- Simba SC imepania kufanya usajili mkubwa ikiwa ni maandalizi kuelekea msimu wa 2025/26 wa Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC.
- Mo Rais wa Heshima wa Simba SC ametoa tamko zito kuhusu usajili, Fadlu Davids Kocha Mkuu wa Simba SC kwenye kazi kubwa.
- Feisal Salum wa Azam FC anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi hao wenye maskani yao Msimbazi.
Simba SC imepania kufanya usajili mkubwa kuelekea msimu wa 2025/26. Ikumbukwe kwamba timu hiyo msimu wa 2024/25 ilikosa mataji yote iliyokuwa inayapambania jambo ambalo linawafanya waje na hasira zaidi. Miongoni mwa wachezaji ambao wanatajwa kuwa katika rada za Simba SC ni Feisal Salum wa Azam FC na Balla Conte wa CS Sfaxien ya Tunisia.

Soma hii: Simba SC wamefungukia kuiwinda saini ya Feisal Salum kiungo wa Azam FC

Nafasi ya Simba SC kwenye ligi ya NBC 2024/25
Kwenye ligi ilimaliza ikiwa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 30. Katika dakika 2,700 uwanjani ushindi ulikuwa katika mechi 25, sare tatu na ilipoteza mechi mbili. Mechi zote mbili ambazo ni dakika 180 ilikuwa dhidi ya Yanga SC ambao ni mabingwa wa ligi inayodhaminiwa na NBC.
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 0-1 Yanga SC. Mzunguko wa pili ilikuwa Yanga SC 2-0 Simba SC. Ni mabao matatu Yanga SC walifunga mbele ya Simba SC iliyokosa kuvuna pointi kwenye Kariakoo Dabi.
Wachezaji walioachwa Simba SC

Soma hii: Aishi Manula amesaini mkataba kuitumikia Azam FC akitokea Simba SC i
Kuna orodha ya wachezaji walioachwa na Simba SC kuelekea msimu wa 2025/26. Aishi Manula ambaye ni kipa huyu atakuwa ndani ya Azam FC. Omary Omary huyu amepelekwa kwa mkopo Mashujaa FC. Fabrince Ngoma mkataba wake umeisha. Kelvin Kijili atakuwa ndani ya Singida Black Stars.
Orodha ni ndefu ndani ya Simba SC. Tetesi zinaeleza kuwa Awesu Awesu atapelekwa KMC FC kwa mkopo. Joshua Mutale huyu bado anajadiliwa aondolewe kwa mkopo ama abaki ndani ya Simba SC.
Semaji Ahmed Ally kuhusu usajili
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC ameweka wazi kuwa wanakuja na kishindo. Ahmed aliongeza kuwa safari hii hatasema sana kuhusu usajili. Alimtaja Fadlu Davids ambaye ni kocha wa Simba SC kuwa ataongoza jahazi kwenye usajili.
Ally amesema wanatambua kwamba ulikuwa ni msimu wenye ushindani hivyo Wanasimba wasiishiwe nguvu, mipango inapangwa na usajili unafanyika mkubwa kuelekea msimu mpya wa 2025/26.
“Kwa sasa viongozi wa Simba SC wametapakaa kila kona kwenye nchi za Afrika kwa ajili ya kumalizia usajili wa wachezaji wapya. Huu ni usajili mwingine wa kishindo na sitaongea sana safari hii nitaacha watu waone wenyewe.”.
Mataji waliyopishana nayo Simba SC
Taji la Ngao ya Jamii ni Yanga SC walitwaa, taji la CRDB Federation Cup, Yanga SC walitwaa taji la Ligi Kuu Bara inayodhaminiwa na NBC ni Yanga SC walitwaa huku lile la Kombe la Shirikisho Afrika ni RS Berkane ya Morocco walitwaa taji hilo.
Tamko la Mo Dewji kuhusu usajili

Soma hii: Mo Dewji aibua jambo Simba SC
Rais wa heshima wa Simba SC, Mohamed Dewji maarufu kwa Mo Dewji aliweka wazi kuwa wanafanya maboresho makubwa. Mo alivunja ukimya huo kwa mashabiki kutokana na kutoongea mara baada ya msimu wa 2024/25 kutamatika. Kuhusu usajili Mo alisema kuwa wamejipanga ili kupata wachezaji wazuri na imara.
“Wanasimba niwaambie kwamba tupo pamoja na kwenye nyakati hizi ngumu lazima tuungane. Tumemaliza msimu uliokuwa na ushindani mkubwa licha ya changamoto nyingi. Tunashukuru tukiwa na kocha mpya Fadlu Davids kuna hatua tumepiga.
“Kuelekea msimu mpya tutakuwa imara zaidi. Ikumbukwe kwamba bado tunajenga timu. Tutashirikiana na tutakuwa na timu imara ambayo haitashikika msimu mpya,” alisema Mo.
Sakata la Kibu Dennis na Mohamed Hussen
Wachezaji wawili, Kibu Dennis na Mohamed Hussen Zimbwe Jr hawa wanatajwa kuondoka. Kibu mkandaji inaelezwa kuwa anataka kucheza nje ya Afrika na sasa yupo nchini Marekani. Mohamed Hussen ambaye ni nahodha inaelezwa yupo kwenye rada za Yanga SC.

Kibu bado ana mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Simba SC. Zimbwe Jr mkataba wake umeisha ndani ya Simba SC na hajaongeza mkataba mwingine. Sakata hilo limezua gumzo kila kona kwa mashabiki wa Simba SC.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC aligusia hayo. Kuhusu Kibu alisema bado ni mchezaji wa Simba SC na yupo Marekani. Suala la Zimbwe alikiri mkataba wake umeisha.
“Kibu Dennis huyu ana mkataba wa mwaka mmoja na Simba SC hivyo hakuna mashaka. Tunajua yupo Marekani na familia yake. Zimbwe Jr mkataba wake umeisha.Hivyo viongozi wanafanya mazungumzo kuona namna gani ataongeza mkataba.”
Maeneo yatakayofanyiwa usajili Simba SC
Maeneo ambayo Simba SC itafanya usajili inatajwa ni eneo la safu ya ulinzi. Kuondoka kwa Hussen Kazi, Kelvin Kijili kunaongeza uhitaji eneo hilo. Kwenye eneo la ushambuliaji na kiungo mshambuliaji. Leonel Ateba ambaye ni mshambuliaji anatajwa ataondoka hivyo mbadala wake anatafutwa.
Hitimisho
Simba SC inatarajia kuweka kambi nchini Misri kwa maadalizi ya msimu mpya wa 2025/26. Kabla ya kuondoka itatangaza wachezaji wake wapya. Fadlu Davids na Seleman Matola watakuwa na kazi kusuka kikosi upya cha ushindani.


