetu nao wanazihitaji pia pointi hizo ambazo ni muhimu kwa kila mmoja.

“Mashabiki wamekuwa pamoja nasi kwenye mechi ambazo tunacheza hili ni kubwa na ninapenda kusema kwao asante sana wanatupa nguvu ya kupambana kwenye mechi ambazo tunacheza iwe ugenini ama nyumbani.”

KITUO KINACHOFUATA KWENYE LIGI

Gamondi Yanga
MIGUEL Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga :Source Yanga

Baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa kwenye mchezo wa mzunguko wa pili kituo kinachofuata ni Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Kagera Sugar unatarajiwa kuchezwa Mei 8 2024.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja kwa timu zote kuwa kwenye hesabu ya kusaka pointi tatu muhimu ndani ya uwanja ikiwa ni lala salama ndani ya msimu wa 2023/24.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Kaitaba, baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 0-0 Yanga. Hivyo kwa wababe hawa wawili walitoshana nguvu mzunguko wa kwanza kila timu inahitaji kupindua meza kibabe.

AZIZ KI KWENYE VITA NYINGINE

Aziz KI
Aziz KI kiungo mshambuliaji wa Yanga mwenye mabao 15 ndani ya ligi :Source Yanga.

Mwamba Aziz KI mwenye tuzo ya mchezaji bora ndani ya Aprili ambaye ni namba moja kwenye utupiaji ndani ya Ligi Kuu Bara yupo kwenye vita yake nyingine nje ya uwanja kuwania tuzo ya ufungaji bora.

Ipo wazi kwamba Aziz KI katupia jumla ya mabao 15 kwenye ligi akiwa ni namba moja kwa mastaa wenye mabao mengi ndani ya Yanga anafuatiwa na Maxi Nzengeli mwenye mabao 9 katika kikosi hicho cha masta Gamondi.

Ni mechi 22 kacheza mwamba Aziz KI kati ya 25 ambazo Yanga imecheza akitengeneza pasi 7 za mabao hivyo kahusika kwenye jumla ya mabao 22 ndani ya kikosi cha Yanga.

Kwenye mechi 22 ambazo kacheza KI kayeyusha dakika 1,730 akiwa na wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 78 uwanjani katika mabao hayo alifunga hat trick moja dhidi ya Azam FC, mzunguko wa kwanza.

Ipo wazi kwamba Yanga imefunga jumla ya mabao 56 kwenye ligi baada ya kucheza jumla ya mechi 25 ambazo ni dakika 2,250 Ki alikosekana kwenye mechi tatu pekee.

Vita yake ni dhidi ya kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum ambaye katupia jumla ya mabao 15 na pasi saba za mabao akiwa ni namba moja kwa wakali wa kucheka na nyavu ndani ya Azam FC.

Fei kacheza jumla ya mechi 24 akikomba dakika 1,992 akiwa ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu Yusuph Dabo kwenye eneo la kiungo mshambuliaji ndani ya timu hiyo ya matajiri wa Dar.

Nyota huyo ana wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 90 na katika mabao hayo 15 bao moja alifunga dhidi ya mabosi wake wa zamani Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa pili uliochezwa Uwanja wa Mkapa.

Ipo wazi kwamba Azam FC imefunga jumla ya mabao 52 ndani ya ligi ambapo Fei kacheza jumla ya mechi 24 akikosekana kwenye mchezo mmoja uwanjani.

HAWA KAGERA SUGAR

Kagera Sugar ndani ya Ligi Kuu Bara sio ya kubeza kwa kuwa ipo ndani ya 10 bora hivyo inapambana kujihakikishia nafasi nzuri ya kumaliza ligi msimu huu ambao una ushindani mkubwa.

Baada ya kucheza jumla ya mechi 25 imekusanya pointi 30 kwenye msimamo ipo nafasi ya 7 inanolewa na Kocha Mkuu Felix Minziro ambaye ameweka wazi kuwa kikubwa ambacho kinahitajika kwenye mechi wanazocheza ni ushindi.

 

 

Share this: