Ateba v AuchoAteba v Aucho
  • Yanga SC vs Simba SC Juni 15 2025 hawa wachezaji wakuchungwa ndani ya uwanja kutokana na hatari waliyonayo kwenye kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.
  • Prince Dube anawatambua vizuri Simba SC ni mkali kwenye eneo lakufunga ndani ya uwanja akiwa na hat trick yake aliyowafunga Mashujaa Uwanja wa KMC Complex.
  • Ellie Mpanzu wa Simba SC ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Yanga SC vs Simba SC Juni 15 2025 hawa wachezaji wakuchungwa kutokana na kuwa na hatari wawapo uwanjani katika kutimiza majukumu yao. Mchezo wa jasho kwa wababe wawili uwanjani kwenye msako wa pointi tatu kutokana na kila timu kupambania ubingwa.

Bacca na Ateba
Bacca na Ateba mzunguko wa kwanza walikuwa kwenye mpambano mzito. Source: Yanga SC.

Soma hii:Yanga SC vs Simba SC iliyopangwa Juni 15 2025: Ngoma imekuwa ngumu, Yanga yatishia maamuzi magumu

Yanga SC kwenye msimamo ni nafasi ya kwanza pointi 73 baada ya kucheza mechi 27 ndani ya msimu wa 2024/25. Tofauti yao ni pointi moja dhidi ya watani wa jadi Simba SC ambao wana pointi 72 wote wakiwa wamecheza mechi 27. Mzunguko wa kwanza ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba SC 0-1 Yanga SC huku Leonel Ateba wa Simba SC beto yake na Ibrahim Bacca ikiwa ni gumzo.

Kwenye upande wa mabao safu ya ushambuliaji ya Yanga SC imefunga mabao 71 na ile ya Simba SC ni mabao 63 hivyo mchezo wa Kariakoo Dabi umeshikilia maamuzi ya kupata bingwa wa msimu wa 2024/25. Ukiweka kando hayo hapa tunakuletea baadhi ya wachezaji ambao wanapaswa kuchungwa kuelekea mchezo huo ambao shujaa huwa hatabiriki kutokana na uwezo wao ndani ya uwanja katika kutimiza majukumu yao, hapa tunakuletea namna hii:-

Prince Dube wa Yanga SC

Dube
Prince Dube mshambuliaji wa Yanga SC. Source: Yanga SC.

Soma hii: Simba SC yawatoa mashaka mashabiki yabainisha Kariakoo Dabi itachezwa Juni 15 2025

Prince Dube wa Yanga sio wakubeza kwa kuwa ni mtambo wa mabao ndani ya kikosi hicho akiwa anajua kufunga na kutengeneza pasi za mabao kwenye mechi za ligi ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika. Anawatambua vizuri Simba SC kwa kuwa hata alipokuwa ndani ya Azam FC alikuwa akiwafunga.

 Ametoa jumla ya pasi 8 za mabao katika kikosi hicho akiwa katupia mabao 13. Amehusika kwenye mabao 21 kati ya 71 yaliyofungwa na Yanga SC ndani ya ligi. Ipo wazi kwamba Dube ni nyota wa kwanza kufunga hat trick msimu wa 2024/25 ilikuwa dhidi ya Mashujaa kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC, Complex. Kwenye mchezo huo Dube alichaguliwa kuwa mchezaji bora.

Pacome Zouzoua wa Yanga SC

Kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Pacome Zouzoua ni mchezaji wakuchungwa kutokana na uwezo alionao kwenye mashuti yake ya nje ya 18 na kuelekea kwenye Kariakoo Dabi ana hatari kubwa akiwa uwanjani.

Pacome kibindoni ana mabao 9 na kutoa pasi 9 za mabao hivyo kahusika kwenye mabao 18 kati ya 71 yaliyofungwa na timu hiyo inayoongoza ligi kwa msimu wa 2024/25. Pacome ni miongoni mwa wachezaji wakuchungwa kwa kuwa anaweza kubadilisha usomaji wa matokeo ndani ya uwanja.

Clement Mzize wa Yanga SC

Mshambuliaji namba moja kwa wazawa ni Clement Mzize akiwa kafunga jumla ya mabao 13. Mzize ambaye ni chaguo la kwanza la Miloud kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate alichaguliwa kuwa mchezaji bora.

Yanga SC ikiwa imefunga mabao 71, kafunga mabao 13 na kutoa pasi tatu za mabao ambazo zinamfanya ahusike kwenye jumla ya mabao 16. Ni miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa na mchango mkubwa ndani ya Yanga SC kwenye mechi za ushindani.

Huyu hapa atakosekana kwa Yanga SC

Aziz Wydad
Aziz kiungo wa zamani wa Yanga SC. Source: Wydad.

Soma hii: Stephane Aziz Ki huyoo Marekani kuwavaa Manchester City ya Guardiola

Kiungo Aziz Ki kwa msimu wa 2024/25 kabla yakupata changamoto mpya Wydad Casablanca alikuwa amehusika kwenye mabao 16 ndani ya kikosi hicho ambacho kimefunga jumla ya mabao 71 kwenye ligi namba nne kwa ubora.

Hatakuwa sehemu ya mchezo kwa kuwa amepata dili jipya hivyo atakuwa mtazamaji wa Kariakoo Dabi kwa msimu wa 2024/25 kwenye mzunguko wa pili. Kiungo huyo mguu wake wenye nguvu ni ule wa kushoto.

Steven Mukwala wa Simba

Mshambuliaji wa Simba SC, Steven Mukwala ni miongoni mwa nyota wanaopaswa kuchungwa kwa kuwa amejenga urafiki na nyavu kwenye mechi za hivi karibuni ndani ya ligi. Mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Singida Black Stars, Mukwala alifunga bao pekee la ushindi kwa timu yake.

Mukwala na Ahoua
Mukwala na Ahoua nyota wa Simba SC. Source: Simba SC.

Soma hii: https://blog.sportpesa.co.tz/2025/06/12/hatuchezi-ya-yanga-sc-imehamia-simba-sc-kuelekea-juni-15/

Nyota huyo mbali na kufunga anajua kutengeneza pasi za mabao. Ni pasi tatu za mabao katengeneza akiwa amefunga jumla ya mabao 12 hivyo kahusika kwenye mabao 15 ya Simba SC iliyofunga mabao 63 msimu wa 2024/25.

Jean Ahoua wa Simba SC

Jean Ahoua wa Simba ni kinara kwa utupiaji wa mabao kwenye ligi na anajua kutoa pasi za mabao. Katengeneza jumla ya pasi 8 za mabao na kafunga mabao 13. Kahusika kwenye mabao 23 kati ya 63 yaliyofungwa na timu hiyo iliyo nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Ahoua kafunga mabao 14 akitumia mguu wa kulia na kafunga bao moja kwa pigo la kichwa ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Pamba Jiji alipotumia pasi ya Ellie Mpanzu ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Ellie Mpanzu wa Simba SC

Winga Ellie Mpanzu ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids amekuwa kwenye ubora wake katika mechi za ushindani. Amekuwa na uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mabao ni miongoni mwa wachezaji ambao wanapaswa kuchungwa katika mchezo wa Kariakoo Dabi. Amefunga mabao matatu na kutoa pasi tatu za mabao.

Kariakoo Dabi mvutano wakutosha

Licha ya mchezo huo kuwa na mvutano mkubwa bado Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) haijatoa taarifa mpya. Ikumbukwe kwamba awali mchezo huu ulitarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 ukaahirishwa na TPLB, Yanga SC wao walifika uwanjani na kubainisha kuwa hawatakuwa tayari kucheza mchezo mwingine namba 184 kwa kuwa kazi yao imekamilika.

Juni 9 2025 Yanga SC walibainisha kuwa hawatakuwa tayari kucheza mchezo wa Juni 15 2025 mpaka matakwa yao manne yatakapotimia ilikuwa kupitia kwa Ofisa Habari wa Yanga SC Ali Kamwe. Meneja wa Idara ya Habari Simba SC alibainisha kuwa mchezo upo palepale.

Share this: