- Mastaa watano wa Yanga hali zao bado hazijaimarika kutokana na kupata maumivu
- Masta Gamondi ashusha presha na kutoa maneno ya maana katika anga la kimataifa
- Kazi bado haijaisha Yanga wataja namna watakavyopeta kimataifa
NYOTA watano wa kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kuanza kwao kikosi cha kwanza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali Machi 30 dhidi ya Mamelodi Sundowns kunategemea na watakavyoimarika.
Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa ndani ya Ligi Kuu Bara imekuwa na mwendelezo mzuri kwa kupata matokeo kwenye mechi zake ilizocheza ikipoteza mechi mbili na inaongoza ligi msimu wa 2023/24.
Baada ya kucheza mechi 20 ndani ya ligi imepoteza mechi mbili ilikuwa dhidi ya Ihefu ugenini na mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulichezwa Uwanja wa Mkapa pia walikuwa ugenini.
Katika mchezo dhidi ya Azam FC wachezaji wa Yanga chaguo la kwanza la Gamondi walipata maumivu kwenye mchezo huo na hawakufanikiwa kukamilisha dakika 90 kwenye mchezo huo na sasa wanapambania hali zao kurejea kwenye ubora.
KIMATAIFA HAWA HAPA WAPINZANI WAO
Kazi kubwa kwa Yanga kwenye anga la kimataifa ni dhidi ya Mamelodi Sundowns mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.
Ipo wazi kwamba wapinzani wao sio wakubeza kutokana na kasi waliyonayo uwanjani huku ikiwa ni moja ya timu yenye inayofanya vizuri kwenye mechi za kimataifa.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa Machi 30 ikiwa ni robo fainali ya kwanza na mchezo wa pili ambao utaamua mshindi wa kutinga hatua ya nusu fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika utachezwa Afrika Kusini.
HAWA HAPA WACHEZAJI YANGA

Kiungo Pacome Zouzoua anasumbuliwa na maumivu ya goti alipata maumivu mchezo wa Mzizima Dabi uliochezwa Uwanja wa Mkapa Machi 17 ambapo alianza kikosi cha kwanza na alikwama kukamilisha dakika zote 90 katika mchezo huo.
Ipo wazi kwamba mwisho wa mchezo huo ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Azam FC 2-1 Yanga huku mwamba Pacome ambaye ameitwa kwenye timu ya taifa ya Ivory Coast nafasi yake ilichukuliwa na Joseph Guede ambaye ni mshambuliaji.
Mbali na Pacome nyota mwingine ni Khalid Aucho ambaye ni kiungo mkabaji bado hajawa fiti kwa muda na hakuwepo kwenye mchezo wa Mzizima Dabi yeye anasumbuliwa na goti.
Kiungo mzawa mzee wa mikato ya kimyakimya Zawadi Mauya naye hayupo fiti naye hakuwa sehemu ya mchezo huo uliokuwa na presha kubwa wakati bao la ushindi likifungwa na Feisal Salum aliyewahi kucheza Yanga.
Beki wa kupanda na kushuka Attohoula Yao mwenye pasi 7 ndani ya ligi aliumia kwenye nyama za paja ambapo maumivu hayo alipata kwenye mchezo dhidi ya Azam FC.
Kiraka mwingine ambaye kazini kwake kuna kazi ni Kibwana Shomari anasumbuliwa na enka yeye alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Geita Gold uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Kwenye mchezo huo Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na kiungo mshambuliaji Aziz KI akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya Geita Gold.
MAANDALIZI YANAENDELEA

Tayari wachezaji wa Yanga chini ya Gamondi wameanza maandalizi kuelekea mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao unatarajiwa kuwa na kasi kubwa Uwanja wa Mkapa.
Gamondi ameweka wazi kuwa wanatambua ushindani uliopo kwenye mechi kubwa hivyo kila kitu kitapangwa kwa umakini kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa shauku kubwa na wapenda michezo Afrika.
“Kila kitu kinahitaji maandalizi mazuri na wachezaji wanatambua kwamba kupata ushindi kwenye mchezo wa kwanza ni muhimu ili kuongeza nafasi ya kufikia malengo yetu.
“Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kila hatua inakuwa tofauti hivyo jambo la msingi ni kuwa makini kwa kufanya maandalizi mazuri na kuhakikisha kwamba nafasi ambazo zitapatiana uwanjani zinakuwa na faida kwa upande wetu hilo linawezekana,”.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amewekà wazi kuwa hakuna cha kuhofia mchezo wao ujao ambacho kinafanyika kwa sasa ni maandalizi na wanapaswa kushirikiana katika kila hali.
“Benchi la ufundi linasubiri ripoti kutoka kwa madaktari kujua hali zao zipoje kwa kuwa lakini hatupaswi kuwa na hofu jambo la msingi ni kuwa pamoja na mshikamano, daima mbele nyumamwiko.
“Mashabiki kwenye hili ni muhimu kuungana na kuendeleza umoja wetu, ni mchezo mkubwa na muhimu kwetu kupata matokeo mazuri,’.

