- Kariakoo Dabi joto linazidi kupanda kwa kasi kila pande
- Tambo zatawala kila kona kubainisha kwamba ushindi ni lazima ndani ya dakika 90
- Azam FC wabanana na Mashujaa kwenye ligi, Namungo wapeta nyumbani
KARIAKOO Dabi joto linazidi kupanda kuelekea Aprili 20 2024 huku ushindani ndani ya ligi nao ukizidi kuwa wa moto kwa kila timu kupata kile inachostahili baada ya dakika 90 kwenye mechi ambazo wanacheza msimu wa 2023/24.

Ikumbukwe kwamba Yanga inayodhaminiwa na SportPesa inatarajiwa kuwakaribisha Simba kwenye mchezo wa ligi mzunguko wa pili ambapo timu hiz zote zinapiga hesabu ya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara huku mabingwa watetezi wakiwa ni Yanga.
Ipo wazi kwamba Aprili 17 kuna mechi za mzunguko wa pili ziliendelea kuchezwa ambapo matajiri wa Dar, Azam FC walikuwa kazini na mwisho waliambulia pointi moja mbele ya Mashujaa ambao waliwafungashia virago Simba kwenye hatua ya 16 bora CRDB Federation Cup.
HAYA HAPA MATOKEO YA MECHI

Kwenye mchezo dhidi ya Azam FC iliyo nafasi ya pili ikiwa nyumbani baada ya dakika 90 ubao wa Azam Complex ilikuwa ni Azam FC 0-0 Mashujaa kwenye mchezo wa mzunguko wa pili.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC isalie nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 51 huku Mashujaa ikiwa nafasi ya 14 baada ya kukusanya jumla ya pointi 22 na timu hizi zote zimecheza jumla ya mechi 23 za ligi.
Wakati Azam FC wakitoshana nguvu na Mashujaa wakiwa nyumbani, Namungo hawakufanya ajizi mbele ya Coastal Union walikomba pointi zote tatu mazima kwenye mchezo wao wa ligi.
Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Namungo 1-0 Coastal Union, Uwanja wa Majaliwa na mtupiaji bao la ushindi alikuwa ni Hassan Kabunda dakika ya 8 lilidumu mpaka mwisho wa mchezo huo.
Tabora United 0-3 Kagera Sugar watupiaji wakiwa ni Moubarack Amza dakika ya 24, Obrey Chirwa dakika ya 48 na Mbaraka Yusuph dakika ya 72 mchezo huu ulichezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
KARIAKOO DABI HOMA
Yote yanaendelea kwenye ligi huku homa ya Kariakoo Dabi ikizidi kupanda kwa kila timu kuwa chimbo kufanya maandalizi kuelekea mchezo huo unaosubiriwa kwa shauku kubwa na mashabiki wa timu zote mbili Yanga na Simba.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amebainisha kwamba wapo tayari kuelekea mchezo huo na wanawaheshimu wapinzani wao Simba kutokana na uimara walionao pamoja na kuwa na wachezaji wenye uzoefu.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu Simba kuelekea kwenye mchezo wetu wa mzunguko wa pili ni moja ya timu bora na ina wachezaji wenye uzoefu hivyo tutafanya kazi kubwa kupambana kupata matokeo.
“Kikubwa ambacho tunakifanya kwa wakati huu ni kuwa tayari kuelekea mchezo huo yale yaliyopita kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza tunasahau na huu ni mchezo mwingine na tunaamini kwamba kila mmoja anatambua kwamba huu ni mchezo mkubwa.
“Wachezaji wanatambua kazi ni kubwa na sisi viongozi tunatambua hilo ndio maana imekuwa ni kazi kwetu kufanya maandalizi mazuri, mashabiki wajitokeze kwa wingi kushuhudia burudani,”.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kwamba mchezo huo ni muhimu kupata matokeo mazuri ili kurejea kwenye ubora.
“Timu haijawa na matokeo kwenye mechi zake za hivi karibuni hilo linaumiza lakini tupo tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Yanga, tunawaheshimu na tupo tayari,”
KARIAKOO DABI WALIFUNGA
Kweye mchezo wa mzunguko wa kwanza baada ya dakika 90 Novemba 5 2023 ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 1-5 Yanga hawa hapa walikuwa wafungaji kwenye mchezo huo:-
Kennedy Musonda
Huyu alifunga bao la kwanza kwa Yanga ilikuwa dakika ya tatu akiwa ndani ya 18 kwenye mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa.
Maxi Nzengeli
Kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza mwamba alitupia jumla ya mabao mawili akiwa ni nyota aliyefunga mabao mengi zaidi katika mchezo huo na mpaka sasa kafuga jumla ya mabao 9 kwenye ligi.
Aziz KI
Kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi alifunga bao moja na mpaka sasa ana jumla ya mabao 14 kibindoni akiwa ni namba moja kwa mastaa wenye mabao mengi zaidi ndani ya Kariakoo Dabi.
Pacome
Pacome alipachika bao moja kwa mkwaju wa penalti kwenye mchezo wa Karikoo Dabi akikamilisha bao la tano mbele ya Simba akiwa kafunga jumla ya mabao 7 kwenye ligi msimu wa 2023/24.

Kibu Dennis
Novemba 5 2023 ilikuwa chungu kwa Simba walipopoteza pointi tatu mazima, bao pekee la Simba lilifungwa na Kibu Dennis ambaye alikwama kukamilisha dakika 90 baada ya kupata maumivu kwenye mchezo huo.

