Yanga kwa MkapaYanga kwa Mkapa

WAKATI zikiwa zimesalia saa chache dunia kushuhudia Kariakoo Dabi, sakata limeibuka la kikanuni baada ya Simba kugomea mchezo huo dhidi ya Yanga ambao ulitarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Machi 8 2025 licha ya maandalizi yote kuwa kamili. TPLB imetoa nakala yake kuhusu sakata hilo ikitoa ufafanuni na namna hali itakavyokuwa huku ikiahidi kuwa taarifa ya mchezo itatolewa mapema baada ya uchunguzi kukamilika.

Bacca v Ateba
Bacca akipambana na Ateba kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza, Kariakoo Dabi Uwanja wa Mkapa. Source: Yanga.

Taarifa rasmi imeeleza namna hii: “Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) katika kikao chake cha Machi 8 2025 ilipitia shauri la Klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu ya NBC, (Yanga na Simba ) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo kuanzia saa 1:15 usiku.

“Katika shauri hilo, Klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajawa hapo juu huku pia ikieleza nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya 17:45 ya ligi kuhusu Taratibu za mchezo.

“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo, (ambao walishuhudia tukio hilo) kutuma taarifa za tukio haraka ili hatua zinazostahili kuchukuliwa ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharula cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi.

“Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwemo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, kamati ilibaini kuwa Klabu ya Simba wakati ikielekea kutumia haki yake iliyoainishwa kwenye kanuni 17:45 ya Ligi Kuu haikuwasiliana na ofisa yeyote wa mchezo , timu mwenyeji wala mamlaka ya uwanja kuhusu nia yao ya kufanya mazoezi katika uwanja huo ili maandalizi ya kikanuni yafanyike.

“Katika taarifa hizo, kamati ilibaini pia kuwa walinzi ambao baadhi walifahamika kwa sura kuwa ni wa Klabu ya Yanga walishiriki tukio la kuzuia basi la Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya kanuni ya 17:47 ya ligi kuhusu taratibu za mchezo.

Ahmed Arajiga
Ahmed Arajiga huyu alitangazwa kuwa mwamuzi wa mchezo wa Kariakoo Dabi, Machi 8 2025, Uwanja wa Mkapa.

“Kwa sababu bodi ilipokea taarifa ya ofisa usalama wa mchezo ambayo imeanisha matukio kadhaa yaliyoambatana na tukio hilo la Klabu ya Simba kushindwa kufanya mazoezi na kwamba baadhi ya matukio yanahitaji uchunguzi ambao hauwezi kukamilika kwa wakati , Bodi ya Ligi Kupitia Kamati yake ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo tajwa hapo juu kwa mujibu wa kanuni ya 34:1, (1.3) ya Ligi Kuu kuhusu kuahirisha mchezo ili kutoa nafasi yakupata taarifa zaidi zitakazosaidia kufanya maamuzi ya haki.

“Bodi itatoa taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo na kutangazatarehe ya mchezo huo mapema iwezekanavyo.” 

KIPENGELE KILIANZA USIKU WA MANANE

Kipengele kilianza usiku wa manane baada ya Simba kutoa taarifa kuwa wanagomea mechi kwa kuwa walizuiwa kufanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Mkapa hivyo hawatacheza mchezo wa Machi 8 2025, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, (TPLB) Steven Mguto mapema alibainisha kuwa wanalifanyia kazi suala hilo.

Yanga mashabiki
Yanga mashabiki ambao wamejitokeza Uwanja wa Mkapa, Machi 8 2025 kwa ajili ya Kariakoo Dabi. Source: Yanga.

Ikumbukwe kwamba mchezo wa leo ni mzunguko wa pili baada ya ule wa mzunguko wa kwanza ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Simba 0-1 Yanga ulikuwa unatarajiwa kuchezwa saa 1:15 usiku kwa wababe hawa kukutana uwanjani kusaka pointi tatu muhimu.

Mguto kupitia E FM amesema: “Najua huu mgogoro na sio kitu cha kupuuzwa hivyo tutafanyia kazi kwa naitisha kikao asubuhi cha saa 72 ndiyo kamati ambayo inafanyia kazi kwenye kuendesha ligi hivyo tutafanyia kazi na umma utajulishwa.

“Usiniulize ninafanyia kazi kitu gani mpelelezi huwezi kumwambia kazi yao unaifanyia namna gani, sisi tuna namna yetu, wasubiri ni kitu nyeti sio kitu cha kudharau wanaweza kuwa Simba wanahoja hivyo tutajua. Sisi wakati tunatengeneza kanuni na tukishazipitisha kila mdau anakuwa nazo kanuni.”

YANGA NAO SIO KINYONGE

Taarifa rasmi kutoka Yanga imeeleza kuwa wanatambua mchezo upo na hakuna mabadiliko yoyote yale kwa kuwa kila kitu kimezingatiwa hivyo watapeleka timu uwanjani na hawatambui tarehe nyingine ambayo itapangwa kwa Kariakoo Dabi.

SIMBA NAO WATAO NENO

Ahmed Ally
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba. Source: Simba.

Kupitia kwenye ukurasa rasmi wa Instagram wa Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameandika namna hii: “Ndugu zangu Wanasimba pole kwa usumbufu mlioupata leo.
Niwape pole pia wenzetu waliosafiri kutoka mikoa mbalimbali kuja kuitazama mechi ya leo.

“Muhimu tuelewe kuwa maamuzi yaliyofanywa na viongozi wetu ni kwa maslahi ya klabu yetu na maslahi ya mpira wetu hivyo sisi mashabiki hatuna budi kuyapokea. Tayari mamlaka za mpira wa miguu zimeshatoa taarifa rasmi ya kuahirishwa mchezo huo, hivyo Simba hatuna budi kuheshimu taarifa hiyo na kusubiri taarifa nyingine.

“Wale ambao walishafika uwanjani, nichukue nafasi hii kuwasihi mrudi nyumbani mkawahi kufuturu na wale wa mikoani kama mtaanza safari jioni hii niwatakie safari njema, Mungu awafikishe salama
Lakini msirudi kinyonge kwani haki imeshinda.”

 

Share this: