- Ufungaji bora Kariakoo Dabi kesi kumalizwa 2024/25, Jean Ahoua, Clement Mzize kwenye kasi kubwa katika kucheka na nyavu.
- Feisal Salum ngoma imekuwa nzito anakimbiza katika eneo la kutengeneza nafasi za mabao kwenye ligi namba nne kwa ubora Afrika.
- Pacome kiungo mshambuliaji wa Yanga SC amehusika kwenye mabao 20 kati ya 76 yaliyofungwa na timu hiyo inayoongoza ligi ikiwa na pointi 76.
Ufungaji bora Kariakoo Dabi kesi kumalizwa 2024/25.Mchezo wa funga kazi utatoa majibu kamili kwa kuwa kwa sasa kila mchezaji ana nafasi kutwaa tuzo hiyo. Jonathan Sowah wa Singida Black Stars katupia mabao 12, mchezo dhidi ya Tanzania Prisons utakuwa ni wa raundi ya 30 ana nafasi kuendeleza kasi yake. Wachezaji wa Simba SC na Yanga SC wamekuwa wakivutana jezi kwenye eneo hilo kwa sasa.

Soma hii: Tuzo ya ufungaji bora vita yake inazidi kuchangamka
Hapa tunakuletea orodha ya waliohusika kwenye mabao mengi ikiwa ni vita kwenye msako wa mchezaji atakeyetwaa tuzo ya kiatu cha ufungaji bora ambayo msimu wa 2023/24 ilikwenda Yanga SC kwa kiungo Aziz Ki aliyekamilisha msimu akiwa na mabao 21. Mchezo wa watani wa jadi Juni 25 2025 utatoa picha kamili ya nani atakuwa nani. Hii hapa orodha ya wakali kwenye kuhusika na mabao mengi ipo hivi:-
Jean Ahoua, Simba SC-25

Kinara wa kucheka na nyavu ndani ya ligi ni kiungo mshambuliaji wa Simba SC Jean Ahoua. Nyota huyo kaufunga jumla ya mabao 16 ndani ya msimu wa 2024/25. Bao la 16 alifunga kwenye mchezo dhidi ya KenGold dakika ya 75 kwa mguu wa kulia akitumia pasi ya Leonel Ateba.
Jean Ahoua wa Simba katengeneza jumla ya pasi 9 za mabao na kafunga mabao 16. Kahusika kwenye mabao 25 kati ya 68 yaliyofungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 75 baada ya mechi 28 ambazo ni dakika 2,520. Simba SC ni namba mbili kwa timu ambazo zimefunga mabao mengi ndani ya ligi. Ahoua ujanja wake ni kwenye mguu wa kulia akiwa kafunga mabao mengi kwa kutumia mguu huo ambayo ni mabao 15.
Prince Dube, Yanga SC-21

Prince Dube wa Yanga SC katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao katika kikosi hicho akiwa katupia mabao 13. Amehusika kwenye mabao 21 kati ya 76 yaliyofungwa na Yanga SC ndani ya ligi. Alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons dakika ya 22 nafasi yake ilichukuliwa na kiungo mshambuliaji Clatous Chama ambaye yeye kafunga mabao matano na pasi tatu za mabao ndani ya ligi.
Pacome Zouzoua wa Yanga SC-20
Pacome ni mkali kwenye kufunga na kutengeneza pasi za mabao akiwa uwanjani. Ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Miloud Hamdi na mguu wake wenye nguvu ni ule wa kulia. Huenda akaanza kikosi cha kwanza kwenye mchezo ujao wa Yanga SC vs Dodoma Jiji, Juni 22 2025.

Pacome kibindoni katupia jumla ya mabao 11, ametengeneza pasi za mabao 9 hivyo kahusika kwenye mabao 20 kati ya 76 yaliyofungwa na timu hiyo inayoongoza ligi kwa msimu wa 2024/25.Kwenye mchezo dhidi ya Tanzania Prisons wa raundi ya 29 alifunga mabao mawili na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
Feisal Salum wa Azam FC-17
Ni mkali kwenye kutengeneza pasi za mabao ndani ya ligi namba nne kwa ubora. Huyu ni mzawa namba moja kwenye eneo hilo. Mguu wake wenye nguvu ni ule wa kulia akiwa kwenye majukumu yake ndani ya uwanja. Feisal katengeneza jumla ya pasi 13 za mabao na pasi yake ya kwanza alitoa kwenye mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ilikuwa dakika ya 19. Idd Nado ni mfungaji wa bao la kwanza ndani ya kikosi cha Azam FC kwenye ligi msimu wa 2024/25.

Weka mbali kutengeneza pasi za mwisho, Feisal anajua kufunga na mguu wake wenye nguvu ni ule wa kulia akiwa kafunga jumla ya mabao manne ndani ya ligi. Kahusika kwenye mabao 17 ndani ya Azam FC iliyo nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi 60 ikiwa imefunga mabao 53.
Clement Mzize wa Yanga SC-17
Mshambuliaji namba moja kwa wazawa ni Clement Mzize akiwa kafunga jumla ya mabao 13. Mzize ambaye ni chaguo la kwanza la Miloud kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate alichaguliwa kuwa mchezaji bora. Yanga SC ikiwa imefunga mabao 76, kafunga mabao 13 na kutoa pasi nne za mabao ambazo zinamfanya ahusike kwenye jumla ya mabao 17 kutoka kwa timu hiyo ambayo inaongoza ligi.
Leonel Ateba wa Simba SC-17
Mshambuliaji wa Simba SC, Leonel Ateba kafunga mabao 13 na kutengeneza pasi nne. Kwenye mchezo dhidi ya KenGold alifunga bao lake la 13 na alitoa pasi moja inayomuongezea namba mpaka kuwa na pasi nne za mabao msimu wake wa kwanza akiwa na uzi wa Simba SC.
Aziz Ki wa Yanga SC-16
Kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Aziz Ki kwa msimu wa 2024/25 kabla yakupata changamoto mpya ndani ya Wydad alikuwa amehusika kwenye mabao 16 ndani ya Yanga SC iliyofunga jumla ya mabao 76 msimu wa 2024/25. Msimu wa 2023/24 Ki alikuwa mfungaji bora alipofunga jumla ya mabao 21 na pasi 8 ambazo zilimfanya ahusike kwenye mabao 29.

