Ahmed SemajiAhmed Semaji
Ahmed Ally
Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari Simba amesema Simba Day ni Ubaya Ubwela.Source: Simba.

SIMBA Day 2024 imepamba moto ikiwa tayari amshaamsha zimeanza kwa mashabiki na viongozi kuelekea kwenye tukio hilo kubwa ambalo linasubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki duniani.

Tukio hilo ni maalumu kwa ajili ya utambulisho wa wachezaji wapya waliosajiliwa na wale ambao walikuwa na kikosi cha Simba msimu wa 2023/24 wakati ikigotea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.

Kwa mujibu wa Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa tukio la msimu huu litakuwa kubwa vibaya mno kutokana na maandalizi mazuri na upekee kwenye kila hatua.

“Ninamuomba Mungu atupe uzima ili tuione Simba Day kwa kuwa ni tukio kubwa na litakuwa la kipekee kweli. Kama mnavyojua kila mwaka tunajaribu kufanya jambo jipya ili kuongeza thamani ya jambo letu itakuwa hivyo msimu huu pia.

SIMBA DAY UZINDUZI WAKE NI HAPA

“Kutokana na umuhimu wa sekta ya utalii pamoja na kuwafikia Wanasimba wengi safari hii uzinduzi wake itakuwa ni Mikumi, Morogoro hapo ndipo tutakwenda. Twendeni Hifadhi ya Mikumi tukawaonyeshe Watanzania kuna hifadhi, ni karibu na kiingilio ni 5,900. Kuna wengine wakisikia utalii wanajua ni mamilioni kumbe ni hela kidogo.

“Lakini pia ni kwenda kutangaza treni mpya ya SGR. Kwanza ni bidhaa mpya ambayo inatakiwa kutangazwa na sisi Simba ndio Wenyenchi tunapaswa kuitangaza.

SAFARI YA MOROGORO RATIBA IPO HIVI

“Safari yetu itakuwa ni Julai 24, 2024 na treni itaondoka Dar saa 12:00 alfajiri, muda wa kufika kituoni ni saa 11:00 alfajiri. Wale wote ambao wanatamani kuungana nasi kuelekea Morogoro kufika kwa wakati. Tutafika Morogoro saa 1:30 asubuhi. Mpaka sasa tumekodi behewa tatu kwa ajili ya Wanasimba na kwa mashabiki wetu hakutakuwa na nauli. Kila shabiki wa Simba ambaye anahitaji kuandika historia kupanda SGR, kufika Mikumi, kushiriki uzinduzi wa Wiki ya Simba afike akiwa na jezi ya Simba.

“Tukifika Morogoro tutakuta Wanasimba wenzetu wamekuja kutupokea. Kwa hili niyashukuru matawi ya Simba Morogoro. Tunataka kwenda kuishangaza Morogoro na ninyi mnatujua sisi sio watu wa kufanya mambo madogomadogo, tunafanya kwa ukubwa wake.

“Na nichukue nafasi hii kuwaambia wakazi wa Morogoro anayekwenda kazini awahi mapema kabla ya saa 1:30 asubuhi maana Mnyama akifika atakuwa mtaani kufanya hamasa zake.

“Tutafanya utalii mbugani na baada ya hapo tutacheza mechi tutarudi Morogoro mjini na kuanza safari kurudi Dar. Hii itakuwa tarehe 24, Julai. “Tutakwenda na kurudi lakini kama ukitaka kulala Morogoro unaruhusiwa. Julai 25 itakuwa mapumziko maana shughuli ya Morogoro itakuwa nzito. Julai 26 itakuwa siku ya droo. Tutakuwa na Simba Week Bonanza ambayo itashirikisha matawi yote ya Simba.

“Bonanza litafanyika kwenye uwanja wa Mwembe Yanga uliopo Temeke. Kutakuwa na michezo mbalimbali, nyama choma na vinywaji. Tawi lolote ambalo linahitaji kushiriki wajiandikishe, tutatoa maelekezo namna ya kujiandikisha.

SIMBA DAY NDANI YA SIMBA WEEK

Awesu Awesu
Awesu Awesu nyota mpya wa Simba. Source: Simba.

“Julai 27 itakuwa Simba Week Bonanza pale Uwanja wa Mwembe Yanga Temeke. Julai 28 tutakuwa Mbagala, huwezi kufanya Simba Week bila kufika Mbagala, tutakwenda kuliamsha. Ndani ya wiki hii tutafanya kwanza burudani, kurudisha kwa jamii.

Ikumbukwe kwamba Simba Day kutakuwa na utambulisho wa wachezaji wapya na miongoni mwao ni pamoja na Awesu Awesu, Kelvin Kijili, Valentino Mashaka huku wale waliokuwa na kikosi miongoni mwao ni Mohamed Hussen, Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin.

SIMBA DAY 2024 VIINGILIO

Mzunguko itakuwa ni 5,000

Machungwa itakuwa ni 10,000

VIP C itakuwa ni 20,000

VIP B itakuwa ni 30,000

VIP A itakuwa ni 40,000

Platinum itakuwa ni 200,000.

“Mwaka huu ni Ubaya Ubwela. Tunakwenda nayo hii tunatambua kwamba kuna mengi yanakuja hivyo mashabiki tuzidi kuwa pamoja na tiketi mapema kila mmoja ajipatie yake kuelekea kwenye Simba Day.”  Ally.

USHINDI WAMEANZA NAO

Ahoua
Ahoua nyota wa Simba jezi namba 10 aishanguilia na wachezaji wenzake: Source: Simba.

Ikiwa ni mchezo wa kwanza wa kirafiki kucheza kikosi cha Simba kikiwa nchini Misri kilianza kwa kupata  ushindi mbele ya El Qanah Egypt kwa mabao 3-0 ilikuwa ni Julai 22 2024.

Mbao ya Simba yalifungwa na Ahoua alifunga mabao mawili dakika ya 14, 16 na Okejepha alitupia bao moja.

Ikumbukwe kwamba hayo ni maandalizi kwa ajili ya msimu wa 2024/25 unaotarajiwa kuanza Agosti 2024. Ni Yanga walitwaa ubingwa msimu wa 2023/24 walimaliza wakiwa nafasi ya kwanza na pointi 80 hawa wana kazi ya kutetea taji lao kwa msimu mpya.

Simba walitwaa taji ya Ngao ya Jamii ambapo wataanzia kwenye hatua ya nusu fainali inayotarajiwa kuchezwa Agosti 8 2024 dhidi ya Yanga, Uwanja wa Mkapa.

 

Share this: