MABINGWA Yanga msimu wa 2023/24 kwenye Ligi Kuu Bara ikiwa ni taji lao la 30 chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi kwenye anga la kimataifa wameandika rekodi yao kwa kutinga hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi nje ndani dakika 180 huku Coastal Union na Azam FC wakiumaliza mwendo katika mashindano ya kimataifa.
Yanga inayodhaminiwa na SportPesa haikuwa na jambo dogo kwenye mechi zake zote mbili ikishinda zaidi ya mabao matatu kwenye kila mchezo huku wakikomba milioni 50 ikiwa ni zawadi ya goli la mama kwenye ushindi ambao wameupata kwa kuwa kila bao lina thamani ya milioni 5.

Gumzo kubwa limekuwa ni uwezo wa nyota Clatous Chama ambaye katika mechi za kimataifa kafanya kazi kubwa kwa ushirikiano na wachezaji wengine.
Katika zote mbili dhidi ya Vital’O ya Burundi Chama kahusika kwenye mabao sita.
Kazi ilianza Agosti 17 2024 wakati ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Vital’O 0-4 Yanga alifunga bao moja akifikisha mabao 19 kiujumla kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kete ya pili ilikuwa Agosti 24 2024 wakati ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Yanga 6-0 Vital’O alifunga bao moja na pasi nne za mabao akifikisha jumla ya mabao 20 katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
DUBE MUUAJI ANAYETABASAMU

Muuaji anayetabasamu Prince Dube ameweka wazi kuwa furaha kubwa ni kupambana akiwa na uzi wa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ili wafikie malengo yao kitaifa na kimataifa.
Ipo wazi kuwa Agosti 24 2024 wakati ubao wa Uwanja wa Azam Complex ukisoma Yanga 6-0 Vital’O alipachika bao moja huku mabao mengine yalifungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 14 kwa mkwaju wa penalti, Clement Mzize dakika ya 49, Clatous Chama dakika ya 51, Dube alifunga dakika ya 71, Aziz Ki alifunga dakika ya 78 na Mudathir Yahya alifunga bao dakika ya 86.
Ikumbukwe kwamba katika mchezo wa awali Agosti 17 wakati ubao ukisoma Vital’O 0-4, Dube alipachika pia bao moja hivyo ni mabao mawili kafunga kimataifa huku mabao mengine yakifungwa na Chama dakika ya 68, Mzize dakika ya 74, Aziz Ki dakika ya 90 kwa mkwaju wa penalti.
Nyota huyo amesema kuwa furaha kubwa ni kuona wanapata matokeo mazuri kwenye mechi ambazo wanacheza kutokana na ushirikiano ambao unapatikana kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi.
“Ushirikiano ni mkubwa na tunapambana kufikia malengo kikubwa ni kuwa pamoja na malengo ni kuoa tunapata matokeo kwenye mechi zetu tunazocheza.”
AZAM FC NA COASTAL UNION MWENDO WAMEUMALIZA

Azam FC walikuwa wakipeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo kete ya kwanza walianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APR mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex.
Katika kete ya pili wakiwa ugenini, baada ya dakika 90 ubao ulisoma APR 2-0 Azam FC hivyo wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwendo wao wameumaliza mpaka wakati mwingine wakiwa chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo raia wa Senegal.
Ikumbukwe kwamba katika mchezo wa kwanza baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APR mchezo uliochezwa Azam Complex, Dabo aliweka wazi kuwa wanatambua uimara wa APR ni kwenye ulinzi hivyo watafanyia kazi makosa yaliyopita katika mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani.
Kwa upande wa Coastal Union kutoka Tanga wao walikuwa wakipeperusha bendera kwenye Kombe la Shirikisho Afrika ambapo walikuwa wakipambania kete yao kusonga mbele dhidi ya Bravos.
Mchezo wa kwanza walipoteza kwa kufungwa mabao 3-0 ugenini ilikuwa Agosti 17 na kete ya pili wakipambana kupindua meza iligotea matokeo hayohayo kwa ubao wa Uwanja wa Azam Complex, Agosti 25 2024 kusoma Coastal Union 0-0 Bravos.
HAWA WAPINZANI WA SIMBA KIMATAIFA

Simba haikuanza kwenye hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa inasubiri mshindi kutoka katika hatua hiyo kupatikana ili acheze naye na hatimaye imeshamtambua mpinzani wake.
Ni kwenye hatua ya pili katika Kombe la Shirikisho Afrika Simba itacheza na Al Ahly Tripoli ambapo Simba itaanza ugenini mchezo unaotarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 13-15 na ule wa pili unatarajiwa kuchezwa kati ya Septemba 20-22 2024.

