MAFAHARIToto
Azam FC
NYOTA wa Azam FC kikosi kinachonolewa na Kocha Mkuu,Yusuph Dabo. Source:Azam FC.

MAFAHARI wawili wapiganapo kuna mmoja ambaye huibuka mbabe na kubeba pointi za ushindi ambazo zinatokana na sababu mbalimbali. Ipo hivyo pia hata kwenye ulimwengu wa mpira ndani ya uwanja ambapo kwa Bongo msimu wa 2023/24 kulikuwa ni mafahari wawili wanapambana.

Ni kwenye kumaliza nafasi ya pili ndani ya ligi baada ya ubingwa kuwa mikononi mwa Yanga inayodhaminiwa na SportPesa. Azam FC na Simba kwenye mechi za funga kazi walikuwa wanapambania nani atakuwa nani na vita yao ilikamilika kwa mwendo huu:-

MATAJIRI WA DAR AZAM FC

Dabo Masta
Yusuph Dabo, Kocha Mkuu wa Azam FC itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika. Source: Azam FC.

Matajiri hao wa Dar wananolewa na Kocha Mkuu Yusuph Dabo wana kazi kubwa kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye anga la kimataifa ikiwa ni Ligi ya Mabingwa Afrika, (Champions League) ipo wazi kwamba mabingwa watetezi wa taji hilo ni Al Ahly ya Misri.

Al Ahly kwa msimu wa 2023/24 kwenye hatua ya makundi ilifungwa bao moja pekee na Yanga kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa na mtupiaji wa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi ikiwa inadhaminiwa na SportPesa alikuwa ni Pacome Zouzoua.

Hivyo Azam FC inakazi kubwa kusaka rekodi mpya ikiwa ni kutinga hatua ya makundi, robo fainali nusu fainali mpaka fainali kwa kuwa kwenye mpira kila kitu kinawezekana na ukizingatia kwamba miundombinu ya Azam FC inawaruhusu kufanya makubwa zaidi.

WAMEBEBA NAFASI YA SIMBA

Ipo wazi kuwa kukwea pipa kwa Azam FC kwenda kupeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wamebeba nafasi ya Simba iliyofanya hivyo msimu wa 2023/24 ilipogotea nafasi ya pili kwenye ligi na msimu huu imegotea nafasi ya tatu hivyo Simba ikikwea pipa itakuwa ni kwenye Kombe la Shirikisho.

Ipo wazi kwamba kasi kubwa ya Azam FC ilikuwa kwenye kupambania kutwaa taji la ligi ilikwama na kushuhudia Yanga wakitwaa taji hilo wakimaliza msimu wakiwa na pointi 80 baada ya kucheza mechi 30 hivyo juhudi za Azam FC zikagotea nafasi ya pili.

Matajiri hao wa Dar waliipiga bao Simba jumla katika baadhi ya maeneo ikiwa ni kwenye eneo la ushambuliaji na uimara kwenye ulinzi jambo lililowafanya wagotee nafasi ya pili kwa kuwa kila idara walikuwa wakifanana na Simba mwanzo mwisho na wote walikusanya pointi 69.

Azam FC baada ya kucheza mechi 30 ilipata ushindi kwenye mechi 21, sare 6 na ilipoteza jumla ya mechi tatu pekee katika rekodi hizi ngoma ilikuwa ni sawa kabisa na Simba inayonolewa na Kocha Mkuu Juma Mgunda ambaye aliingoza timu hiyo kwenye mechi 9.

Kwenye eneo la ushambuliaji hapa ilikuwa sehemu nyingine ambayo Azam FC waliwapoteza Simba baada ya Azam FC kufunga jumla ya mabao 63 huku Simba safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 59 baada ya kucheza mechi 30 ambazo ni dakika 2,700. Tofauti ya mabao ikiwa ni nne kuweza kulingana nao na kwenye ukuta Azam FC iliruhusu mabao 21 huku Simba wakiruhusu mabao 25.

MITAMBO YA MABAO KWA WABABE HAO

FEI Toto
FEI Toto kiungo mshambuliaji wa Azam FC mwenye mabao 19 ndani ya ligi 2023/24. Source: Azam FC.

Ni Feisal Salum kiungo mshambuliaji wa Azam FC ni namba moja kwa kutupia nyavu Azam FC akifunga mabao 19. Ipo wazi kwamba Feisal alikuwa anawania tuzo ya kiatu bora pamoja na Aziz KI mwisho alipotezwa na kiungo wa Yanga ambaye alifunga jumla ya mabao 21.

Saido
Saido Ntibanzokiza kiungo mshambuliaji wa Simba ndani ya ligi katupia mabao 11. Source: Simba.

Kwa upande wa Simba mkali wao ni Saido Ntibanzokiza ambaye katupia mabao 11 msimu wa 2023/24. Kwa msimu wa 2022/23 Ntibanzokiza alikuwa ni namba moja kwa watupiaji pia upande wa Simba alitupia mabao 17 sawa na Fiston Mayele aliyekuwa ndani ya kikosi cha Yanga.

FEI NA TUZO

Feisal baada ya kupishana na tuzo ya ufungaji bora kwenye ligi msimu wa 2023/24 alibainisha kuwa yote ni kheri huku akimpa pongezi nyota aliyetwaa tuzo hiyo ambaye ni Aziz KI wa Yanga anayevaa jezi namba 10 mgongoni.

Fei alikuwa anapambania tuzo ya kiatu cha ufungaji bora ambacho kipo mikononi mwa Aziz Ki, kiungo mshambuliaji wa Yanga aliyefunga jumla ya mabao 21 na pasi 8 akihusika kwenye jumla ya mabao 29 kati ya 71 yaliyofungwa na timu hiyo.

Kwa upande wa Fei ni jumla ya mabao 19 kafunga katika hayo 17 kafunga akiwa ndani ya 18 huku mawili akifunga akiwa nje ya 18. Hat trick ilikuwa moja kwenye mchezo dhidi ya Tabora United, Uwanja wa Azam Complex.

Kahusika kwenye mabao 26 kati ya 63 yaliyofungwa na timu hiyo iliyogotea nafasi ya pili na pointi 69 ikiwa na uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/25.

Fei amesema: “Tunafurahi kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ilikuwa ni kazi kubwa kwa kila mchezaji kushirikiana. Tunaamini kwamba tutafanya vizuri wakati ujao na ushirikiano utazidi kuimarika.”

 

 

Share this: