MIKATABA ya nyota wawili kwenye timu mbili tofauti imezua utata
Dau la Dube weka mbali na watoto, Bruno huru kujiunga na timu yoyote
Simba walipata nao tabu kila walipokutana nao kwenye mechi za ushindani
UTATA mtupu umeibuka kutokana na ishu ya mastaa wawili kutoka timu mbili tofauti kuamua kusitisha mikataba yao huku taarifa zikitolewa siku moja ambayo ni Machi 4 2024.
Wakati shangwe kubwa kwenye bara la Afrika ikiwa ni kwenye kutinga hatua ya robo fainali kwa timu mbili ambazo ni Simba na Yanga utata umeibuka ishu ya mikataba ya nyota wawili wa timu mbili tofauti Singida Fountain Gate Bruno Gomes na Prince Dube wa Azam FC.
Mshambuliaji Dube aliyewavuruga Simba akiwa na uzi wa Azam FC walipokutana kwenye mechi za ushindani anatajwa kuwa kwenye rada za timu zenye maskani yake Kariakoo kwa ajili ya kupata changamoto mpya kwa kuwa anatajwa hana furaha ndani ya Azam FC.
Ni Machi 2 2024 taarifa rasmi kutoka Azam FC kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano Azam FC, Zakaria Thabit, Zakazakazi zilieleza kuwa nyota huyo ameandika barua kuomba kuondoka huku wao wakiwa hawana tatizo kwa kumruhusu kuondoka.
UTATA MTUPU ISHU YA MKATABA
Wakati utata mtupu ukiibuka huku mkataba wa Dube ukiwa haujawekwa wazi mkataba inatajwa kwamba lazima atomize masharti yaliyopo kwenye mkataba mpya aliosaini alipoongeza mkataba mpya kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Inatajwa kwamba miongoni mwa masharti ya kuvunja mkataba wake ni pamoja na kulipa Dola za Kimarekani laki tatu (300,000) kwa mujibu wa mkataba ambazo ni zaidi ya milioni 700 kwa fedha za Tanzania.
BARUA YA KUVUNJA MKATABA MEZANI
Zakazakazi Mkuu wa Kitengo cha Habari ndani ya Azam FC ameweka wazi kuwa wamepokea barua hiyo na wanatambua kwamba Dube aliongeza mkataba kabla ya msimu kuanza ambao unatarajiwa kuisha 2026.
Jambo ambalo anapaswa kuchagua ni kulipa fedha hizo ambazo zinatakiwa ili kuvunja mkataba huo na chaguo la pili ni kubaki ndani ya Azam FC mpaka mkataba wake utakapoisha. Pia timu inayomuhitaji Dube inapaswa kuzungumza na uongozi lakini inapaswa kulipa fedha ili kuipata saini yake.

DUBE ANAKWENDA WAPI?
Tetesi zinaeleza kuwa Dube anatajwa kuwa kwenye rada za Yanga ambao ni vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 43 ndani ya ligi katupia mabao 7 inaelezwa anapenda kuwa kwenye timu yenye ushindani mkubwa kitaifa na kimataifa.
Ikiwa mpango huo utakuwa hivyo basi Yanga ambayo inadhamiwini na SportPesa ina kazi ya kufuata utaratibu wa kwenye mkataba na kuweka mkwanja mezani kupata saini ya mshambuliaji huyo.
SIMBA WALIPATA NAYE TABU
Miongoni mwa mabao aliyonayo ambayo ni saba kati ya hayo aliwafunga Simba kwenye Mzizima Dabi mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba na mwisho ubao ukasoma Simba 1-1 Azam FC.
Dube alipachika bao hilo dakika ya 14 akimtungua kipa Ayoub Lakred ambaye alianza langoni wakati Aishi Manula kipa namba moja wa Simba naye aliwahi kutunguliwa na Dube kwenye Mzizima Dabi.

Ikumbukwe kwamba Manula alitunguliwa na Dube ilikuwa ni Oktoba 27 2022 ubao wa Uwanja wa Mkapa uliposoma Simba 0-1 Azam FC mtindo ulikuwa ni uleule wa matengenezo ya mashambulizi ya ufungaji, mpira ulianzia kwa kipa kisha ukaguswa na wachezaji waziozidi watatu wa Azam FC Dube akafunga.
Ipo wazi kwamba Dube msimu wa 2023/24 bao lake la kwanza alifunga kwenye mchezo dhidi ya Tabora United kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ilikuwa dakika ya tano Agosti 16 2023.
BRUNO NAYE GUMZO HUKO
Wakati Dube akiwa kaandika barua ya kuomba kusepa ndani ya Azam FC mkali mwingine ndani ya Singida Fountain Gate naye amefikia makubaliano ya kusitisha mkataba wake na mabosi hao.
Bruno ni mkali wa kutumia mguu wa kulia katika mapigo huru Mbarzil Bruno Gomes ameweka wazi kuwa atawakumbuka sana wanafamilia ya Singida Fountain Gate kutokana na maisha ambayo alikuwa akiishi hapo.

Nyota huyo raia wa Brazil alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za Simba lakini mabosi wa Singida Fountain Gate wakabainisha kwamba bado yupo na mwamba hauzwi hivyo kwa sasa yupo huru.
SINGIDA FOUNTAIN GATE MWENDO WAKE
Mwendo wa Singida Fountain Gate kwenye mechi za ligi umekuwa tofauti ndani ya msimu wa 2023/24 ambapo timu ya Singiada Fountain Gate haijawa kwenye mwendo mzuri kwenye mechi za hivi karibuni ndani ya Ligi Kuu Bara.
Bara Machi 4 2024 taarifa zimeeleza kuwa wamefikia makubaliano ya kuvunja mkataba wake baada ya makubaliano ya pande zote mbili kufikiana makubaliano mazuri.
Bruno Gomes msimu wa 2022/23 alikuwa ni chaguo la kwanza kikosi cha kwanza na aliwahi kufunga kwa mapigo huru kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC kwa pigo huru.
Pia aliwahi kuwafunga Simba kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Mkapa kwa pigo huru akiwa nje kidogo ya 18 langoni alikuwa ni Aishi Manula.
