KIKOSI cha Simba rasmi kimewasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi fupi ya kujiandaa na mchezo wao wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.

KIVUMBI KUWAKA IJUMAA MACHI 29

Kuendana na droo ya Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika ambayo ilifanyika Machi 12, mwaka huu huko kwenye makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), nchini Misri.
Mchezo wa kwanza wa Simba ambao wamewahi kulamba dili la udhamini wa Kampuni SportPesa utapigwa Ijumaa ya Machi 29, mwaka huu dhidi ya Al Ahly mtanange utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa saa tatu usiku.
Mchezo wa marudiano utapigwa Aprili 5 jijini Cairo nchini Misri na mshindi wa jumla atasonga mbele na kutinga nusu fainali.
Ikumbukwe droo hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika imefanyika mara baada ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumalizika kwa rekodi ya aina yake, ambapo Tanzania imekuwa Taifa pekee ambalo limefanikiwa kutoa timu mbili ambazo zimefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali.
Wawakilishi hao wa Tanzania walifanikiwa kufuzu kutokea kundi B la mashindano hayo wakimaliza kwenye nafasi ya pili na pointi zao tisa ambazo wamekusanya katika michezo sita. Kutoka kwenye kundi lao ni wao na Asec Mimosas ya Ivory Coast ndio wamefuzu Robo Fainali.
ALICHOSEMA MENEJA WA SIMBA AHMED ALLY

Meneja Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally amesema kikosi kimeondoka kwa ajili ya kuweka kambi ya siku saba kujiandaa na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Machi 29.
Ahmed amesema kambi hiyo ya Zanzibar itahusisha wachezaji ambao hawakuitwa kwenye timu zao Taifa ambao ni wengi ili kumpa nafasi kocha kufanya maandalizi ya kutosha kutokana na ukubwa wa mechi.
“Kikosi chetu kimewasili Zanzibar kwa ajili ya kuweka kambi ya siku saba kujiandaa na mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa Machi 29.
“Kambi hii ya Zanzibar itahusisha wachezaji ambao hawakuitwa kwenye timu zao Taifa ambao ndio sehemu kubwa ya kikosi ili kumpa nafasi kocha kufanya maandalizi ya kutosha kutokana na ukubwa wa mechi,” Amesema Ahmed.
REKODI: ROBO FAINALI YA NNE KWA SIMBA
Hii ni Robo fainali ya nne ya Ligi ya Mabingwa katika kipindi cha miaka mitano tangu mwaka 2019. Ikumbukwe mwaka 2020 ndio mwaka pekee ambao haikutinga robo fainali ya michuano hii.
Haya hapa matokeo ya mechi tatu za hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zilizopita.
- Aprili 6, 2019
Simba 0 -0 Tp mazembe
Mechi ya marudiano Aprili 13, 2019
Tp mazembe 4 -1 Simba
- Mei 15, 2021
Kaizer Chiefs 4-0 Simba
Mechi ya marudiano Mei 22, 2021
Simba 3 -0 Kaizer Chiefs
- Aprili 22, 2023
Simba 1 -0 Wydad Casablanca
Mechi ya marudiano Aprili 28, 2023
Wydad 1-0 Simba
Penati 4-3
SIMBA WATANGAZA KUITAKA NUSU FAINALI
Uongozi wa timu hiyo umeweka wazi kuwa utaingia katika mchezo huo wakiwa na kiu kubwa ya kuvuka hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali ya michuano hii mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika.
Uongozi wa Simba pia umeweka wazi kuwa unafahamu Al Ahly ni timu yenye historia kubwa barani Afrika kwa kuchukua taji hili mara nyingi, huku wakiweka wazi kuwa safari hii watavuka.
BENCHIKHA AIPA JEURI SIMBA

Miongoni mwa sababu kubwa ambazo zinawapa jeuri ya kuamini zitawasaidia kufanikisha lengo lao ni uwepo wa Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha ambaye sio mgeni wa mechi kubwa na zenye presha kama hizi.
Msimu uliopita kocha huyo aliiwezesha USM Alger ya Algeria kuchukua taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga Yanga ya Tanzania.
Benchikha akiwa na USM Alger pia alichukua taji la Super Cup kwa kuifunga Al Ahly msimu huohuo uliopita.
CHAMA ATOA TAMKO ZITO
Kiungo mshambuliaji, Clatous Chama amesema itakuwa mechi ngumu na wanaiheshimu Al Ahly lakini hawawaogopi na wapo tayari kupambana nao.
Chama amesema katika miaka mitano waliyofika hatua hiyo wamejifunza mambo mengi na wanajua jinsi ya kukabiliana na miamba hiyo.
“Tunaiheshimu Al Ahly lakini hatuwaogopi, tumejifunza mambo mengi na tupo tayari kuwakabili, tunahitaji nasi kuvuka na kuingia nusu fainali,” amesema Chama.
