- Dakika 21 zaongezwa Uwanja wa KMC Complex msako wa pointi tatu ndani ya uwanja.
- Leonel Ateba atupia kamba mbili kwa mikwaju ya penati mbele ya Mashujaa FC.
- Kibaya awaonyesha ubaya Simba SC kwa bao kali akiwa nje ya 18 akitumia mguu wakushoto.
FADLU Davids, Kocha Mkuu wa Simba SC amewapa pongezi wachezaji kupambania pointi tatu muhimu mbele ya Mashujaa FC kwenye mchezo wa ligi mzunguko wa pili.

Mei 2 2025 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC, Complex ulisoma Simba SC 2-1 Mashujaa FC. Kwenye mchezo huo Mashujaa FC walianza kupata bao la mapema kipindi cha kwanza. Novemba Mosi 2024 ubao wa Lake Tanganyika ulisoma Mashujaa 0-1 Simba SC. Hivyo kwenye dakika 180, Mashujaa FC wamepigwa nje ndani wakipoteza pointi sita mbele ya mnyama.
Fadlu ameweka wazi kuwa mchezo wao dhidi ya Mashujaa FC ulikuwa na ushindani mkubwa na kila timu ilikuwa inahitaji pointi tatu jambo ambalo liliongeza ugumu.
“Ulikuwa ni mchezo mgumu, ninawapongeza wachezaji kwa namna ambavyo walipambana kusaka pointi tatu hili lilikuwa muhimu kwa kuwa hizi ni mbio kwenye ligi kinachohitajika ni ushindi.
“Mashujaa FC walikuwa imara kipindi cha kwanza ila kipa wao alikuwa anapoteza muda mara nyingi kwa kulala na kipindi cha pili hali ilikuwa hivyo hatukupata muda mwingi kucheza kwa kuwa walikuwa wakipoteza muda.
“Kilichotokea kupata pointi tatu ninawapongeza wachezaji wamefanya kazi kubwa katika kupambania malengo, kila mchezo kwetu ni muhimu na tunatambua kwamba ushindani ni mkubwa.”
Ateba afikisha 10, atoa neno
Leonel Ateba mshambuliaji wa Simba ameweka wazi kuwa hesabu kubwa kwenye mechi ambazo wanacheza ndani ya uwanja ni kuvuna pointi tatu kulingana na ushindani uliopo.

Mei 2 2025 Ateba alichaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Mashujaa FC uliochezwa Uwanja wa KMC Complex. Kwenye mchezo huo kipindi cha kwanza ziliongezwa dakika 6 na kipindi cha pili dakika 15 zikifanya jumla dakika 21 kuongezwa kufidia muda uliopotea.
Katika mchezo huo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba SC 2-1 Mashujaa, mabao ya Simba yalitokana na adhabu ya penati yalifungwa na Ateba dakika ya 65 na 90 na bao la Mashujaa FC lilifungwa na Jaffary Kibaya dakika ya 6.

Kibaya alipachika bao hilo akiwa nje ya 18 kwa shuti la mguu wa kushoto baada ya nyota Valentin Noum awa Simba kutoa pasi ambayo ilikutana na Kibaya kwenye njia akaachia shuti la moja kwa moja.
Baada ya mechi 23 safu ya ulinzi ya Simba SC inaruhusu mabao 9 ikiwa ni timu ambayo imefungwa mabao machache ndani ya ligi msimu wa 2024/25.
Ateba amesema kuwa kwenye kila mchezo ambao wanacheza kikubwa ambacho kinatafutwa ni pointi tatu kutokana na ushindani ambao upo.
“Ushindani ni mkubwa na kila mchezo ambao tunacheza ambacho tunahitaji ni pointi tatu, kila timu inapambana kupata pointi nasi tutaendelea kufanya hivyo.”
Ateba amefikisha mabao 10 ndani ya ligi akiwa ni mfungaji namba mbili ndani ya kikosi cha Simba kinara ni Jean Ahoua mwenye mabao 12 na pasi 7 za mabao. Kinara wa utupiaji ni Clement Mzize wa Yanga mwenye mabao 13.
Simba SC penati 12
Simba SC ni timu namba moja kupata penalti ndani ya Ligi Kuu Bara ikiwa imepata jumla ya penalti 12 msimu wa 2024/25 katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Penalti mbili ambazo wamezipata dhidi ya Mashujaa FC Mei 2 2025 zote zikifungwa na Leonel Ateba katika ushindi wa mabao 2-1 Mashujaa FC zinamfanya Ateba kufikisha jumla ya penalti 7 zakupiga akipata sita na kukosa moja huku tano zikifungwa na Jean Ahoua.
Kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa FC mabao yote mawili ya Simba SC yalitokana na adhabu ya penati zinazofikisha penati 12 kwa mnyama ndani ya msimu wa 2024/25 katika ligi.
Mwamuzi wa kati alikuwa ni Kefa Kayombo ambaye alikuwa akisimamia sheria 17 za mpira na kipindi cha pili alimuonyesha kadi nyekundu kipa namba moja wa Mashujaa Patrick Munthali kwa kuwa alionyeshwa kadi mbili za njano kwenye mchezo huo ya kwanza ilikuwa dakika ya 50 na ile ya pili ilikuwa dakika ya 78.
Nafasi ya Simba SC
Simba SC inafikisha pointi 60 ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo na Mashujaa nafasi ya 10 pointi 30 kibindoni. Tofauti yake ni pointi 10 na vinara wa ligi Yanga SC wenye pointi 70 baada ya mechi 26 huku Simba SC ikiwa imecheza mechi 23 bado mechi tatu walingane na mabingwa watetezi wa ligi.
Katika upande wa mabao yakufunga Simba SC imetupia mabao 54 na Yanga SC mabao 68 na hapa tofauti yao ni mabao 14 kwa msimu wa 2024/25.

