- Simba SC 1-0 Kagera Sugar ni mchezo wa mwisho 2024/25 ndani ya ligi wakiwa nyumbani kwenye msako wa pointi tatu muhimu.
- Steven Mukwala apeleka kilio kwa Kagera Sugar dakika ya 17 ya mchezo akitumia pasi ya David Kameta.Mzunguko wa kwanza Kagera Sugar 2-5 Simba SC.
- Jean Ahoua akamwa kukamilisha dakika 90, ashikilia chati ya kinara ufungaji kwenye ligi akiwa na mabao 16 na pasi 9.
Simba SC 1-0 Kagera Sugar ni mchezo wa mwisho 2024/25 ndani ya ligi. Mchezo huo wa raundi ya pili ulichezwa Uwanja wa KMC Complex ikiwa ni funga kazi kwa Kagera Sugar ambayo imeshuka daraja. Simba SC inafikisha pointi 78 ikiwa nafasi ya pili na vinara ni Yanga SC wenye pointi 79 nafasi ya kwanza.

Soma hii: Yanga SC vs Simba SC vita ya ubingwa bado inaendelea
Rekodi zinaonyesha kuwa ni mchezo wa 30 wababe hawa wanakutana. Simba SC imeshinda mechi 16, sare ni 7 huku Kagera Sugar ikipata ushindi kwenye mechi 7 ndani ya uwanja katika msako wa pointi tatu. Kagera Sugar amepoteza pointi sita mbele ya Simba SC kwa kuwa mzunguko wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-5.
Mchezo wa mwisho kwa Simba SC
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba SC amesema kuwa mchezo wao dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa KMC Complex, Juni 22 2025 ni wa mwisho kwa msimu wa 2024/25 wakiwa nyumbani.

Soma hii: Tuzo ya ufungaji bora vita yake inazidi kuchangamka
Simba SC ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar mtupiaji akiwa ni Steven Mukwala ambaye alitumia pasi ya David Kameta dakika ya 17. Bao hilo lilidumu mpaka dakika ya 90 na Simba SC kuvuna pointi tatu wakifikisha pointi 78.
Ahmed amesema: “Mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar ni mchezo wa mwisho wa msimu 2024/25 tukiwa nyumbani.Hatuna mchezo mwingine wowote uliopo mbele yetu ambao tutakuwa nyumbani hata kama tutakuwa na michezo 10. Hivyo huu ni mchezo wa mwisho kwetu.”
Mukwala aimaliza Kagera Sugar kipindi cha kwanza
Mshambuliaji wa Simba SC inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, Steven Mukwala amefikisha jumla ya mabao 13 ndani ya ligi. Kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar Juni 22 alipachika bao moja. Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 1-0 Kagera Sugar. Bao hilo alipachika dakika ya 17 akiwa ndani ya 18. Mukwala alituma pasi ya David Kameta ambaye alipokea pasi elekezi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Jean Ahoua.
Kameta kwenye mchezo wa funga kazi Uwanja wa KMC Complex alikomba dakika 90. Alishuhudia beki mwingine anayecheza upande wake Shomari Kapombe naye akiingia kwenye mchezo huo. Kapombe alipoingia Duchu alikuwa mchezaji huru akicheza kila eneo na alikuwa akipewa maelekezo mara nyingi na Kapombe.

Mukwala anafikisha mabao 13 kwenye ligi akiwa saw ana Leonel Ateba wa Simba SC huku akiwa saw ana Clement Mzize na Prince Dube wa Yanga SC na Jonathan Sowah wa Singida Black Stars ambaye alifunga kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons. Kinara kwenye chati ya ufungaji wa mabao ndani ya ligi ni Jean Ahoua wa Simba SC ambaye amefunga jumla ya mabao 16. Kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar hakukomba dakika 90 wala hakufunga.
Kikosi cha Simba SC vs Kagera Sugar
Kwenye mchezo wa Simba SC vs Kagera Juni 22 2025 kulikuwa na mabadiliko makubwa kwa wachezaji walioanza kikosi cha kwanza. Ni kipa Moussa Camara alianza ikiwa ni mchezo wake wa 27 kukaa langoni. Camara ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Soma hii: Ufungaji bora Kariakoo Dabi kesi kumalizwa 2024/25
Wachezaji wengine ambao walikuwa wakianza mara kwa mara kikosi cha kwanza walianzia benchi. Miongoni mwa wachezaji ambao walianzia benchi ni Mohamed Hussen Zimbwe Jr, Shomari Kapombe, Kibu Dennis na Leonel Ateba.
Kikosi cha Simba SC kilichoanza Juni 22 2025 kilikuwa namna hii: Camara, Duchu, Nouma, Che Malone, Chamou, Ngoma Fabrince, Ladack Chasambi, Mavambo, Steven Mukwala, Jean Ahoua, Awesu Awesu. Akiba ni Ally Salim, Kapombe, Zimbwe, Okejepha, Joshua Mutale, Ateba, Kibu, Ellie Mpanzu, Valentino Mashaka na Bashir.
Hizi hapa dakika za wachezaji wa Simba SC vs Kagera Sugar
Mousa Camara dakika 90, David Kameta dakika 90, Nouma dakika 90, Che Malone dakika 90, Chamou dakika 82, Zimbwe Jr dakika 8, Fabrince Ngoma dakika 58, Kibu Dennis dakika 32, Ladack Chasambi dakika 77, Shomari Kapombe dakika 13, Mavambo dakika 90, Steven Mukwala dakika 58, Okejapha dakika 32, Jean Ahoua dakika 58, Joshua Mutale dakika 32, Awesu dakika 90.
Kagera Sugar safari imegota mwisho
Kagera Sugar inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Kaseja imegota mwisho ndani ya ligi 2024/25. Timu hiyo imemaliza msimu ikiwa nafasi ya 15 ikiwa na pointi 23 baada yakucheza mechi 30. Ushindi ni kwenye mechi 5, sare 8 ikipoteza mechi 17. Safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 22.
Mbali na Kagera Sugar timu nyingine ambayo imeshuka daraja ni KenGold. Ni pointi 16 inazo kibindoni baada yakucheza mechi 30. Safu ya ushambuliaji imetupia mabao 22. Safu ya ulinzi ni mabao 62 imefungwa ikiwa nit imu namba moja kufungwa mabao mengi ndani ya ligi.

