Simba SC vs Singida Black StarsSimba SC vs Singida Black Stars
  • Simba SC ikishinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars kukutana na mtani wa jadi Yanga SC katika hatua ya fainali CRDB Federation Cup.
  • Singida Black Stars kwenye kibarua cha kutibua rekodi mbele ya Simba SC kwenye mchezo wa nusu fainali.
  • Jean Ahoua kiungo mshambuliaji wa Simba SC anaingia kwenye orodha ya viungo walioivuruga Singida Black Stars, nje ndani.

Simba SC vs Singida Black Stars Mei 31 2025 nusu fainali CRDB Federation Cup, Uwanja wa Tanzanite Kwaraa na mshindi atakutana na Yanga SC ambaye tayari yupo pale kwenye mstari wa fainali.

Kapombe vs Singida Black Stars
Kapombe vs Singida Black Stars. Source: Simba SC.

Ikiwa ushindi utakuwa kwa Simba SC watakutana na mtani wake wa jadi, Yanga SC itakuwa ni Kariakoo Dabi katika mchezo wa fainali.

Kete zikiwa kwa Singida Black Stars, wababe hawa wawili, Yanga SC vs Singida Black Stars watakutana kwenye mchezo wa fainali itakayoamua nani atakuwa bingwa.

Wababe hawa wawili, Simba SC na Singida Black Stars wametoka kukamilisha dakika 180 za ligi na huu ni mchezo wao wa nusu fainali.

Rekodi za Simba SC vs Singida Black Stars CRDB Federation Cup

Rekodi zinaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara 9 katika michuano yote na Singida Black Stars haijawahi kupata ushindi zaidi ya kutoa sare mara moja huku ikifungwa michezo 8.

Singida Black Stars ni miongoni mwa timu ambazo ni imara ndani ya uwanja kutokana na ushindani wake mkubwa kwa msimu wa 2024/25.

Katika mechi ambazo wamekutana kwa msimu wa 2024/25 na Simba SC ushindani ulikuwa ni mkubwa na bao lilikuwa linapatikana moja pekee.

Kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa Liti, baada ya dakika 90 ubao ulisoma Singida Black Stars 0-1 Simba SC.

Pointi tatu zilikuwa mali ya Simba SC ugenini. Bao la ushindi kwenye mchezo lilifungwa na Fabrince Ngoma kwa pigo la kichwa.

Ngoma alitumia pasi ya kiungo mshambuliaji Jean Ahoua ambaye kwenye mchezo huo alipiga kona iliyokutana na kichwa cha Ngoma akamfunga Metacha Mnata.

Mchezo wa mzunguko wa pili ilikuwa ni Mei 28 2025, ubao wa Uwanja wa KMC Complex ulisoma Simba SC 1-0 Singida Black Stars.

Mukwala Vs Singida BS
Mukwala Vs Singida BS. Source: Simba SC.

Katika mchezo huo bao la ushindi lilifungwa na mshambuliaji Steven Mukwala. Pointi tatu zikawa mali ya Simba SC kwa mara nyingine tena.

Soma hii:Simba SC 1-0 Singida Black Stars 28 Mei 2025: Matokeo, magoli, Kifuatacho Kariakoo Dabi

Mwiba kwa Singida Black Stars

Kwa msimu wa 2024/25 kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Jean Ahoua amekuwa mwiba kwa Singida Black Stars kutokana na kuhusika kwenye mabao yote waliyofungwa.

Ahoua J C
Ahoua Jean kiungo mshambuliaji wa Simba SC. Source: Simba SC.

Ahoua alikuwa ni mtengeneza pasi za mwisho zilizoleta bao kwenye mechi ambazo walikutana ndani ya uwanja kwenye msako wa pointi tatu.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza alitoa pasi ya bao kwa Ngoma. Mwisho pointi tatu zikarejea Dar mitaa ya Msimbazi.

Kwenye mchezo wa mzunguko wa pili, Simba SC ilivuna pointi tatu kwa bao la Mukwala ambaye ni mshambuliaji. Nyota huyo naye alitumia pasi ya Ahoua kuimaliza Singida Black Stars.

Jumla Ahoua kwenye ligi katoa pasi 8 na kwa upande wa mabao amefunga jumla ya mabao 15 msimu wa 2024/25.

Wakali kutoka Singida Black Stars

Singida Black Stars kwenye eneo la ushambuliaji wanaye Jonathan Sowah ambaye huyu ni kinara katika eneo la kucheka na nyavu.

Sowah kafunga mabao 11 akiwa ni ingizo jipya ndani ya kikosi hicho kwenye dirisha dogo. Ni miongoni mwa wahambuliaji ambaye wanapenda kufunga wanapopata nafasi.

Ikumbukwe kwamba mchezaji huyo anaingia kwenye orodha ya wachezaji waliomfunga kipa namba moja wa Yanga SC, Djigui Diarra kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex.

Kelvin Nashon wa Singida Black Stars

Nashon
Nashon kiungo wa Singida Black Stars. Source: Singida Black Stars.

Kiungo mzawa Kelvin Nashon ni miongoni mwa wakabaji ambao wamekuwa na kazi kubwa wanapokutana na Simba SC.

Nashon ni aina ya wakabaji wanaokaba bila kuchoka jambo ambalo humfanya mara nyingi anapokutana na wachezaji wa Simba SC kuonyeshwa kadi ya njano.

Hata mchezo uliopita kwenye ligi, Nashon alionyeshwa kadi ya njano aligotea kutumia dakika 45 pekee hakurudi kipindi cha pili.

Viingilio vya mchezo

Mzunguko itakuwa ni 10,000, VIP B itakuwa ni 20,000 na VIP A ni 30,000.Tayari tiketi zinaendelea kuuzwa kwa ajili ya mashabiki kuingia uwanjani kushuhudia burudani.

Ni Uwanja wa Tazania Kwaraa ngoma inatarajiwa kupigwa kwa wababe hawa kuwa uwanjani kusaka tiketi ya kutinga hatua ya fainali.

Mshindi wa mchezo wa Mei 31 2025 atakutana na Yanga SC kwenye fainali ya CRDB Cup. Ikumbukwe kwamba Yanga SC waliifungashia virago JKT Tanzania.

Share this: