KOCHAsimbasctanzania------------------------------------------
Fred Michael
Fred Michael mshambuliaji wa Simba akiwa kwenye mazoezi ndani ya uwanja. Surce: Simba

MRITHI mikoba ya Baleke Jean unyamani Simba aliyekutana na mkono wa asante kwenye dirisha dogo msimu wa 2023/24 amekingiwa kifua na uongozi wa timu hiyo kwa kubainisha kwamba akipewa muda atafanya makubwa.

Ipo wazi kuwa ni Michel Fred ambaye Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba hupenda kumuita fungafunga alikuwa ni mrithi wa Baleke ndani ya kikosi hicho cha Simba.

Baleke wakati anaondoka Simba alikuwa amefunga jumla ya mabao 16 kwenye ligi msimu wake wa kwanza ilikuwa ni msimu wa 2022/23 ambapo alifunga mabao 8 na msimu wa pili ilikuwa ni msimu wa 2023/24 alitupia mabao 8.

FUNGAFUNGA NDANI YA JUMBA

Fred kwa sasa yupo ndani ya kikosi cha Simba akipambana kutimiza majukumu yake kwa ushirikiano na wachezaji wengine katika kikosi hicho ikiwa ni pamoja na Clatous Chama, Saido Ntibazokiza, Ayoub Lakred.

BENCHIKHA
KOCHA Mkuu wa Simba, Benchikha. Source: Simba

Licha ya kwamba yeye ni mshambuliaji bado hajawa chaguo la kwanza chini ya Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha kwenye mechi za ushindani ambapo mara nyingi amekuwa akianzia benchi na wakati mwingine alipoanza kipindi cha kwanza alikwama kukamilisha dakika 90.

Miongoni mwa mchezo aliokwama kukamilisha dakika 90 ilikuwa ni ule wa ligi dhidi ya Ihefu uliochezwa Uwanja wa Liti ambapo alikomba dakika 45 kwenye mchezo huo.

Nafasi yake ilichukuliwa na Pa Jobe ambaye alikamilisha dakika 45 wakati ubao uliposoma Ihefu 1-1 Simba walipogawana pointi mojamoja ndani ya dakika 90 kwenye mchezo huo wa ligi.

Ni Chama alifunga bao la usawa kwa Simba kwa pigo la penalti iliyosababishwa na mwamba Kibu Dennis ambaye kafunga bao moja ndani ya ligi kwa msimu wa 2023/24.

Katika mchezo wa Kariakoo Dabi, Fred alifunga bao moja akitokea benchi ilikuwa dakika ya 73 alimpa tabu Djigui Diarra akitumia pasi ya Chama kwenye mchezo huo ambao Simba ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.

Nyota huyo amesema: “Wachezaji tunatambua kwamba mashabiki wanapenda matokeo mazuri hilo lipo wazi hivyo tunawaomba wazidi kuwa pamoja nasi kwenye mechi zetu zote ambazo tunacheza tunaamini tutapata matokeo mazuri,”.

MWENDO WA SIMBA KWENYE LIGI

Mwenda Israel
Mwenda Israel beki wa Simba akiwa kwenye mazoezi na wachezaji wenzake: Source: Simba

Simba ndani ya ligi Simba imekuwa kwenye mwendo wa kusuasua katika kupata matokeo yake licha ya kwamba ipo ndani ya tatu bora baada ya kucheza jumla ya mechi 21.

Timu hiyo imekuwa na ukuta ambao una wastani wa kuruhusu bao moja kila baada ya dakika 90 kwa kuwa ni mabao 21 imefungwa mpaka sasa kwenye ligi ikiwa namba moja kwa timu iliyoruhusu mabao mengi ndani ya tatu bora.

Miongoni mwa wachezaji wanaounda ukuta ni Israel Mwenda, Shomari Kapombe, Henock Inonga, Che Malone, Zimbwe kwaupande wa ukabaji ni Sadio Kanoute, Fabrince Ngoma.

Pointi zake ni 46 tofauti ya pointi 13 na vinara wa ligi Yanga inayodhaminiwa na SportPesa ikiwa na jumla ya pointi 59 kibindoni baada ya kucheza mechi 23 kwenye ligi.

NENO LA SEMAJI ALLY

Kutokana na mwendo wa mshambuliaji huyo kwenye mechi za ushindani Ahmed Ally amebainisha kwamba Fred ataonyesha makubwa na kuwafikisha kwenye kilele cha mafanikio kwa ushirikiano na wachezaji wengine.

“Wakati mwingine Matokeo yasiyoridhisha ya timu huwa yanafifisha ubora wa mchezaji mmoja mmoja au matokeo mazuri ya timu hua yanaficha madhaifu ya mchezaji mmoja mmoja.

“Fredy Michael Fungafunga tangu amewasili Simba Sports amefunga jumla ya mabao 10 katika mashindano yote aliyoshiriki ni wastani mzuri sana kwa mshambuliaji.

“Champions League 1, ligi kuu ya NBC 4, Kombe la CRDB 4, Kombe la Muungano 1. Imani yangu ni kwamba kadri anavyopata muda wa kucheza, kadri anavyoaminiwa ndivyo anathibitisha ubora wake.

“Kwetu sisi Wana Simba jukumu letu ni kumuunga mkono mshambuliaji wetu na tukumbuke ya kwamba hii ndio nafasi ngumu zaidi kwenye mpira duniani kote.

“Kwa alichokionesha Fredy hatuna budi kusimama nae ili atufikishe kwenye kilele cha mafanikio,”.

MABAO MANNE TU

Kwa mwend ambao anakwenda nao mwamba Fred ni mabao manne amebakisha kufikia rekodi ya Baleke ambaye alifunga mabao hayo kabla ya kupewa mkono wa asante ili akapate changamoto mpya.

Simba safu yake ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao 41 na katika hayo mkali wa kutengeneza pasi za mwisho ni Chama ambaye ametoa jumla ya pasi sita na amefunga mabao saba kwenye ligi.

Hivyo Chama katika kikosi cha Simba amehusika kwenye mabao 12 na bado ligi haijagota mwisho ikiwa atapata nafasi kwenye mechi zinazofuata kuna uwezekano akaendelea kutoa pasi za mabao ama kufunga sawa na Fred ambaye yeye ni mshambuliaji halisia.

Share this: