- Mnyama Simba ana hesabu nzito kuelekea Kariakoo Dabi Aprili 20 2024 Uwanja wa Mkapa
- Mnyama kaweka kambi Zanzibar kujifua kumkabili mtani Yanga
- Aziz KI ana balaa zito kwa mguu wake kushoto itafahamika

MNYAMA Simba kuelekea mchezo wao wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga ameweka wazi kuwa hesabu nzito ni kufanya mabadiliko kwenye kila idara kabla ya kuwakabili wapinzani wao kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa msimu wa 2023/24.
Ipo wazi kwamba Simba inakwenda kukutana na Yanga inayodhaminiwa na SportPesa kwenye mchezo wa mzunguko wa pili wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wao wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Mnyama Simba katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 ubao ulisoma Simba 1-5 Yanga ambapo ni Yanga walianza kufunga dakika ya tatu kupitia kwa mshambuliaji wao Kenedy Musonda na Simba ilipata bao pekee la kufutia machozi kupitia kwa Kibu Dennis.
Pointi tatu Simba waliziacha mazima kwa Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu Miguel Gamondi ambapo zama hizo Mnyama alikuwa anafundishwa na Roberto Oliveira raia wa Brazil ambaye alikutana na mkono wa asante.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa ni lazima wafanye mabadiliko makubwa kuelekea mechi zinazofuata za mashindano kwenye ligi ili kuwa na mwendelezo mzuri.
HUYU HAPE SEMAJI

“Tumekuwa kwenye mwendo ambao hatuufurahii kutokana na matokeo ambayo tunayapata lakini kikubwa ni kuona kwamba tunafanyia kazi makosaambayo yamepita katika michezo iliyopita ndani ya ligi ili kuwa bora.
“Ushindani ni mkubwa na kila timu inahitaji kufanya vizuri hilo tunalitambua ambacho tunakifanya kwa sasa ni kuendelea kuimarisha yale ambayo yalikuwa ni mapungufu yetu kwenye mechi zilizopita na tunaona kwamba kila kitu kinakwenda vizuri kwa upande wa wachezaji.
“Kuwa na matokeo yasiyofurahisha inaumiza vibaya mno na hakuna ambaye anafurahia mwendo huu hivyo mashabiki ni muhimu kuendelea kuwa pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupata matokeo mazuri inawezekana kwa kuwa wachezaji wapo tayari na benchi la ufundi linfanyia kazi makosa,”.
MATOKEO YAKE YALIYOPITA
Timu hiyo mchezo wake uliopita wa ligi ilishuhudia ubaowa Uwanja wa Liti baada ya dakika 90 kukamilika ukisoma Ihefu 1-1 Simba. Hivyo wakiwa ugenini waligawana pointi mojamoja kwenye mchezo wao wa ligi.
Bao la Simba lilifungwa na kiungo mshambuliaji Clatous Chama kwa mkwaju wa penalti akifikisha mabao sita ndani ya ligi sawa na pasi sita ambazo ametoa kwa msimu wa 2023/24.
Ikumbukwe kwamba mchezo huo walikuwa ugenini na wanakwenda kuwakabili Yanga wakiwa ugenini kwa mara nyingine tena kwenye msako wa pointi tatu nyingine uwanjani.
WATANI WANAPETA

Wakati Simba ikitoka kugawana pointi mojamoja ugenini, watani zao wa jadi Yanga mchezo wao uliopita ilikuwa ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate walipokomba pointi tatu mazima.
Baada ya dakika 90 ubao ulisoma Singida Fountain Gate 0-3 Yanga ambapo mabao yalifungwa na nyota wawili Joseph Guede aliyefunga mabao mawili na Aziz KI aliyefunga bao moja akiwa nje ya 18.
Bao la Aziz KI linamfanya afikishe jumlaya mabao 14 akiwa ni namba moja kwa wakali wa kucheka na nyavu ndani ya Yanga na Ligi Kuu Bara kiujumla kutokana na kasi hiyo ambapo amefunga mabao 12 kwakutumia mguu wa kushoto na mabao mawili kwa mguu wake wa kulia.
SIMBA NDANI YA ZANZIBAR
Kikosi cha Simba kinachonolewana Kocha Mkuu Abdelhak Benchikha kimeweka kambi Zanzibar kwa ajili ya mchezo wao ujao dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.
Mapema Aprili 16 msafara wa Simba uliwasili Zanzibar na kuanza mazoezi kuelekea mchezo wao dhidi ya Yanga ambao joto lake limezidi kuwa kubwa kwa sasa kwa kila timu kupiga hesabu za kupata pointi tatu.
Simba inatambua umuhimu wa pointi tatu na Yanga pia inatambua umuhimu wa pointi tatu kwenye mchezo huo jambo ambalo linafanya kila timu kupambana kuwa imara kuelekea kwenye mchezo huo.
Ni Simba ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 20 na pointi zake kibindoni ni 46.
Imeachwa kwa pointi 9 na watani zao wa jadi Yanga ambao wao wamekusanya jumla ya pointi 55 kibindoni.

