Aziz KiAziz Ki

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Yanga leo Novemba 30 2024 wanakibarua cha kusaka pointi tatu muhimu kwenye mchezo wa funga kazi ndani ya Novemba wakiwa ugenini, Uwanja wa Majaliwa dhidi ya Namungo saa 12:30 jioni wakiwa na kumbukumbu za kupita dakika 270 zenye ganzi ya maumivu kwenye furaha.

Yanga yenye viungo wa kazi ikiwa ni Clatous Chama, Aziz Ki, inayodhaminiwa na SportPesa kwenye mechi mbili mfululizo za ligi haijawa kwenye mwendo bora kutokana na kukosa matokeo chanya ambapo kwenye msako wa pointi sita iliyeyusha zote uwanjani kwa kuambulia patupu.

Chama
Chama Clatous kiungo wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Ilikuwa Yanga 0-1 Azam FC huu ulichezwa Uwanja wa Azam Complex na Yanga 1-3 Tabora United nao pia ilikuwa palepale, Azam Complex. Sasa Yanga imetangaza rasmi kuhama Uwanja wa Azam Complex na mechi zake za nyumbani itatumia Uwanja wa KMC ambao unatumiwa pia na Simba.

Baada ya mwendo huo wa kusuasua iliachana na Miguel Gamondi ambaye alikuwa mchora ramani wa timu hiyo mikoba ipo mikononi mwa Sead Ramovic raia wa Ujerumani na mchezo wake wa kwanza ilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya dakika 90 ubao ulisoma Yanga 0-2 Al Hilal.

HESABU ZA RAMOVIC DHIDI YA NAMUNGO

Saed Yanga
Saed Ramovic, Kocha Mkuu wa Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Kocha Mkuu wa Yanga Ramovic ameweka wazi kuwa wanakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Namungo hilo lipo wazi lakini watapambana kupata pointi tatu muhimu. Amebainisha kuwa maandalizi yapo vizuri na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ambao utakuwa na ushindani mkubwa na malengo ni kuona wanapata pointi tatu muhimu.

“Tuna mchezo mgumu mbele yetu, katika maandalizi yetu mpaka sasa kila kitu kipo vizuri, tunafahamu Namungo wana wachezaji wazoefu lakini sisi hatupo hapa kutafuta kingine zaidi ya alama tatu.

“Ni jambo la kujivunia kuwa hapa, nawashukuru mashabiki wa Yanga wanaotoka Dar. Mashabiki wamekuwa na moyo kwa kuwa wapo pamoja na timu kila mahali hivyo nasi tunapaswa kuwapa furaha kwa kupata ushindi.”

HUYU HAPA NKANE

Nkane
Nkane Dennis nyota wa kikosi cha Yanga 2024/25. Source: Yanga.

Kwa upande wa nyota wa Yanga, Dennis Nkane amesema kuwa wachezaji wanatambua umuhimu wa mchezo huo na wapo tayari kupata pointi tatu kwa kuwa hicho ni kitu ambacho wanahitaji.

“Sisi wachezaji tunatambua umuhimu wa alama tatu kwenye ligi, tumekaa chini na kuzungumza wapi kwa kuboresha, tunamsikiliza mwalimu na kujituma kwa dhati ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.

“Tunajua kuwa mchezo utakuwa ni mgumu lakini tupo kwaajili ya kupambana na kushinda. Mashabiki wajitokeze kwa wingi kwa kuwa tupo tayari na makosa yaliyopita benchi la ufundi limefanyia kazi.”

MASTAA HAWA KUKOSEKANA

Job
Job beki wa Yanga 2024/25 uzi wake ni namba 5. Source: Yanga.

Kuna baadhi ya wachezaji ambao huenda watakosekana kwenye mchezo wa leo kutokana na sababu mbalimbali hivyo wale ambao watakuwa fiti watabeba mikoba yao kupambania kusaka pointi tatu muhimu ndani ya uwanja.

Miongoni mwa nyota ambao wanatarajiwa kutokuwa kwenye mchezo wa leo ni Ibrahim Bacca ambaye ni beki huyu ana adhabu ya kadi nyekundu ya moja kwa moja aliipata kwenye mchezo dhidi ya Azam FC hakuwa kwenye kikosi mchezo dhidi ya Tabora United.

Mbali na Bacca ambaye kiongozi wao wa safu ya ulinzi ni Dickson Job kiungo Aziz Andambwile naye bado hajawa fiti kama ilivyo kwa Khalid Aucho ambaye huyu ni kiungo mkabaji mwenye uzoefu kitaifa na kimataifa, Clement Mzize naye anaingia kwenye orodha ya nyota ambao huenda wakaukosa mchezo wa leo kwa kuwa hawajawa fiti.

Katika mchezo uliopita wa kimataifa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mastaa hao hawakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga ambacho kilishuhudia ubao ukisoma Yanga 0-2 Al Hilal.

MECHI TATU MAUMIVU

Yanga imecheza mechi tatu mfululizo ikiambulia maumivu kwa kuwa kwenye msako wa pointi tatu ilikwama kushinda zaidi ya kupoteza mechi hizo za ushindani ndani ya 2024/25.

Ilikuwa namna hii: Yanga 0-1 Azam FC na Yanga 1-3 Tabora United mechi hizi mbili zilikuwa za ligi na Yanga 0-2 Al Hilal huu ulikuwa ni mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

MASHUJAA NAO KAZINI

Mbali na mchezo wa Namungo dhidi ya Yanga Uwanja wa Majaliwa kuwa kwenye funga Novemba 2024 kuna wababe wawili wengine watakuwa kazini kwenye msako wa pointi tatu muhimu.

Mashujaa ya mwisho wa reli Kigoma itawakaribisha Kagera Sugar mchezo huu unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma saa 10:00 jioni kwa wababe hao kusaka pointi tatu muhimu na unaweza kubashiri kupitia SportPesa ukavuna mkwanja.

 

Share this: