Aziz KI V ChemaloneAziz KI V Chemalone

KOCHA Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara ambayo ni namba nne kwa ubora dhidi ya Simba unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa. Ni dakika 90 za jasho huku kila timu ikiwa imemkibiza mwenzake eneo lake.

Yanga ni vinara wa ligi wakiwa na pointi 58 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 22 wanatarajiwa kumenyana na Simba iliyo nafasi ya pili ikiwa na pointi 54 baada ya kucheza jumla ya mechi 21 kwenye ligi. Kwenye safu ya ushambuliaji Yanga ni namba moja ikifunga mabao 58 na Simba namba mbili ikifunga mabao 46.

Hamdi Yanga
Hamdi, Kocha Mkuu wa Yanga mchezo wake uliopita ilikuwa Pamba Jiji 0-3 Yanga. Source: Yanga.

Ikumbukwe kwamba mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga, pointi tatu zilielekea Jangwani kwa wababe hao ambao safu yao ya ushambuliaji imefunga mabao 58. Yanga imefungwa mabao 9 na Simba imefungwa mabao 8 baada ya mechi 21.

Hamdi amesema: “Ni matumaini yangu kuwa kesho tutafanya vizuri. Tumefanya maandalizi makubwa ya kutosha kuhimili presha ya Derby. Hatuna wasiwasi na maandalizi yetu, kilichobaki ni kwenda kufanyia kazi kile ambacho tumeandaa kwenye uwanja wa mazoezi.

“Tunaheshimu sana wapinzani wetu, lakini lazima ukweli uwekwe wazi kuwa sisi ni timu bora. Natarajia kuona mchezo wa kimbinu sana, timu zote zina nguvu, timu zite zina dhamira ya kushinda mchezo unaokuja. Nadhani mchezo utakuwa wazi sana kwani kila timu inajiamini.

“Tunatarajia kuona mchezo ambao kila mtu atapambana kwa kila namna. Niseme tu sisi tupo tayari na tupo imara kwa mchezo huo. Wachezaji wote wapo fiti kujiandaa na mchezo, mchezaji pekee ambaye nina wasiwasi nae ni Aziz Ki ambaye alipata shida ya mgongo.

“Siwezi kusema kama atakuwepo au hatakuwepo bado ni 50/50 nafikiri mpaka kesho nitakuwa na majibu sahihi. Hii sio Derby yangu ya kwanza, nimewahi kucheza Derby ambayo ilikuwa na mashabiki tarkibani 120,000. Siwezi kuwa na presha. Isipokuwa tu naheshimu wapinzani wangu, nasubiri tu mchezo mzuri na wa kuvutia. Mashabiki waje kupata burudani wasiwe pia wasije na presha.”

Kocha Msauz wa Simba- Fadlu Davis
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amekiongoza kikosi kwenye mechi 21 msimu wa 2024/25. Source: Simba.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema kuwa wanatambua mchezo utakuwa ni mgumu kwa pande zote mbili lakini wapo tayari kupambana kwa ajili ya kupata pointi tatu kwenye mchezo huo muhimu.

“Hautakuwa mchezo mwepesi hilo tunalitambua hivyo wachezaji wapo tayari na tutaingia uwanjani kwa tahadhari ili kupata pointi tatu muhimu, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.

“Wachezaji wapo tayari na wanatambua umuhimu wa mchezo wetu ndani ya uwanja kikubwa ni utayari na kupambana kupoata pointi tatu ndani ya uwanja.”

SIMBA WAMEKIMBIZWA HAPA NA YANGA

Rekodi zinaonyesha kuwa Yanga ni timu namba moja yenye safu kali ya ushambuliaji ndani ya ligi msimu wa 2024/25 ikiwa imetupia jumla ya mabao 58 baada ya kucheza mechi 22 na washambuliaji wake wawili, Prince Dube na Clement Mzize hawa wote wametupia mabao 10 kila mmoja.

Aziz na Dube
Prince Dube, Clement Mzize washambuliaji wa Yanga wote wametupia mabao 10 ndani ya ligi 2024/25. Source: Yanga.

Kikosi cha Yanga kinachonolewa na Kocha Mkuu, Miloud Hamdi baada ya kucheza mechi 22 kilipata ushindi kwenye mechi 19 kikiambulia sare mchezo mmoja na kupoteza kwenye mechi mbili pekee ambazo ni dakika 180.

Ndani ya dakika 1,980 safu ya ushambuliaji ya Yanga ina wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 34 katika kucheka na nyavu. Ikumbukwe kwamba ilipata ushindi wa mabao 6-1 mbele ya KMC kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa KMC Complex ikiwa ni timu ambayo ilipata ushindi mkubwa kuliko zote mpaka sasa.

Ahmed Arajiga
Ahmed Arajiga mwamuzi wa mchezo wa Kariakoo Dabi Machi 8 2025. Source: Honest Eyes.

Ni Machi 8 2025 wakali hawa wanatarajiwa kukutana ambapo Simba na mwamuzi ni Ahmed Arajiga wao ni mechi 21 walizoshuka uwanjani huku safu ya ushambuliaji ikiwa imetupia mabao 46 na kinara wa utupiaji ni kiungo mshambuliaji Jean Ahoua ambaye katupia mabao 10.

Katika dakika 1,890, Simba ina wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 41 katika kucheka na nyavu. Kwenye mechi zote 21 safu ya ushambuliaji ya Simba ni mchezo mmoja ilikwama kufunga ilikuwa dhidi ya Yanga uliokamilika kwa ubao kusoma Simba 0-1 Yanga lakini katika mechi 20 zote rekodi zinaonyesha kuwa wachezaji wa Simba walifunga.

Vita ni vikali kwa wababe hawa ambao wanasaka taji la ligi lililo mikononi mwa Yanga ambao ni vinara wa ligi wakiwa na pointi zao 58 kibindoni huku Simba nafasi ya pili na pointi 54.

Share this: