
TAARIFA kutoka vyanzo vya habari nchini Misri vimeripoti kuwa klabu ya Pyramids inajiandaa kuwasilisha ofa mezani kwa kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki.
Aziz Ki ambaye mkataba wake wa awali na Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya SportPesa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu, inaelezwa tayari amesaini mkataba mpya wa miaka mitatu ndani ya kikosi cha Yanga.
Nyota huyo wa kimataifa wa Burkina Faso mwenye uimri wa miaka 28, amekuwa na nyakati bora msimu huu akiwa na Yanga ambapo mpaka sasa amefanikiwa kuwa na mchango wa mabao 22 kwenye Ligi Kuu Bara akifunga mabao 15 na kuasisti mara saba.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa sasa Aziz Ki ndiye kinara wa ufungaji akifuatiwa na swahiba wake wa zamani Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye kwenye kikosi cha Azam amefanikiwa kuhusika kwenye mabao 19.
AZIZ KI AZUA GUMZO AFRIKA

Ukiachana na mashindano ya Ligi Kuu Bara, Aziz Ki pia alikuwa nguzo kubwa ya Yanga katika ushiriki wao wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo nyota huyo aliisaidia kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia.
Kwenye mashindano hayo Aziz Ki pia alifanikiwa kuhusika kwenye mabao manne akifunga mara mbili na kuasisti mabao mawili huku akiibuka kuwa gumzo kubwa katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali baada ya kupiga mpira ambao ulizua mjadala mkubwa ikiwa umevuka, au haujavuka mstari wa goli kabla ya kukataliwa na wasimamizi wa mechi na VAR.
VIGOGO AFRIKA VYAGOMBANIA SAINI YAKE
Ukiachana na Pyramids, timu nyingi kubwa vigogo Afrika vimeonyesha nia ya kuisaka saini ya kiungo huyo ambapo mpaka sasa timu kama Mamelodi Sundowns, Zamalek SC, Al Ahly SC, Raja Athletic Club pamoja na Orlando Pirates pia wanasemekana kuuliza kuhusu upatikanaji wa kiungo huyo.
Kwa sasa Pyramids, inayonolewa na kocha Mcroatia, Krunoslav Jurcic inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Misri hii ni baada ya kufanikiwa kukusanya pointi 32 katika michezo yao 15 ya kwanza.
Inaelezwa sehemu kubwa ya maskauti kutokea Afrika Kaskazini walikuwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumamosi kwa ajili ya kumfuatilia nyota huyo katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo ambao uliishuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Matokeo hayo yamewafanya Yanga wazidi kujiweka kwenye nafasi nzuri katika mbio za ubingwa, kwani Yanga kwa sasa imefanikiwa kukusanya pointi 58 baada ya kucheza michezo 22 huku watani zao wa jadi hao wakisalia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 46.
AZIZ KI NA MAYELE

Ikiwa Pyramid watafanikiwa kumsaini Aziz Ki, basi nyota huyo atakuwa anapata nafasi ya kukutana na rafiki yake straika raia wa DR Congo, Fiston Mayele ambaye wamewahi kucheza wote kwenye kikosi cha Yanga kwa kipindi cha misimu miwili kabla ya Mayele kutimkia Pyramids.
Mayele aliuzwa kutokea Yanga mwanzoni mwa msimu huu ambapo inaelezwa Yanga walivuna kiasi kinachokadiriwa kuwa ni zaidi ya Shilingi Bilioni 2 za Kitanzania.
Wakiwa Yanga pacha hiyo ilikuwa hatari kwenye kufumania nyavu kiasi cha Mayele kuibuka mfungaji bora msimu uliopita wa 2022/23 akifanikiwa kufunga mabao 16 sawa na Saido Ntibazonkiza wa Simba ambaye pia alifunga idadi hiyo ya magoli.
KABLA YA YANGA AZIZ KI ALITOKEA WAPI?
Ikumbukwe kuwa nyota huyu alijiunga na Yanga kutokea ndani ya kikosi cha ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambayo aliichezea kwa mafanikio makubwa akifanikiwa kuipa ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na kutajwa kama mchezaji ghali zaidi katika ligi hiyo.
ANAIONEA SIMBA!
Tangu ajiunge na Yanga kutokea nchini Ivory Coast nyota huyo amekuwa na wastani mzuri wa kuifunga Simba, ambapo kwa ujumla mpaka sasa amefanikiwa kucheza michezo nane dhidi ya Simba kwenye mashindano yote, ambapo mara baada ya kuwafunga tena Jumamosi amefanikiwa kufikisha idadi ya mabao matano aliyoifunga Simba tangu walipokutana kwa mara ya kwanza wakati huo akiwa bado ndani ya kikosi cha ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Kabla ya kuvaa jezi za kijani na njano za Yanga, nyota huyo alihusihwa kwa karibu na mpango wa kujiunga Simba.

