Ateba na DiarraAteba na Diarra
  • Kariakoo Dabi mchezo wa watani wa jadi Yanga vs Simba SC mechi ipo palepale Juni 15 2025, Uwanja wa Mkapa.
  • Yanga SC washikilia msimamo wao wagomea kuyumbishwa kwa namna yoyote ile kuhusu Kariakoo Dabi.
  • Simba SC waulizia ripoti ya kuyeyuka kwa Kariakoo Dabi Machi 8 2025, Uwanja wa Mkapa.

Kariakoo Dabi mchezo wa watani wa jadi Yanga SC vs Simba SC mechi ipo palepale kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Simba SC mapema Juni 10 2025 kwa umma kuhusu mchezo huo wa mzunguko wa pili ambao umekuwa na mvutano mkubwa kwa pande zote mbili.

Yanga Vs Simba - Uwanja wa Mkapa
Khalid Aucho vs Mzamiru Yassin kwenye moja ya mchezo wa Kariakoo Dabi. Source: Yanga SC.

Soma hii: Yanga SC vs Simba SC iliyopangwa Juni 15 2025: Ngoma imekuwa ngumu, Yanga yatishia maamuzi magumu

Ikumbukwe kwamba mchezo huo awali ulitarajiwa kuchezwa Machi 8 2025 lakini uliahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB). Taarifa iliyotolewa na TPLB ilibainisha kuwa mchezo huo utapangiwa tarehe nyingine haraka iwezekenavyo.

image

Yanga SC ambao ni wenyeji wa mchezo huo Juni 9 2025 waliweka wazi kuwa hawacheza mchezo huo mpaka matakwa yao manne ambayo wameyaelekeza kuelekea kwa TPLB yatimizwe na ikiwa hayatatimizwa hawatacheza.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa, wababe hawa wawili walipocheza ubao ulisoma Simba SC 0-1 Yanga SC. Pointi tatu zilikuwa ni mali ya Yanga SC iliyopata ushindi kwenye mchezo huo.

Uwanja wa Mkapa
Uwanja wa Mkapa ambao ulitumika kwa mchezo wa Kariakoo Dabi mzunguko wa kwanza. Source: Simba SC.

Soma hii pia: Yanga SC wametoa matakwa manne yakitimizwa Kariakoo Dabi kuchezwa

Taarifa kutoka Simba SC kuhusu Kariakoo Dabi

Uongozi wa Simba SC umetoa taarifa kwa umma kuwa mchezo wao wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga SC unaotarajiwa kuchezwa Juni 15 2025 upo kama ulivyopangwa. Taarifa ambayo imetolewa mapema Juni 10 2025 na Simba SC imeeleza kuwa Klabu ya Simba inatoa taarifa kwa Wanachama, wapenzi na umma kuwa mchezo nambari 184 dhidi ya Yanga SC uliopangwa kufanyika Juni 15 2025 upo kama ulivyopangwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa inawasihi mashabiki wasihadaike na kelele za mtaani wale ambao walinunua tiketi za mechi ya Machi 8 2025 wazitunze kwa ajili ya matumizivya mchezo huo na we ambao hawajanunua tiketi wajiandae kununua baada ya tangazo la Bodi ya ligi.

Simba SC ambao watakuwa wageni katika mchezo huo wamekuja na sera inayosema kuwa : “Twendeni tukaujaze Uwanja wa Mkapa. Taarifa hiyo imeongeza kuwa inafahamika wazi kuwa Ligi Kuu ya NBC inajumuisha timu 16 na si ligi ya timu moja. Kwa mujibu wa taratibu kabla ya kuanza msimu vilabu vyote 16 hushiriki vikao na kutoa mapendekezo ya kuboresha kanuni na taratibu ili kuimarisha ligi hivyo wenye hoja wafuate taratibu husika.

Simba SC wameiomba Bodi ya Ligi na TFF watoe hadharani ripoti ya uchunguzi juu ya wale wote waliohusika kuharibu mechi ya ligi jioni ya Machi 7 2025 na wachukuliwe hatua stahiki na mamlaka husika.
Wamemaliza kwa kuandika kwamba kutotolewa kwa ripoti na kutochukuliwa hatua kwa wanaoendelea kuchochea ghasia ni sawa ba kulinda uharamia katika mpira ambao unatia dosari mafanikio yaliyopo katika tasnia ya mpira wa miguu nchini kwa sasa.

Simba Dabi
Taarifa ya Simba SC kuhusu Kariakoo Dabi. Source: Simba SC.

Soma hii: Sakata la kuyeyuka Kariakoo Dabi Machi 8 2025, sababu zipo hivi – SportPesa Tanzania

Msimamo wa ligi ulivyo kwa sasa

Yanga SC ni vinara kwenye msimamo wa ligi msimu wa 2024/25 baada ya kucheza mechi 27. Pointi zao kibindoni ni 73 wakitofautiana pointi moja na watani zao wa jadi ambao ni Simba SC. Kwenye chati ya utupiaji namba moja ni Prince Dube na Clement Mzize ambao wote wametupia mabao 13 ndani ya Yanga SC.

Simba SC ni namba mbili kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 27 wakiwa na pointi 72 baada ya kucheza jumla ya mechi 27. Ni mechi tatu wababe hawa wamebakiza kukamilisha mzunguko wa pili msimu wa 2024/25. Kinara wa utupiaji ndani ya Simba SC ni Jean Ahoua mwenye mabao 15.

Yanga SC ambao ni mabingwa watetezi wa ligi wamebainisha kuwa hawapo tayari kucheza mchezo namba 184 wa ligi ikiwa matakwa yao manne hayatafanyiwa kazi. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Juni 15 2025, Uwanja wa Mkapa.

Simba SC chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza walikwama kuvuna pointi tatu mbele ya Yanga SC ambayo kwa sasa inanolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi. Mchezo wa mzunguko wa pili unasubiriwa kwa shauku kubwa.

Hakuna viingilio wala taarifa kuhusu mchezo huo

Yanga SC ambao ni wenyeji kwenye mchezo huo mpaka sasa hawajatoa taarifa yoyote kuhusu maandalizi ya mchezo.Maandalizi hayo ni uwanja utakaotumika, viingilio vya mchezo husika kwa mashabiki watakaojitokeza uwanjani.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga SC aliweka wazi kuwa wanachokisema wanakimaanisha na ikiwa hawatapatiwa majibu ya uhakika hata mechi mbili ambazo wanazitambua kwenye ratiba yao hawatacheza na msimu ujao wa 2025/26 hawatashiriki ligi.

Mechi ambazo Yanga SC wanazitambua kwenye ratiba zao ukiweka kando mchezo wa Kariakoo Dabi ni dhidi ya Tanzania Prisons Juni 18 2025, Juni 22 2025 dhidi ya Dodoma Jiji na mchezo wa fainali ya CRDB Federation Cup dhidi ya Singida Black Stars ambao unatarajiwa kuchezwa Juni 28 2025.

Share this: