Zidane ----Zidane ----

KUMEKUCHA ndani ya ligi namba sita kwa ubora Afrika, Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kila timu kupambana kusaka saini za wachezaji na wengine wakiwa kwenye hesabu za kukutana na Thank You, wababe Yanga, Simba na Azam FC kila mmoja yupo sokoni kupambania kile anachohitaji ndani ya 2025.

Israel
Israel Mwenda mchezaji wa kwanza kutambulishwa Yanga katika dirisha dogo. Source: Yanga.

Ni Israel Mwenda huyu ni mchezaji wa kwanza kutambulishwa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa akiwa hapo kwa mkopo akitokea Singida Black Stars, kuna mastaa kadhaa ambao wanatajwa kuwa huenda wakapata changamoto mpya na wengine wakapewa Thank You.

Hapa tunakuletea baadhi ya tetesi namna hii:-

KIBU DENNIS

Kibu
Kibu Dennis kiungo mshambuliaji wa Simba anayevaa jezi namba 38 kwenye majukumu. Source: Simba.

Mwamba Kibu Dennis mkandaji huyu ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids ambapo inatajwa kuwa kuna timu kutoka Afrika Kusini zinamfuatilia kwa ukaribu kutokana na kiwango chake katika mechi za ushindani.

Ikumbukwe kwamba nyota huyu aliongeza mkataba wa kuitumikia Simba hivyo bado kandarasi yake haijagota mwisho kwa maana hiyo mabosi kutoka Kaizer Chiefs wanaotajwa kuwania saini yake wanapaswa kuvunja akaunti ili kuipata saini yake.

Ndani ya 2024/25 Kibu rekodi zinaonyesha kuwa amecheza mechi 11 akikomba dakika 794 kwenye ligi kati ya mechi 15 ambazo Simba imecheza ikikusanya pointi 40 kibindoni.

FEISAL SALUM

Toto
Fei Toto kiungo mshambuliaji wa Azam FC kwenye majukumu yake. Source: Azam FC.

Ni namba moja kwenye kutengeneza pasi za mwisho ndani ya ligi msimu wa 2024/25 akiwa katoa jumla ya pasi 9 na kufunga mabao manne kati ya 25 yaliyofungwa na Azam FC. Kahusika kwenye mabao 14.

Anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Simba ambao wanahitaji kupata saini ya nyota huyo aliyeibuka viunga vya Azam Complex akitokea Yanga. Dau lake linatajwa kuwa bilioni moja kwa kuwa bado ana mkataba na Azam hivyo Simba wakiwa na mkwanja huo wataipata saini yake.

LADACK CHASAMBI

Wenyewe Simba wanamuita mtoto wa maajabu akiwa kwenye orodha ya nyota wenye rekodi ya kutoa hat trick ya pasi za mabao msimu wa 2024/25 alifanya hivyo kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Kagera Sugar.

Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Kaitaba ilikuwa ni Desemba 21 katika hizo pasi mbili alimpa Steven Mukwala mzee wa Waa na pasi moja ya bao alimpa Fabrince Ngoma.

Huyu anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Kagera Sugar na KMC ambao wanahitaji huduma yake kwa mkopo.

 PHILIPE KINZUMBI

Huyu alikuwa anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Kariakoo Yanga kwenye dirisha kubwa akitokea TP Mazembe dili lake likabuma akaibuka ndani ya Club Africain Tunis ambako yupo kwenye changamoto mpya.

Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Kariakoo wamerejea kwa mara nyingine kusaka saini yake ambapo ni Simba inapewa chapuo kuinasa saini ya nyota huyu raia wa DR Congo mwenye uwezo wa kucheza winga ya kulia na kushoto kwa umakini mkubwa.

YOUB LAKRED

Kipa wa Simba huyu anatajwa kwamba atakutana na Thank You ambapo atarejea Morocco kwa ajili ya kuanza Maisha mapya kutokana na kutokuwa na nafasi kikosi cha kwanza ndani ya Simba.

Lakred hajawa fiti msimu wa 2024/25 baada ya kupata maumivu kwenye maandalizi ya msimu wa 2024/25 akiwa na timu nchini Misri na sasa ni Mousa Camara yeye ni kipa namba moja ndani ya Simba.

AISHI MANULA

Air Manula kipa wa Simba kwa msimu wa 2024/25 katika mechi za ushindani ndani ya ligi hajapata nafasi ya kuanza akiwa shuhuda Mousa Camara kuanza katika kikosi cha kwanza.

Ni mchezo mmoja dhidi ya Al Hilal ambao ulikuwa ni wa kirafiki, Uwanja wa KMC Complex alianza alipokomba dakika 45 nafasi yake ikachukuliwa na Hussen Abel na baada ya dakika 90 ilikuwa Simba 1-1 Al Hilal.

Huyu anatajwa kuwa kwenye mpango wa mabosi wa Azam FC ambao wanahitaji kuipata saini yake kwa mkopo ili kuwa naye ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Dar, Singida Black Stars nao wanatajwa kuwania saini yake.

 GIBRIL SILLAH

Kiungo wa kazi yupo ndani ya Azam FC akiwa na uhakika wan amba kikosi cha kwanza, kwenye mechi 16 ambazo Azam FC imecheza alianza kikosi cha kwanza mechi 14, akifunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao kati ya mabao 25.

Huyu anatajwa kuwa kwenye hesabu za mabosi wa Kariakoo, Yanga ambayo inapewa chapuo kufuatilia saini ya nyota huyu.

SELEMAN MWALIMU

Gomez
Seleman Mwalimu nyota wa Fountain Gate. Source: Fountain Gate.

Yupo ndani ya Fountain Gate ni mkali kwenye kucheka na nyavu akiwa ametupia mabao sita msimu wa 2024/25 ni chaguo la kwanza ndani ya timu hiyo ambayo ipo nafasi ya sita kwenye msimamo na pointi 20.

Anatajwa kuwa kwenye rada za mabosi wa Azam FC huku Yanga na Simba nazo zikitajwa kuipigia hesabu saini ya nyota huyo kuwa katika mitaa ya Kariakoo.

MAKAME LAULIAN

Beki huyu wa Fountain Gate inatajwa kuwa yupo kwenye hesabu za mabosi wa Yanga ambao wanahitaji kuipata saini yake kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho kwenye mechi za ushindani ndani ya uwanja.

JOSHUA MUTALE

Kiungo mshambuliaji wa Simba hajawa kwenye ubora katika mechi za ushindani anatajwa kuwa huenda akatolewa kwa mkopo na mabosi wa Simba ili akaongeze makali yake.

Ni dili la miaka mitatu alisaini Simba na kwenye ligi ni mechi 10 kacheza akikomba dakika 440 hakuna bao wala pasi ya bao aliyotoa.

JEAN BALEKE

Jean Baleke
Jean Baleke mshambuliaji wa Yanga amefunga bao moja ndani ya ligi kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union. Source: Yanga.

Huyu ni mshambuliaji wa Yanga amecheza mechi tano akikomba dakika 188 katupia bao moja ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union ya Tanga.

Anatajwa kuwa atakutana na mkono wa Thank You kwa kuwa hayupo kwenye mpango kazi wa benchi la ufundi la Yanga.

 

ZOUZOU

Matajiri wa Dar, Azam FC wao hawalali, Januari 9 2025 walimtambulisha beki mpya Zouzou Landry aliyekuwa anacheza AFAD Djekanou ya Ivory Coast mwenye miaka minne nyota huyo mwenye miaka 23 anamudu kucheza beki wa kati na kushoto atakuwa hapo mpaka 2028 kwa dili la miaka minne, mwingine ni Zidane huyu yupo ndani ya Azam mpaka 2030 kasaini dili la miaka mitano alitambulishwa Januari 11 2025.

 

Share this: