
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya SportPesa wameendelea kuteka mijadala mikubwa huko nchini Afrika Kusini ambapo achana na ishu ya mchezo wao wa leo Ijumaa dhidi ya Mamelodi Sundowns, uongozi wa timu hiyo pia umeendesha kampeni kubwa ya usajili wa Wanachama wapya kuongezea familia yao.
Yanga jana Alhamisi wamefanya tukio kubwa la kusajili Wanachama wapya wa timu hiyo huku pia wakianzisha Tawi jipya linalofahamika kama ‘Tawi la Yanga Afrika Kusini’
Yanga wanatarajia kuvaana na Mamelodi Sundowns leo Ijumaa ya Aprili 5, mwaka huu katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Yanga wanatarajia kuingia katika mchezo huo huku wakiwa na kumbukumbu ya matokeo ya suluhu katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi ya wiki iliyopita.
INJIA HERSI ATOA TAMKO

Akizungumzia hatua hiyo kubwa, Rais wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa, Injina Hersi Said amesema: “Niweke rekodi sawa, sisi tuna matawi lukuki nje ya mipaka ya Tanzania. Kwa Mfano kule Marekani tunalo tawi la uanachama. Tunasisitiza mashabiki wetu nje ya Tanzania kutumia fursa hii ya kufungua account ya Tanzanite ya CRDB ambapo imetufanya kuwa karibu sana Wanachama wetu wa diaspora.
“Niwapongeze sana idara ya habari na Wanachama kwa kuweka mipango mikakati madhubuti ya kampeni ya ‘Twenzetu kwa Madiba’. Ama kwa hakika idara hizi mbili zina watu wenye upeo mkubwa wa maarifa wa kuanzisha agenda zenye dhima kwa Klabu.
“Nichukue nafasi hii kuwashukuru na kuwapongeza sana mashabiki wa Young Africans SC hapa Afrika Kusini na pia niwashukuru wadhamini ambao wamedhamini safari yetu ya Afrika Kusini, ikiwemo kuleta Mashabiki watano ambao wamejishindia kwenye bahati nasibu ya ‘Twenzetu kwa Madiba’.
ALICHOSEMA ALI KAMWE

Akizungumzia tukio hilo Ofisa habari wa timu hiyo, Ali Kamwe alisema: “Wale Mashabiki wetu waliosafiri kwa njia ya basi tayari wameshaingia nchini ya Afrika Kusini. Tunaomba Mashabiki wa hapa Afrika Kusini kujumuika na hawa wenzetu waliotoka Tanzania kwenda kutafuta matokeo uwanjani siku ya Ijumaa.
WANANCHI WA SAUZ WAWAITA MASHABIKI UWANJANI
Katibu wa tawi hilo jipya la Young Africans – Afrika Kusini, Emson Mchau amesema: “Hii ni ndoto ambayo tumeisubiria kwa muda mrefu sana. Tunamshukuru sana Rais wa Young Africans SC Eng.Hersi Said kwa kuitikia wito wetu wa kuzindua tawi hili. Tunasisitiza mashabiki wengine ambao wapo hapa Afrika Kusini wajitokeze kwa wingi.”
KOCHA YANGA ANASEMAJE KUHUSU MCHEZO WAO

Akizungumzia mchezo huo, Gamondi amesema: “Utakuwa mchezo mgumu lakini ni lazima baada ya dakika 90 kuwe na mshindi mmoja. Mpaka sasa mchezo uko 50/50 bado kila timu ina nafasi, hivyo tuko hapa kuhakikisha tunapambana kupata matokeo mazuri. Siwaandai wachezaji wangu kwa ajili ya historia ya Mamelodi, naandaa timu yangu kutokana na dakika 90 zinazokuja.
“Tunaamini kazi tuliyofanya kwenye Uwanja wa mazoezi, tuna imani na wachezaji na Mashabiki wetu, haitakuwa rahisi kwetu na kwao pia. Tuna Wachezaji wenye uzoefu wenye sifa ya kupambana, msimu uliopita kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho walipoteza nyumbani lakini wote mnajua kilichotokea walipokwenda ugenini.
“Huu ni mchezo tofauti lakini watapambana tena kwa ajili ya mashabiki wetu. Tunasubiri kuona itakavyokuwa kwenye mazoezi ya mwisho, tunaweza kumpata mchezaji katika wale waliokuwa majeruhi. Ni kweli tunaiwaza nusu fainali ya CAF lakini tunajali pia na usalama wa afya za wachezaji wetu pia. Young Africans haichezi mashindano haya peke yake.
“Mechi yangu ya mwisho hapa Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Loftus, nilikuwa Kocha wa Platinum Stars na tuliifunga Mamelodi magoli 2-1. Nina heshima kubwa na Nchi hii, nimeishi vizuri na watu wa hapa lakini kwa sasa nimerudi na Young Africans SC na tunataka kuwafurahisha watu wa Watanzania”
MSAFARA WA YANGA
Kuelekea mchezo huo ambao utapigwa Ijumaa, Yanga ilisafiri na msafara wa mastaa 26 ambao ni;
Makipa
Djigui Diarra
Aboutwalib Mshery
Metacha Mnata
Walinzi
Bakari Mwamnyeto
Ibrahim Bacca
Dickson Job
Yao Attohoula Kouasi
Nickson Kibabage
Joyce Lomalisa
Gift Fred
Kibwana Shomari
Viungo;
Khalid Aucho
Zawadi Mauya
Salum Abubakar
Jonas Mkude
Mudathir Yahya
Maxi Nzengeli
Viungo washambuliaji
Pacome Peodoh Zouzoua
Stephane Aziz Ki
Augustine Okrah
Mahlatse Skudu Makudubela
Farid Mussa
Denis Nkane
Washambuliaji
Clement Mzize
Joseph Guede
Kennedy Musonda
