- Mabingwa watetezi wa CRDB Federation Cup Yanga kazini dakika 90 kusaka ushindi dhidi ya Stand United, Uwanja wa KMC Complex.
- Khalid Aucho, Pacome hatihati kukosekana kwenye mchezo huo kutokana na kutokuwa fiti.
- Rekodi za wababe hawa kwenye ligi zao ni balaa zito

MABINGWA watetezi wa CRDB Federation Cup, Yanga wanatarajiwa kushuka uwanjani kusaka ushindi dhidi ya Stand United, Aprili 15 2025 kwenye mchezo wa hatua ya robo fainali saa 10:00 jioni.
Mchezo huo wa hatua ya robo fainali unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC Complex ambao Aprili 13 2025 ulitumika kwa mchezo dhidi ya mtani wa jadi, Simba 3-1 Mbeya City.
Hivyo Yanga inayodhaminiwa na SportPesa inaingia uwanjani ikiwa na matokeo ya mtani wake wa jadi Simba kutinga hatua ya nusu fainali. Ni wababe Azam FC hawa walifungashiwa virago mapema na Mbeya City walipokutana Uwanja wa Azam Complex.
WAKALI WA KUCHEKA NA NYAVU
Yanga ndani ya ligi ipo wazi ni namba moja kwenye kucheka na nyavu inakutana na Stand United ambayo mchezo wake uliopita ilipata ushindi dhidi ya Songea United, baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Majimaji ulisoma Songea United 1-2 Stand United.

Prince Dube mwenye mabao 12 ndani ya kikosi cha Yanga ni namba moja kwa kucheka na nyavu ambapo alipachika bao moja kwenye mchezo uliopita dhidi ya Azam FC na aliachaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
WANAKUTANA KWA MARA YA KWANZA 2024/25
Wababe hawa wanakutana kwa mara ya kwanza ndani ya msimu wa 2024/25 kwa kuwa Stand United ilishuka daraja hivyo haishiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo Yanga ipo kwa sasa na ipo wazi kwamba wanatetea na taji la ligi pia.
Kabla ya Stand United kushuka mchezo wa Septemba 16 2018 unaingia kwenye orodha ya michezo ya kukumbukwa kwa kuwa baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Yanga 4-3 Stand United, Alex Kitenge wa Stand United aliandika rekodi yake kufunga hat trick ya kwanza ndani ya ligi mbele ya Yanga.
VIINGILIO
Tayari bei imeshawekwa wazi kwa mashabiki wat imu zote mbili ili kujitokeza kwa wingi kupata burudani hiyo ambapo mzunguko ni 10,000 VIP A 20,000.
NAFASI
Yanga ni vinara ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mechi 25 ni pointi 67 wamekusanya kibindoni na safu ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 64 ikiwa ni safu kali kwenye kumalizia nafasi ambazo zinatengenezwa ndani ya uwanja kwenye ligi.

Kwenye dakika 2,225 ina wastani wakufunga bao moja kila baada ya dakika 35 huku ukuta ukiwa na wastani wakuokota bao nyavuni kila baada ya dakika 225 kwenye mechi za ushindani wakiwa uwanjani kutimiza majukumu yao.
Ukuta wake ni namba mbili ndani ya ligi kuruhusu mabao machache ambayo ni 10, timu namba moja kwenye ligi ambayo imeruhusu mabao machache zaidi kwa sasa ni Simba ikiwa imetunguliwa mabao 8 na yote aliyetunguliwa ni kipa Moussa Camara.
Yanga ilipata ushindi kwenye mechi 22, ilikubali sare dhidi ya JKT Tanzania 0-0 Yanga na mechi mbili ilipoteza dhidi ya Azam FC na Tabora United. Wababe hawa wawili ambao walikomba pointi tatu dhidi ya Yanga kwenye mzunguko wa pili walilipa kisasi.
Yanga ilipokutana na Tabora United ugenini ilipata ushindi wa mabao 3-0 na ilipokutana na Azam FC ilipata ushindi wa mabao 2-1. Ni mchezo wao wa ligi dhidi ya Azam FC waliruhusu bao moja langoni akiwa Djigui Diarra ambaye ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Miloud Hamdi.

Stand United inashiriki Championship ikiwa inapambania kurejea ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika. Baada ya kucheza mechi 26 imekusanya pointi 55 kibindoni.
Safu ya ushambuliaji imetupia jumla ya mabao 42 ukuta umeruhusu mabao 22, ushindi kwenye mechi 17, iliambulia sare kwenye mechi nne na kichapo katika mechi tano ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo.
Ndani ya dakika 2,340 kwenye ligi ina wastani wa kuwa na hatari kufunga kila baada ya dakika 55 ikiwa na wastani wakuruhusu bao moja kila baada ya dakika 106 ni miongoni mwa timu ambazo zimekuwa kwenye mwendo mzuri ndani ya Championship kwa msimu wa 2024/25.
WACHEZAJI WATAKAOKOSEKANA
Kwa Yanga ni kiungo mkabaji Khalid Aucho huyu alipata maumivu kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union uliochezwa Uwanja wa KMC Complex. Alikosekana kwenye mchezo dhidi ya Azam FC ambao ulikuwa ni Dar Dabi Uwanja wa Azam Complex.
Mbali na Aucho, kuna hatihati Pacome akakosekana kwenye mchezo dhidi ya Stand United kwa kuwa alipata maumivu kwenye mchezo dhidi ya Azam FC baada ya kufunga bao alikwama kukamilisha dakika 90 wakiwa ugenini.

